Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Madini

Hon. Stanslaus Haroon Nyongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Maswa Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Madini

NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuhitimisha hoja hii ya Wizara yetu hii ya Madini.

Mheshimiwa Spika, nianze ka kutoa pongezi kubwa kwa Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya katika kusimamia Sekta hii ya Madini lakini vilevile nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa uteuzi alioufanya kwa kuweza kumteua Waziri wangu Mheshimiwa Dotto Biteko mimi na yeye kusimamia sekta hii muhimu ya madini kwa kweli namshukuru sana na tunapenda kumwahidi kwamba hatutamwangusha, tutaendelea kufanyakazi vizuri zaidi.

Mheshimiwa Spika, niendelee kumshukuru vilevile tena Mheshimiwa Rais wka kumteua dada yetu Angella Kairuki kushika nafasi ya kuwa Waziri wa Mambo ya Uwekezaji ambayo itakuwa chini ya Waziri Mkuu. Ni hatua kubwa sana mbapo hata sisi kwa upande wa madini ina tija kubwa na itatusaidia sana katika masuala yote ya uwekezaji.

Mheshimiwa Spika, niendelee kuishukuru Wizara ya Madini ikiongozwa na Katibu Mkuu, Profesa Msanjila kwa kazi kubwa anayoifanya tunasaidiana nae lakini vilevile niendelee kuwashukuru sana Wabunge kwa michango yao ambayo kwa kweli leo wamechangia hapa tumeona Kamati ambayo nayo imeweza kutoa maoni yake. Nipende kusema kwamba tunashirikiana vizuri sana na Kamati ya Nishati na Madini na tunafanya kazi bega kwa bega kuhakikisha kwamba tunapeleka sekta hii ya madini kule ambapo kunastahili.

Mheshimiwa Spika, vilevile niendelee kuwashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo la Maswa Mashariki kwa kuendelea kunivumilia kwa kazi kubwa ninayoifanya maana muda mwingi nakuwa niko nao mbali lakini kwa kweli wamezidi kunipa ushirikiano mzuri, tunaendelea kushirikiana nao kuhakikisha kwamba naendelea kusimamia Jimbo langu la Maswa Mashariki kupeleka maendeleo ambayo tulikuwa tumewaahidi wananchi, lakini vilevile wanaendelea kuwa na uvumilivu wa kunivumilia mimi muda mwingi ninapokuwa sipo Jimboni. Vilevile bila kusahau niishukuru sana familia yangu ambayo inanipa nguvu katika kufanya kazi zangu za Wizara.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, niendelee sasa vilevile na kuchangia hoja ambazo Waheshimiwa Wabunge wamezizungumza hapa.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nipende kusema kwamba tunaendelea kupongeza, kumpongeza Mheshimiwa Rais na kupongeza Bunge lako Tukufu kwa kukubali kupitisha au kubadilisha Sheria yetu ya Madini ya Mwaka 2010 na hayo mabadiliko ambayo tumeyafanya mwaka 2017. Kwa kweli kwa muda ambao tumeanza kutumia sheria hii tumeweza kuona mabadiliko makubwa ambayo yameweza kusaidiwa na sheria hii baada ya kufanya haya mabadiliko.

