Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati

Hon. Jesca David Kishoa

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, shukrani. Kabla ya kuendelea na mchango wangu ningependa kuomba kiti chako kutumia kanuni ya 64(1)(a) ambapo ningependa u-set position, kwa maana ya kwamba Kanuni hii imekuwa ikitumika kwa upande wa Waheshimiwa Wabunge ambao imekuwa ikisemakana wanatoa taarifa za uongo Bungeni basi iwe applicable kwa upande wa Waheshimiwa Mawaziri ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakitoa taarifa za uongo na hakuna hatua yoyote inayochukuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Wizara ya Nishati peke yake kuna mambo mbalimbali ambayo yakiahidiwa nami nayahesabia kama ni ya uongo kwa sababu yameshindwa kutekelezeka. Mwaka 2016 mwezi 11 Waziri wa Nishati alipokuwa akijibu swali ndani ya Bunge, swali langu ambalo nilikuwa nina hoji kuhusiana na ujenzi wa miradi ya uzalishaji wa umeme wa upepo aliahidi kwamba kufika mwaka 2017 mwezi wa nne miradi hiyo ujenzi wake utaanza na utakamilika mwaka 2019; lakini mpaka hivi ninavyozungumza Mheshimiwa Naibu Spika hakua taarifa yoyote ambao inaonesha wamekwamba wapi. Ni miezi 30 mpaka sasa hakuna kinachoendelea,

Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 25 Mei, 2018 alisimama AG humu ndani akaahidi baada ya hoja yangu ya mikataba mibovu ikiwemo mkataba wa Songas; akasema ndani miezi miwili, kuanzia mwezi wa tano, kwa maana ya mwezi wa saba, mikataba yote itakuwa imeshafanyiwa review, lakini mpaka kufikia hivi sasa ni takribani mwaka mzima hakuna ambacho kinafanyika. Mwaka 2018 mwezi wa 11 Bunge la mwisho aliyekuwa Waziri wa Madini wakati huo alisimama kutoa taarifa Bungeni kwenye hoja yangu ambayo ilikuwa inahusiana na taarifa kutoka TEITI, taarifa ya nane, iliyokuwa inaonyesha kuna upotevu wa fedha bilioni 30.5, akaahidi akasema kwamba ameshapeleka taarifa kwa CAG na kufikia mwezi wa 12 taarifa itakuwa tayari. Hata hivyo mpaka sasa hivi ninavyozungumza hata kwenye Kamati taarifa hii haijapelekwa na hapa Bungeni kwenye hotuba sijasikia taarifa ya namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kwa sababu gani, ni muhimu tukajenga heshima ya Bunge hili na Mawaziri waanavyokuja humu ndani wajue kabisa wanazungumza na supreme organ of the state. Pia ni vyema tukajua kwamba moja ya vitu ambavyo vina taste credibility ya Bunge hili ni pamoja na masuala kama haya. Kwa sababu hizi ni sensitive issues lakini ni mambo ambayo yanakosa majibu kutoka Serikali. Ninajua na tunatambua kwamba kuna kitengo hapa Bungeni ambacho kinahusisha masuala ya kufuatilia ahadi za Serikali, na wanalipwa mshahara mzuri sana, nashindwa kuelewa wanafanya kazi gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye hoja nyingine kuhusiana na TEITI. Natamani na ninahitaji kujua kwamba Serikali ina mpango gani na TEITI. Wote tunajua kwamba TEITI ni taasisi ambayo inahusiana na masuala ya uwazi na uwajibikaji; Serikali imeifanya TEITI kama mradi wake na wanasahau kwamba TEITI wana wajibu mkubwa sana katika taifa hili ya kuhakikisha kwamba public inakuwa aware na masuala yote yanayohusu matumizi ya makubwa ya rasilimali zao. Ni vyema Serikali ikatuambia kama haioni umuhimu wa TEITI ni muhimu mkajiondoa kwenye umoja huu kitamaifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa ninavyohamu na ninavyoamini kwa Serikali yoyote ambayo ikijipambanua kwamba yenyewe inayopinga ufisadi kwenye mamlaka au taasisi ambazo zinakuwa zina influence transparency zinaunga mkono kwa kiasi kikubwa sana. Nashindwa kuelewa ni kwa nini Serikali inashindwa kuunga mkono suala hili la TEITI na kuisaidia TEITI. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka kufikia Februari, 2019 TEITI hawajapata pesa yoyote. Taatifa ya utekelezaji wa majukumu ya taiti ya mwaka 2016/2017, 2017/2018 zimebaki kwenye droo kwa sababu TEITI haina mratibu. Ni mambo ya aibu kabisa mamlaka kubwa kama hii kukosa mratibu mpaka sasa hivi. Lakini mmewahamisha kutoka Dar es Salaam ambapo walikuwa wanakaa kwenye Ofisi kubwa jengo kubwa mmewahamisha mmewaleta hapa Dodoma wanakaa kwenye vyumba viwili vidogo viniwafinya kiasi kwamba hata taarifa wanashindwa kuziweka kwenye sehemu husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaiona haja ya sisi Wabunge wa Serikali kuhakikisha kwamba tunafanya marekebisho kwenye Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji ya Mwaka 2015 ili kuipa TEITI nguvu na mamlaka yakusimama yenyewe kuwa huru kimiundo na kimifumo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia nigusie suala la bomba la gesi la kutoka Mtwara kwenda Dar es Salam. Moja ya sababu kubwa ya watu wengi kushindwa kununua gesi ya TPDC ni gharama za ujazo wa bomba kuwa kubwa sana. Na kwa sababu mambo hayo mnashindwa kuyaweka wazi kuna taarifa, inasemekana kwamba gharama halisi ya bomba la gesi na gharama tunayolipa kuna ziada ya dola kimarekeni milioni 400.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kulipa gharama zote hizi hii ndio inayopelekea gharama ya gesi hii uwa kubwa. Naomba kupitia Bunge hili Tukufu, na hii nitaishikia shilingi, Serikali iunde timu ya watalamu kwenda kuchunguza gharama halisi ya bomba la gesi, lakini pia wachunguze mkopo ambao tumpewa kutoka China Exim Bank.

Mheshimiwa Naibu Spika, na bahati nzuri sana huu mkataba upo very clear mkataba upo clear kwa maana ya kwamba wanasema hivi, ikitokea kwamba Tanzania tumshindwa kulipa hili deni tujue kabisa kwamba gesi yote inayopatika Mtwara inakwenda kuwa controlled na China na bomba la gesi lenyewe. Hii haitakuwa maajabu kwa sababu hili suala limefanyika Srilanka, limefanyika Zambia. Kwa hiyo ni muendelezo wa mambo ambayo kama hatuwezi kuwa makini tunaweza tukajikuta tunapotea rasilimali muhimu sana katika taifa hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, bomba la gesi ambalo linafanya kazi kwa 6% tu na tumetumia mkopo mkubwa kiasi hicho kwa sababu ya kulijenga, inaonesha ni namna gani kama Serikali tunafanya mambo mengi kwa kukurupuka bila kutafakari na kuwa business plan. Baada ya kusema hayo naomba niunge mkono hoja ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni akushukuru sana. (Makofi)