Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati

Hon. Hamidu Hassan Bobali

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati

MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza nichukue fursa hii kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kufanya social cooperate responsibility yeye akishirikiana na Mkurugenzi wa TPDC, namshukuru sana engineer Kapulya wamewasaidia wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri anafanya kazi nzuri. Katika Mkoa wa Lindi tatizo la umeme sasa hivi katika maeneo mengi limekwisha na nilisema mwaka jana sisi Lindi na Mtwara tulikuwa tuna shida sana ya umeme, lakini walivyotuingiza kwenye grid ya Taifa wamepunguza ile changamoto ya umeme, sasa hivi unaweza kwenda kukaa kijiji kule uka-relax kwa kuwa umeme utakuwa unaupata.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri juzi alikuwepo Lindi na tulizungumza, kuna yule Mkandarasi State Grid sasa hivi ameanza kufanya kazi, lakini katika Majimbo manane ya Mkoa wa Lindi Majimbo ya wenzangu yote yamepelekewa nguzo na kazi inafanyika. Jimbo la Mchinga tu ndiko ambako hata nguzo moja haijapelekwa. Sasa Mheshimiwa Waziri hili analiweza walau leo tu amwagize kwamba walau zile nguzo zipelekwe pale tuwe na imani. Viko vijiji vimeingia kwenye REA awamu III, phase one Vijiji vya Ruvu na Dimba na nimeshampelekea mara nyingi sana Mheshimiwa Waziri na haviko mbali na ulikopita umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunaomba sana Mheshimiwa Waziri hivi vijiji na namshukuru sana Meneja wa TANESCO wa Mkoa ndugu yangu Makota, kama tulivyoongea wakati ule mwezi uliopita alikwenda mpaka kwenye vile vijiji akafanya survey na baadaye nadhani alileta taarifa kwamba yale maeneo hayahitaji nguzo nyingi ili kupelekwa umeme. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri naomba sana na mimi nione kwamba katika maeneo yale ya Ruvu na Dimba nguzo zinapelekwa ili wananchi wale waweze kupata umeme. Ni vijiji ambavyo viko pembezoni mwa bahari, ni wale wavuvi wamejenga nyumba nzuri, wakiweka na umeme pale mambo yataenda vizuri sana. Kama pale Ruvu pana ile bandari ndogo inatumika, bila umeme kwa kweli ni changamoto kidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishauri mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la mradi wa gesi wa LNG, nisipouzungumza huu mimi natoka Lindi, natoka Jimbo la Mchinga ambako ndiyo eneo kabisa mahususi sisi pale na Lindi Mjini mradi huu utatekelezwa. Mradi huu wa LNG kwanza utakuwa na faida kubwa kwa Taifa, utakuwa na faida kubwa kwa wananchi wa Mkoa wa Lindi na wananchi wa Mkoa wa Mtwara na utakuwa ndiyo mradi mkubwa kabisa kuliko miradi yote katika Afrika Mashariki. Mradi wenye uwekezaji wa dola bilioni 30 siyo mradi mdogo ni zaidi ya trilioni 69.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu ukizungumza na wawekezaji, juzi nilikutana nao Lindi, wao wanaonesha kwamba hata kesho wako tayari, Wizara wanaonesha hawana tatizo. Baada ya ku-study huu mchezo, maana kila siku ukiuliza huku unaambiwa hivi, nimegundua tatizo lipo kwenye taasisi ama sekta moja inaitwa Government Negotiation Team, Timu ya Uatanishi/Mapatano ya Serikali inaonesha kwa sababu hata kwenye kitabu cha Waziri kwenye ukurasa wa 93 alipozungumzia huu mradi amezungumzia kwamba mwaka huu bado utaendelea na majadiliano kati ya Serikali na Wawekezaji. Sasa ninachopata shida ni kwamba, wawekezaji wanaonesha wako tayari Serikali wako tayari, kwa nini kwa miaka minne sasa hii negotiation team bado haijamaliza kujadiliana na wawekezaji kujua kwamba Serikali itapata hiki na wao watachukua hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, LNG sisi hatuanzi huu mradi, siyo kwamba Tanzania tunaanza, ziko nchi ambazo tayari wana hii miradi. Nitatoa mfano, Algeria, wameanzisha mradi wao LNG ulianza mwaka 1964. Tangu mwaka 1964 hivi hii Government Negotiation Team inashindwa kusafiri kwenda Algeria kwenda kujifunza wenzetu walikubalianaje, Serikali inanufaikaje na sisi Tanzania tutawezaje kuwekeza kwenye huu mradi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Msumbiji wana Mradi wa LNG, Angola wana Mradi wa LNG, Egypt wana Mradi wa LNG, sisi hatuanzi. Kama kuna tatizo wanaona kwamba labda inawezekana Serikali itaingia hasara, twende tukajifunze kwa hawa wenzetu, hawa ni Waafrika wenzetu. Bahati mbaya sana makampuni yenyewe yanayokuja kuwekeza hapa ndiyo hayo hayo ambayo yako Namibia na Egypt, Shells Equinor, Camel ndiyo hayo hayo kwa sababu haya ndiyo makampuni yanaongoza duniani kwa uwekezaji kwenye gesi. Napata ukakasi sana mradi mkubwa kama huu kila mwaka tunauchezea na gesi ipo tu pale baharini katujaalia Mwenyezi Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tumegundua gesi sambamba na Msumbiji, wenzetu Msumbiji wameanza kunufaika na gesi wanaumeme wa uhakika, maendeleo yao yanakwenda kwa haraka sana, sasa hivi wameshatuacha. Tuna mfano mzuri wa kuutazama Uingereza na Norway waligundua gesi mwaka mmoja. Norway wamenufaika sana na gesi, Uingereza mpaka sasa hawajanufaika chochote na gesi. Ukisoma kwenye vitabu vyao wanasema hata wao hawajui kwanini hawajanufaika na gesi, lakini wamegundua mwaka mmoja na wako jirani pale Norway wame-advance sana, wameendelea kwa kutumia gesi, sasa na sisi tukichelewa wenzetu Mozambique wataendelea watatuacha sisi tutaendelea kukaa kila siku Government Negotiation Team haijamaliza kazi, tunaendelea kuwa maskini wakati siyo watu maskini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo gesi hii ametupa Mwenyezi Mungu ipo pale kwenye visima, Zafarani na maeneo mengine, tuitumie. Kama kuna tatizo wanaliona kwenye makubaliano, basi waende wakajifunze hayo maeneo mengine wenzetu walifanyaje ili huu mradi uweze kuondoka. Sisi tumekaa tunausubiria pale Mchinga, tumejaribu kujipanga ukifika tufanye nini hatuna shida, wananchi tutawapokea hao wawekezaji,watakaa vizuri na eneo wameshaandaa kulipa fidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, angalia, mwaka jana kwenye bajeti ya...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)