Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati

Hon. Ignas Aloyce Malocha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati

MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Wizara hii. Kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote katika Wizara hii, lakini bila kumsahau Meneja wetu wa Mkoa wa Rukwa ndugu Chambua anafanya kazi vizuri sana anamwakilisha Mheshimiwa Waziri vizuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa lazima tutambue kwamba pamoja na kusudio la kupeleka umeme vijijini, ili kuchochea maendeleo lakini vilevile lazima tukubali nia ya Serikali ni kufanya matumizi ya umeme yawe makubwa ili return irudi Serikalini. Nimeona baadhi ya maeneo kijiji kinapelekewa umeme lakini unakuta vijiji vinne watu wanne ndiyo wamevuta umeme au watano au sita, maeneo mengine yote wananchi wanaangalia umeme. Sasa nasema hivi lazima waangalie vipaumbele katika maeneo ambayo watu wanahitaji umeme na wanataka kuutumia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano Jimbo langu la Kwela lina vijiji 115, mpaka sasa hivi ni vijiji 16 tu vilivyopata umeme sawa na asilimia 18.4, vijiji 99 havijapata umeme sawasawa na asilimia 81.6 na Mheshimiwa Naibu Waziri anafahamu kabisa amepita katika eneo lile karibu kila kijiji ni kama mji watu wanataka umeme na kutokana na uwezo walionao walishaweka solar ila solar wanashindwa matumizi mengine makubwa. Kwa hiyo tunaomba sana waweze kutupelekea umeme katika Jimbo letu la Kwela.

Mheshimiwa Naibu Spika, utakumbuka mwaka 2014, REA II, walichukua umeme Sumbawanga wakapitisha kwenye Jimbo langu wakapeleka Katavi, wakaacha karibu vijiji sita bila kuweka umeme jambo ambalo kwa wananchi linawaumiza. Mpaka sasa katika Jimbo langu kuna Kata 16 hazijapata umeme; Kata za Kilangawana, Kaoze, Kapenta, Ilemba, Nankanga, Milepa, Zimba, Kalumbaleza, Mwadui, Mfinga, Msandamuungano, Kaengesa, Kanda, Lyangalile na Mnokola, Kata 16 havijapata umeme hata vijiji vyake. Sasa jamani lazima tufike mahali tuangalie hawa watu wanahitaji umeme na bahati nzuri Jimbo langu wananchi wanataka umeme, wafanyabiashara wameshaanza kufunga viwanda vya mashine za kukoboa mchele, lakini wanasubiria umeme wameshafunga viwanda zaidi ya 20 lakini umeme hakuna.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningeomba juhudi ile ile ya Naibu Waziri alipofika kule Mto Wisa alisema lazima umeme uwake. Umeme uliwaka pale Mto Wisa lakini waliruka Vijiji vya Kalakala, Uzia, Kifinga, Mkamba, Mwela, havijapata umeme na kule Kilyamatundu alipohimiza kweli umeme umeshawaka lakini haujasambaa kwenye zile Kata nyingine na Mheshimiwa Waziri alifika kule Nyangalua, akahimiza umeme ukawashwa na alisema vijiji vyote vinavyozunguka maeneo yale lazima vipate umeme, lakini mpaka sasa hivi vile Vijiji vya Tunko, Kamsamba, Kavifuti, Movu, Mkowe, havijapata umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri wahimize na naomba Meneja wetu wa Mkoa wa Rukwa kama kuna bajeti ameleta ya kuomba pesa ya kujaziliza, wampe bajeti ya kutosha, anatusaidia sana na anaweza akawaokoa sana hata kuchelewa kwa wakandarasi, huyu Meneja ana uwezo mkubwa sana, tena nafikiri wakati mwingine angeweza kupewa fedha huyu angeweza kufanya haraka zaidi kuliko hata mkandarasi. Huyu Meneja wametuletea Meneja kweli kweli, anawajibika, si kwa Jimbo moja kwa mkoa mzima. Pia si kwa umeme huu wa REA hata wa TANESCO, anatoa majibu kila siku kwamba kuna tatizo hili na analishughulikia. Naomba sana kama amepeleka bajeti, wamsaidie bajeti yake ipite, atatusaidia sana katika kueneza umeme katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nahimiza sana Wizara wanajitahidi, Waziri anajitahidi, Naibu Waziri anajitahidi ila tunaomba sasa waongeze kasi na wanapopeleka umeme waangalie maeneo ya Jimbo la Kwela, wananchi wanahitaji umeme. Lile Jimbo hatuna shida, wanavuta hata umeme wa TANESCO kutoka Sumbawanga, itakuwa umeme wa REA? Watuletee umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nashukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)