Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Madini

Hon. Ezekiel Magolyo Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Madini

MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi bahati mbaya ukunitaja kabla kidogo nijipange. Naomba kwanza niipongeze sana Serikali na hasa Mheshimiwa Rais kwa mabadiliko makubwa, marekebisho makubwa sana yaliyofanyika kwenye sekta hii. Kama mnavyofahamu Waheshimiwa wenzangu mimi natoka mgodi wa Bulyanghulu; nimekuwa na matatizo na kero nyingi ambazo nimekuwa nikizilalamikia hapa lakini kwa kweli awamu hii tumeona kazi kubwa nampongeza sana Mheshimiwa Rais. Nimpongeze sana pia Mheshimiwa Waziri na Nibu pamoja nawatendaji wote wa Wizara pia mnafanya kazi kubwa kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais, pia kusimamia mifumo mipya ya sheria za madini ambayo inanufaisha sana wananchi hasa wachimbaji wadogo wadogo.

Mheshimiwa Spika, nina mambo kama mawili tu ambayo nilitaka kuyazungumzia; kwanza kwa wachimbaji wakubwa. Kama nilivyosema mgodi wa Bulyanghulu una changamoto zake kwa sasa hivi tunafahamu kwamba walishasimamisha uzalishaji na wanaendelea na mazungumzo na Serikali kuhusu migogoro yao ya kule nyuma.

Sisi kama wananchi wa pale tumekuwa tukisema tuna matatizo yetu ambayo tumekuwa nayo kwa muda mrefu; la kwanza ambalo nilikuwa naomba sana Mheshimiwa Waziri utusaidie; tumekuwa tukidai service levy mapunjo kabla hawajaanza kulipa zero point three percent, walikuwa wanalipa dola 200,000 jumla yake ni kama dola milioni 8.6 ambazo ni takriban shilingi bilioni 16. Tulishaomba kupitia Wizara ya TAMISEMI kwa sababu ni suala liko chini ya halamashauri kwamba Waziri Jafo pamoja na Wizara ya Madini mtusaidie kumbana huyu mwekezaji ili haki yetu tuweze kulipwa. Nilikuwa naomba suala hilo lilwe mezani kwako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilitaka vilevile nimuombe sana Mheshimiwa Waziri, tulishamweleza kuhusu matatizo ya migogo ya wananchi ambayo imekuwepo pale; kubwa zaidi ni fidia mgodi wa Bulyanghulu ulipoanzishwa mwaka 1996 wananchi waliokuwepo pale ni kaya 4,600, waliolipwa ni kaya 34 tu, na hili suala nimekuwa nikilieleza na Wizara inalifahamu. Tunaomba tuendelee kulifuatilia, suala la fidia kwa wananchi wa Bulyanghulu bado halijawa settled.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, tatizo lingine ni wachimbaji wadogo wadogo, tuna matatizo ya maeneo kule kwetu tulikuwa tulishaunda vikundi kuna kikundi kinaitwa Kasi Mpya Gold Mining Cooperative Society, kiliomba leseni eneo la Mwazimba; na kikundi kinaitwa Bushimangila and Masabi and Segese Gold Mining Cooperative Society (BMS) waliomba eneo la Bushimangila, Mheshimiwa Waziri ulifika; walishaomba leseni kwa taratibu zote. Kwa bahati mbaya sana utoaji wa leseni katika maeneo haya umekuwa na matatizo; na Mheshimiwa Waziri ulishaagiza amesema Mheshimiwa Musukuma hapa; katika vita tuliyonayo ya kupambana na ufisadi na rushwa moja ya maeneo ambayo tunayo bado ni kwenye Maafisa wetu wa madini. Afisa Madini Mkaazi wa Kahama, baada ya kuwa umeshaagiza siku mbili baadaye aliondolewa; akaja Afisa Madini mwingine, kazi yake ya kwanza aliyoifanya ni kutoa leseni kwa mtu mwingine ambaye wala hakuwa katika maombi ambayo tulikuwa tumeshakuomba na ulishaelekeza.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri kwa sasa hivi tayari pale kuna mgogoro, kwa sababbu kuna leseni ambayo imeshatolewa na ulishaagiza kwamba wale watu wapewe leseni lakini hamna kilichofanyika. Nilikuwa naomba sana, mgogoro wa leseni wa Mwazimba, mgogoro wa leseni wa Bushimangila leo utusaidie angalau kauli itoke kwa sababu kule tunategemea wananchi wangu watafurahi wakisikia kauli yako na msimamo wa mwisho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni la kuomba wachimbaji hawa wadogo wadogo ambao wamewezeshwa kwa kiasi kikubwa sana wanamatatizo ya kupata hasara kwa sababu wanachimba kwa kubahatisha sana. Mbinu tunzozitumia sisi za kienyeji hizi za kupiga ramli hazitusaidii kujua mahala ambapo dhahabu ipo. Kwa bahati nzuri maeneo mengi ambayo sasa hivi wanaachiwa ni yale yaliyofanyiwa exploration na makampuni makubwa na data zimetunzwa na makampuni lakini copy ziko Wizarani. Tulikuwa tunaomba takwimu hizi ziwe shared na hawa wachimbaji wadogo wadogo ambao wanapewa leseni ili waweze kujua exactly mashapo yako wapi na waweze kuchimba with a focus kuliko huu uchimbaji wa kubahatisha bahatisha; tutaweza kuokoa hasara wanazopata, lakini tutaongeza tija katika shughuli zao. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Spika, naomba kusema naunga mkono jitihada za Serikali, naunga mkono bajeti hii, ahsante sana kwa nafasi.(Makofi)