Mheshimiwa Spika, cha kwanza kabisa ni ile Serikali kumiliki asilimia 16 kwenye miradi yote ya migodi ya madini. Kwa kweli imeonekana kuwa na tija kubwa na watu wote, wawekezaji wote wa upande wa madini wako tayari kutoa asilimia 16 ambayo Serikali itakuwa inazimiliki japokuwa Kambi ya Upinzani walikuwa na wasiwasi kuona kwamba labda inamilikiwa na nani, lakini niwatoe tu wasiwasi Kambi ya Upinzani kwamba hii asilimia 16 sasa hivi iko chini ya Treasury kwa maana ya Hazina. Vilevile mapendekezo yao walikuwa wanayatoa kwamba iwe STAMICO, ok fine, inaweza ikawa STAMICO lakini inaweza ikawa kwa upande wa Treasury, lakini bado iko upande ule ule wa Serikali. Ile ownership ya 16 percent bado inamilikiwa na Serikali na Serikali inapopata gawiwo basi itapeleka maendeleo kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, vilevile kwa mabadiliko haya haya tunashukuru na kuona tija kubwa ambayo imekwenda hasa katika kubadilisha kiwango cha mrabaha kutoka asilimia nne na asilimia tano sasa hivi tunatoza asilimia sita kwenye madini ya metali na asilimia sita hiyo kwenye madini ya vito. Tumeona jinsi ilivyoweza kupandisha mapato na kuweza kupata maduhuli makubwa kutokana na ku-charge asilimia hiyo sita ikiwa ni pamoja na tozo jipya la asilimia moja kwa maana ya clearance fee. Kwa kweli niwashukuru wachimbaji wamejitolea na wame-comply vizuri na sheria hii na wanatoa hiyo tozo na kwa kweli hawana malalamiko yoyote.

Mheshimiwa Spika, isipokuwa tu niendelee kumshukuru tena Mheshimiwa Rais pale tarehe 21 Januari, 2019 baada ya kukaa na wachimbaji akaongea nao kwa kweli walitoa malalamiko mengi na hasa katika kodi ambazo zilikuwa zinatozwa katika sekta hii ya madini. Nishukuru kwamba baada ya kuondoa hiyo VAT pamoja na withholding tax kwa kweli unafuu umeonekana mkubwa na sasa hivi wengi wa wachimbaji wanaonekana kutoa ushirikiano katika kufanya biashara kwa sababu tumepunguza kodo hiyo.

Mheshimiwa Spika, pia nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwamba kupitia Shera hii ya madini amekuwa na msisitizo mkubwa katika kuanzisha masoko ya madini. Kwa kweli uanzishwaji wa masoko ya madini imeonekana kuwa na tija kubwa. Mfano mzuri, soko moja tu la kule Chunya, siku ya kwanza ambapo tumefungua soko la madini tuliweza kupata zaidi ya kilo 13 za dhahabu na kupata zile kilo 13 za dhahabu tulipata zaidi ya shilingi milioni 68 kwa siku moja tu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ina tija kubwa na sasa tumefungua masoko 22 na kwa kweli ni kwamba ukusanyaji wa fedha umekuwa ni wa hali ya juu, tumeona jinsi fedha ilivyokusanywa kwa sababu dhahabu iliyopita kwenye masoko mpaka hivi sasa ninavyozungumza ni zaidi ya kilo 578 ambapo zina thamani zaidi ya bilioni 48 na sisi kama Serikali kupitia huo mrabaha tumeweza kupata zaidi ya bilioni 3.6.

Mheshimiwa Spika, kwa kweli tukiendelea na kusimamia vizuri masoko haya basi tunaweza tuakajikuta tunakusanya vizuri zaidi na nipende tu kuishukuru Kamati ya Nishati na Madini imetoa mapendekezo yake na niseme tu kwamba tumeyachukua mapendekezo hayo, tunakwenda kuyatumia mapendekezo hayo katika kuboresha masoko haya na kuhakikisha kwamba masoko haya yanaendesha vizuri shughuli zake.

Mheshimiwa Spika, niendele kuwaasa wachimbaji, walete madini kwenye masoko haya kwa sababu ukileta madini kwenye masoko haya unapata uhalali wa Serikali, utaingia kwenye ule utaratibu sahihi wa Kisheria ambapo madini yako sasa yatatambulika Kiserikali na wee utalipa kodi yako lakini vilevile Serikali itapata kipato chake na Serikali itakulinda, itakupa usalama wa madini hayo na itakupa usalama wa soko.

