Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati

Hon. Ester Michael Mmasi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati

MHE. ESTER M. MMASI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Bunge lako Tukufu. Kabla sijaenda mbali napenda kumpongeza sana Waziri mwenye dhamba Dkt. Kalemani pamoja na dada yetu mpendwa dada Subira, kazi zenu zinaonekana. Mimi nimekuwa nikitembea mikoa mbalimbali kuongea na vijana wa vyuo vikuu, wengine wamediriki kuniambia kwamba wazee wao wamefika hata kuwasahau watoto wa majirani lakini majina yenu nyuso zenu wanazijua fika. Mmetembea Tanzania mmezunguka mikoa yote vijiji kwa vitokoji. Tunawapa pongezi za dhati kwenye hili la kusimami sekta ya nishati msiyumbe kwa kweli mpo vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nitajikita kwenye taasisi moja tu ya TPDC. Sambamba na pongezi zangu kwa Wizara na viongozi wa Wizara lakini pia ninapenda kwa namna ya pekee nimpongeze Engeneer Msomba pamoja na timu yake, mwenyekiti wa bodi Bakukula lakini pia wadada watatu ambao wameonekana kujituma sana katika taasisi ya TPDC nanyi pia mpokee pongezi za za dhati. Ninamfahamu Venosa lakini pia ninamfahamu Dorah, ninamfahamu Maria. Kwa kweli sisi kama wanawake vijana tunawapongezini sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, TPDC kwa miaka ya nyuma ulikuwa ukiitaja hapa Bungeni, nafikiri hata kama michango ukiipata ni michango dhaifu, kwa sababu kila mtu alikuwa ame-tend ku-withdraw, hakuna mtu mwenye hamu ya kutaka kuisikiliza TPDC ni nini, lakini, kwa heshima na taadhima napenda kuipongeza Taasisi hii ilienda ikajitafakari ikaja na turnaround strategy na leo ninathubutu kutaja mafanikio makubwa yaliyopatikana kwenye Taasisi hii ya TPDC. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kupitia Gesi ya Kinyerezi I na II, TPDC imeweza kufanya mambo makubwa katika nchi hii, umeme viwandani, kwa sasa Dangote analipa shilingi bilioni tano za Kitanzania kila mwenzi, lakini siyo hivyo Goodwill Ceramic analipa 2.2 bilioni kwenye uchumi wa Tanzania kutokana na Kinyerezi I na II. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Cocacola juzi amepewa umeme wa gesi, analipa shilingi milioni 150 kwa mwezi, ninapoongea hapa Lodhia Steel, lakini pia NAF Industries leo hii wanaenda kulipa shilingi milioni 512 kwa mwezi kwa sababu ya gesi ya Kinyerezi I na II. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambasamba na haya, TANESCO kwa mara ya kwanza kabisa na nitaomba ikikupendeza wenzetu hawa waweze kutafakari ni nini walichokiandika katika ukurasa wa sita kwa sababu wametuambia bado kwamba TANESCO inalipa capacity charge, huu ni uongo na ni upotoshaji mkubwa, nitaomba niweke rekodi hizi vizuri katika Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapoongea hapa kwa mara ya kwanza tumeondokana na capacity charge za Aggreko, tumeondokana na capacity charges za Artumas, tumeondokana na capacity charges ambazo tulikuwanazo kwenye Richmond saga katika Bunge lako hili Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Hizi ni pongezi za hali ya juu, sisi ni waumini katika...

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

MBUNGE FULANI: Hebu endelea.

MBUNGE FULANI: Endelea.

MBUNGE FULANI: Endelea.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mmasi kuna taarifa. Mheshimiwa Mwakajoka.

T A A R I F A

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kumpa taarifa mchangiaji, anasema tumeondokana na TANESCO, wameondokana na capacity charge wanazotoa kwenye makampuni yanayowauzia umeme, si kweli, anazungumzia capacity charge zinazoondolewa kwa wateja wadogowadogo, lakini TANESCO bado wanalipa capacity charge wanakonunua umeme kwenye makampuni mbalimbali, kwa hiyo anachoongea ni uongo kabisa huyo. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa pamoja na kwamba unachotoa ni taarifa Kanuni uliyotumia siyo, kama unaona anasema uongo, ungetumia Kanuni ya 63 ama 64. Mheshimiwa Ester Michael Mmasi.