Mheshimiwa Spika, vilevile niwaase wanunuzi; bado wanakwenda kununua madini katika masoko ya pembeni au ya uchochoroni. Tuwaase na kuwashauri kwamba waje katika masoko ya madini kwa sababu masoko haya tumeyatengeneza kukutanisha wauzaji na wanunuzi wa madini. Wakifika katika soko utaratibu wote unachukuliwa na wataalam wetu wako pale, wanapima madini hayo na kuhakikisha madini siyo feki, madini ni sawasawa, kipimo utatolewa sawa sawa lakini vilevile ni kwamba utakuwa na uhakika na kile ambacho wewe umekinunua.

Mheshimiwa Spika, niendele kushukuru katika marekebisho haya haya ya Sheria ambayo tuliweza kuyafanya, kuna suala la local content; wafanyabiashara wengi au wachimbaji wengi wame-comply na Sheria ya Local Content, mpaka sasa hivi tuna uhakika kampuni nyingi sasa hivi wanaajiri Watanzania, lakini Kampuni nyingi vilevile sasa hivi zinakwenda kutumia bidhaa za Tanzania.

Mheshimiwa Spika, pia tushukuru kwamba kwa kweli hata wafanyabiashara wa Kitanzania wameonekana kuwa na kufanya biashara ambayo iko katika viango ambavyo wenye migodi wanahitaji. Zamani ilikuwa ni shida kupeleka bidhaa au wafanyakazi ambao wana ile quality au ule ubora ambao wachimbaji wanautaka, lakini kwa kutumia Sheria hii, Watanzania wamekuwa tayari kufanya biashara na migodi mikubwa na kuhakikisha kwamba wanakidhi yale mahitaji na ubora ambao wachimbaji wetu wanataka.

Mheshimiwa Spika, vilevile katika sheria hii tuliona suala la CSR na Wabunge wengi wameliongelea. Katika suala hili la CSR kuna Halmashauri nyingi ambazo sasa hivi wameanza kuona matunda yake ikiwepo Halmashauri ya Manispaa ya Geita. Geita sasa hivi wanakwenda kupata zaidi ya bilioni tisa na bilioni tisa hiyo itakwenda kufanya maendeleo katika Mji wa Geita. Hapo awali ni kwamba hii CSR ilikuwa ikitoka unakuta wanatueleza tu kwamba leo wamejenga shule, ukiuliza bei ya shule wanakwambia tumejenga kwa bilioni moja. Ukiangalia thamani ya shule hiyo haiendani na bilioni moja hata milioni 200 haifiki.

Mheshimiwa Spika, lakini sasa hivi Madiwani watasimamia fungu hili na wanaposimamia fungu hili watahakikisha kwamba value of money ipo kuhakikisha kwamba miradi hiyo sasa inakuwa na tija na ubora lakini inalingana na kiwango cha fedha ambayo imetengwa.

Mheshimiwa Spika, kuna suala la service levy; niendelee tu kutoa ushauri kwa halmashauri zote, watu wote wanaotoa huduma kwenye migodi watupe ushirikiano kwa kushirikiana na halmashauri. Mtu yoyote ambaye hayuko tayari kutoa service levy katika Sekta hii ya Madini sisi tutambana. Tuhakikishe kabisa kwamba watu wote wana comply na sheria ya ya kulipa service levy ambayo ni asilimia
0.3 na waweze kutoa kwa halmashauri husika. Mfano mzuri juzi nilikuwa Shinyanga, yule mchimbaji mmoja ambaye alipata almasi kubwa kabisa ambayo haijawahi kutokea hapa Tanzania yenye carat zaidi ya 512, palepale tumemchaji katika soko la madini amelipa mrabaha wetu zaidi ya milioni mia moja na themanini na kitu; lakini vilevile katoa fedha kwa ajili ya clearance fee na palepale tukatoa fedha ambayo ni 0.3 percent kwa ajili ya Halmashauri ya Kishapu; na halmashauri imepata fedha. Huo ndio mfano mzuri kwa wachimbaji wote waweze kuhakikisha wanafuata taratibu na sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile nishukuru kwamba katika Wizara yetu tumeendelea kusimamia masuala ya uongezaji wa thamani ya madini (value addition), sasa hivi katika kituo chetu cha TGC cha pale Arusha tunaendelea kutoa mafunzo kuhakikisha kwamba vijana wetu wanajifunza namna ya kukata madini na kuweza kuongeza thamani katika madini hayo.

Mheshimiwa Spika, tuna Taasisi ya GST ambayo ni muhimu sana kwa wachimbaji Waheshimiwa Wabunge wameiongelea. Nipende kukuhakikishia katika Bunge lako kwamba tunaendelea kufanya tafiti mbalimbali na kuchora ramani ambazo zinaonesha uwepo wa madini kwa kila mkoa na kwa kila Wilaya. Katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri wangu imeeleza, kwamba tumeshatengeneza ramani hiyo na wachimbaji wote wanaweza wakaja GST kuweza kupata taarifa mbalimbali za uwepo wa madini mbalimbali katika yale maeneo tuliyonayo.

Mheshimiwa Spika, STAMICO; kwa mara ya kwanza sasa hivi STAMICO imefufuka na hapa tunavyozungumza mgodi wa STAMIGOLD ambao ulikuwa unatengeneza hasara tulikuta hasara ya zaidi ya bilioni 64. Sasa hivi mgodi wa STAMIGOLD unatengeneza faida tumeshapata faida zaidi ya bilioni moja; ni kwa sababu ya usimamizi mzuri na tulibadilisha pale menejimenti sasa hivi wanachimba kwa faida. Nipende tu kuwahakikishia ile STAMICO iliyokuwa inazungumzwa zamani vibaya na Bunge lako hili Tukufu, kwa sababu Waheshimiwa Wabunge kweli ilikuwa inawachefua sasa hivi tunakwenda kuongelea faida katika uchimbaji au katika miradi ya STAMICO. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kuzungumzia issue ya Mheshimiwa Kishimba. Amezungumzia katika ufungaji wa Mgodi wa Buzwagi; ni kweli kuna shimo kubwa pale ambalo liko pale na ndani ya shimo hilo au tuseme chini bado kuonaonekana kuna chembechembe au kuna uwepo wa dhahabu zaidi ya ounce milioni moja. Ni kweli, lakini katika masuala ya uchimbaji dhahabu inaweza ikawa chini haina tatizo lakini namna ya kuichukua dhahabu hiyo chini kuna gharama, gharama inapokuwa kubwa; kwa mfano sasa hivi ounce moja iko kwenye dola 1200, ukaweza kuchimba kwa gharama ya dola 1100, 1200, bado kuna wasiwasi inawezekana ukatengeneza hasara kubwa. Lakini kama unaweza ukachimba, sasa hivi pale Buzwagi mpaka wanafikia mwisho walikuwa wanachimba ounce moja kwa gharama ya dola 900, kwa hiyo ukienda kuuza kwa dola 1200 unapata faida.

Mheshimiwa Spika, lakini sasa hivi ni kwamba wana mitambo mikubwa, ukisema uchimbe dhahabu iliyoko pale kwao hawataweza kutengeneza faida; labda aje mchimbaji ambaye anaweza kuchimba kwa gharama ndogo, akichimba kwa gharama ndogo kwa hali iliyoko pale anaweza akatengeneza faida. Lakiini kinachotokea shimo lile ni kubwa kuna matetemeko yanapita yanahatarisha usalama wa wananchi wanaoishi maeneo yale. Tuna mfano mzuri pale katika mgodi wa Lisolute pale Nzega mashimo yameachwa, ni hatari kweli kweli. Sasa katika uchimbaji sheria inasema unapotaka kuanza kuchimba lazima utupe mining plan yako lakini lazima utupe mining closure yako plan ikoje na Kamati ya mining closure lazima ione na iridhie. Sasa hivi wameshawasilisha mining closure plan yao na ni lazima wafukie shimo hilo.