MHE. ESTER M. MMASI: Mheshimiwa Naibu Spika, utamaduni na utaratibu wa Bunge lako tukufu ikiwa Mbunge anapotosha, ni sharti alete kithibitisho, niko radhi kuleta uthibitisho kwenye Bunge lako tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, capacity charge aliyokuwa analipwa na Serikali, shilingi bilioni 6.9 imeondoka kwenye mahesabu ya TANESCO na huo ni uthibitisho tosha, data ninazo lakini haitoshi, mimi niko pamoja na wengine huko kwenye Kambi yenu, tunahudumu Kamati moja, haya masuala tunaongea kwenye Kamati, kwa nini nidanganye leo hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, asinipotezee muda, naikataa taarifa yake, Sambamba na matokeo chanya haya, lakini leo hii kwa mara ya kwanza mwaka wa tatu leo, TANESCO imeondokana na ruzuku ya bilioni 143 iliyokuwa inalipa kwa mwaka. Haya ni mafanikio makubwa, hakuna wa kubeza katika hili, sisi ni waumini wa maendeleo ya Taifa hili, sisi ndiyo wabeba Ilani wa Taifa hili tupeni nafasi tufanye kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza sana TPDC, naupongeza uongozi, ampongeza Waziri na Naibu Waziri, kazi inaonekana, leo TPDC ina rekodi faida ya shilingi bilioni 9.57 na mpango wa miaka ijayo tunaenda kurekodi bilioni 59 na huu ni mpango wa miaka mitatu ijayo ni nani wa kubeza katika hili. Uthibitisho ninao, nitaleta mkinitaka nilete katika Bunge hili, TPDC kwa turnaround strategy imeenda kufanya mabadiliko makubwa sana kwenye sekta ya nishati ya gesi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu nitapenda niongelee Sheria ya Mafuta na Gesi, ya mwaka 2015, Sheria namba 21. Katika Sheria hii niseme tu kwamba nafikiri Wizara ipate muda iweze kufanya rejea na kuondokana na yale masharti hasi, ambayo yako katika ile sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii TPDC sharti la kwanza katika ile sheria inaitaka TPDC ifanye kazi kibiashara, ijiendeshe kibiashara, irekodi faida, lakini sharti lililowekwa katika sheria ile wanasema kwamba raslimali ya gesi na mafuta irudi Serikalini. Leo TPDC akitaka kununua mitambo, either katika kufanya utafiti wa upper stream or downstream ama katika kununua mitambo ya kusafirisha gesi itapaswa kupita kwenye utaratibu wa Kiserikali kuandika minute sheet, kuandika folios iende kwenye Cabinet Ministers ndiyo waweze kupata approval. Kwa sharti la kisheria kwamba hii TPDC iweze kujiendesha Kibiashara, nafikiri ni muhimu sana, Wizara ikaona umuhimu wa kuondokana na hizi red tapes hazitatusaidia. (Makofi)

Mheshishimiwa Naibu Spika, sambasamba na takwa hili la kisheria...

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ester Mmasi kuna taarifa. Mheshimiwa Salome Makamba.

T A A R I F A

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Mimi napenda kumpa taarifa ndugu yangu Mheshimiwa Ester Mmasi kwamba taarifa zinazotolewa kwenye ripoti ya Kambi zinatokana na sources ambayo mojawapo ni ripoti ya CAG. Sasa tunaomba utufahamishe, hicho unachokisema unakitoa wapi? Usije ukawa unatulisha matango pori humu.

MBUNGE FULANI: CAG na wewe nani mwongo?

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Salome Makamba unauliza swali huku unatoa taarifa, taarifa ni kwamba mtu kile anachokisema unakuwa unamwongezea kama hakijakamilika ama kimekaa namna fulani, sasa wewe unamuuliza swali ili aanze kujibizana na wewe jambo ambalo haliruhusiwi.

Mheshimiwa Ester Michael Mmasi malizia mchango wako.

MHE. ESTER M. MMASI: Mheshimiwa Naibu Spika, hapa kuna homa ambayo haijapata tiba, dengue leo inatiba, lakini homa ya kwetu humu ndani, haijapata tiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, iko hivi TANESCO leo anaambiwa anarekodi hasara, si kila hasara ni hasara, mtu anapodaiwa si kosa la jinai na kudaiwa si hasara, nini kigumu katika hicho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niikatae taarifa ya rafiki yangu mpenzi, comrade wangu Salome, naomba niendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye masharti ya Sheria hii ya mwaka 2015 ya Petroleum Act inatuambia kwamba ni sharti kwamba Taasisi hii iweze kuwa Mfuko wa Rasilimali ya Gesi na Mafuta, ni sharti zuri sana, haina mjadala, lakini katika masharti ya Mfuko huu, leo hii TPDC mwaka huu wa fedha peke yake imepeleka bilioni 66, lakini Mfuko huu una jumla ya bilioni 102, lakini toka TPDC imeanza kupeleka kule hakuna a single coin iliyoweza kutoka na kwenda kufanya re- investment kwenye masuala ya maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo Waziri amesimama pale anasema kwamba anaenda kwenye mpango wa nyumba 200, baada ya hapo nyumba 1000, leo tunatakiwa tuongelee nyumba 10,000 au 20,000 leo tunatakiwa tusikie maendeleo ya kuleta nishati ya gesi Dodoma, lakini tuko Dar es Salaam pale tunahitaji Mfuko huu ufanye kazi Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, Mfuko wa REA unafanya kazi, tuondoe sharti la kisheria la asilimia tatu, halitatusaidia Mheshimiwa Waziri. Tunaomba sharti la asilimia tatu kama kifungo cha Waziri iondoke kwenye ile sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hili, upo mkopo wa EXIM Bank of China ambayo ni shilingi 1.225 bilioni US Dollars. Kwa kuwa moja ya jukumu la Serikali katika kuandaa mazingira wezeshi ya investors ni pamoja na kuweka miundombinu. Leo hii Serikali imeenda imekopa pesa China inakuja inamwekea TPDC ina m-charge zile pesa. Leo hii TPDC ameandikiwa rekodi ya bilioni ya 340 kama rejesho lake, yaani huyu amepewa hesabu kama ni mdaiwa wa mkopo huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili ni jukumu la Serikali kuandaa miundombinu ili TPDC aweze hata kukopesheka akienda leo sokoni hawezi kukopesheka, kwa sababu anaonekana ana taarifa chafu. Naomba Mheshimiwa Waziri aje atuambie ni kwa nini asione umuhimu wa kuondokana na mkopo huu kwa Taasisi ya TPDC ili iweze kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili imeshagongwa Mheshimiwa, ahsante sana. (Makofi)

MHE. ESTER M. MMASI: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.