Mheshimiwa Spika, lakini kama Mheshimiwa Mbunge anaendelea kutushawishi kwamba inawezekana mtu anaweza akachimba kwa gharama nafuu atuhakikishie ufunikaji wa shimo hilo; kitu ambacho tunaona ni kitu kigumu. Kwa hiyo bado majadiliano yanaendelea ya kuona namna ya kufanya.

Mheshimiwa Spika, lakini vilevile niendelee kumueleza Mheshimiwa Kishimba, amezungumzia hoja ambayo hata sisi tunakubaliana nayo; kuhusu service levy kwa yale makampuni yalikuwa yanatoa huduma ya bima katika migodi hiyo. Huduma ya bima ilikuwa inatolewa katika migodi hiyo, wale waliokuwa wanatoa huduma hiyo ni makampuni ya nje. Niliwahi kuzungumza tukiwa na Mheshimiwa Mbunge, tukiwa Kahama tukiwa katika msafara wa Mheshimiwa Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu; nikasemaje; hatuna shida sisi kuwabana makampuni haya yatoe ushirikiano wa kutambua yale makampuni ambayo yalitoa huduma na kutueleza walioweza kuwalipa shilingi ngapi ili tuweze ku-charge asilimia 0.3 ambayo ni service levy kwa halmashauri ya Kahama.

Mheshimiwa Spika, niliwaeleza kwamba halmashauri hiyo ifanye ufuatiliaji huo lakini mpaka sasa tunavyozungumza hawajatuletea kutueleza ni nani wamewasiliana naye, je amekubali au amekataa? Nimshauri tu Mheshimiwa Mbunge kwamba atuletee taarifa hiyo ili tuweze kufanya mawasiliano na hawa watu waliohusika. Lakini vilevile tutambue kwamba wale wote waliokuwa wanatoa service kwenye migodi kila mmoja ana wajibu wa kulipa service levy ambayo ni asilimia 0.3

Mheshimiwa Spika, kuna hoja nyingine ambayo imezungumziwa hapa na Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusiana na mradi wa Tancoal. Kuna mengine yataelezwa na Mheshimiwa Waziri atazungumzia na wahusika, Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara amezungumza. Lakini nipende tu kuongelea mambo mawili kuna suala la barabara kilomita 40 kutoka pale Ngaka kwenda Kitai; kwa kweli hili suala linaongeza gharama ya uendeshaji au uzalishaji wa makaa ya mawe kwa sababu gani, kutoka Ngaka kwenda Kitaiā€¦

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante malizia Mheshimiwa Waziri dakika moja.

NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kutoka Ngaka kwenda Kitai ni kilomita 40 na madaraja yaliyopo pale katikati ni madaraja 12 na kila daraja lina uwezo wa kupitisha tani 15 tu za makaa ya mawe na wakati magari yale ambayo yanabeba makaa ya mawe kwenda Rwanda na Burundi yanatakiwa yabebe tani 30, kwa hiyo inabidi magari madogo yaliyo chini ya tani 15 yapitishe kwenye yale madaraja mpaka Kitai halafu Kitai pale ndipo yapakiwe sasa kuingia kwenye magari makubwa ambayo ni Semi trailer. Kwa kweli hii inasababisha ongezeko kubwa la uzalishaji, nikubaliane na tumeshakuongea na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma pamoja na watu wa utengenezaji wa barabara (TARURA) ambao wamesema watakwenda kujenga madaraja hayo na kuhakikisha kwamba sasa baada ya muda wakishajenga madaraja hayo usafirishaji pale utakuwa wa bei nafuu kwa sababu magari ya tani 30 yataweza kufika kule Ngaka.

Mheshiimiwa Spika, baada ya kusema hayo nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, ahsante sana. (Makofi)