Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Riziki Saidi Lulida

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru na mimi kupata nafasi ya kuchangia katika hoja iliyokuwepo mezani; nitachangia michezo pamoja na walemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania imeridhia haki za walemavu ndani ya Umoja wa Mataifa, na katika eneo ambalo inabidi lifanyiwe kazi ni utalii ndani ya Umoja wa Mataifa. Katika takwimu tulizonazo za dunia walemavu tuko asilimia 15, na katika kuwa asilimia 15 walemavu wale wanahaki ya kufanya utalii katika nchi yetu ya Tanzania. Ndiyo maana leo mmewaona Tembo Warriors wamekuja hapa kuja kuwawakilisha walemavu na kumtangaza Tembo katika nchi yetu ya Tanzania. Kila Mtanzania anatakiwa kusema say no to poaching; ujangili basi, imetosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanini nazungumza hivi kila mwaka Kenya wakiwa katika mkutano wa UN wanasema come and visit Kenya and visit Serengeti, and visit Ngorongoro and Zanzibar. Kwanini, wenzetu wako wanajitangaza. Mimi leo nasema nimejitolea ninataka kusimama kwa hili nikishirikiana na mashirika yote ya utalii ya TANAPA na Ngorongoro watushirikishe na kumpa bendera Mheshimiwa Ikupa aende UN akatangaze utalii ndani ya UN. Naomba Wizara tatu za kushirikiana nazo zimpe ushirikiano Ikupa. Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje, Wizara ya Maliasili na Utalii na Ofisi ya Waziri Mkuu impe ushirikiano Ikupa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina sababu za msingi; kule ndani ya Mkutano wa UN kuna event inafanyika katika kila nchi, state parties. Si kila siku Ikupa atakwenda Marekani anakwenda kufanya nini; tunataka akapeleke ujumbe kama Tanzania yenye utalii na walemavu inawezekana. Na walemavu waliokuwa kule ni maprofessor, wafanyabiashara; ina maana hii 17 percent ambayo ni point two mnaitegemea, tunauwezo wa kuiongezea na iwe hela nyingi zaidi katika suala la utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ninaona katika Bunge hili walemavu tunazidi kuongezeka Mheshimiwa Kigwangwala sasa hivi ni mlemavu wa matatizo ya mikono, tunakukaribisha katika kundi la walemavu, karibu sana unakaribishwa, Mheshimiwa Kanyasu ukiwa mrefu sana na ukiwa mfupi sana vile vile nalo lina matatizo kidogo ya kiulemavu ulemavu ulemavu; na wewe vile vile katika kundi letu la walemavu na mtuunge mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lile desk linafurahisha, ina maana tutawaunganisha walemavu ambao watahudhuria katika mkutano ule na kuwaambia Tanzania kuna utalii. Juzi ilikuja meli na watalii 2500 wameshindwa kushuka Dar es Salaam kwa vile hakuna mazingira ya walemavu wale kuingia Dar es Salaam. Kurudia makosa ni kosa lakini sisi tunataka kusema kwamba kuanzia leo Jiji la Dar es Salaam lianzishe mradi wa city tour ili walemavu waweze kupata uwezo wa kutembelea Jiji la Dar es Salaam. Nina imani Mkurugenzi wa Dar es Salaam Mama Spolar Liana amelianzisha hili, mpeni ushirikiano Spolar aanzishe utalii Dar es Salaam ili watalii wa kawaida na walemavu waanze kuingia Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe pongezi zangu za dhati. Kwanza nimpongeze Allan Kijazi, nimpongeze Manongi kwa kweli mimi sina cha kusema; hawa watu wameweza kusimamia mifumo mizuri ndani ya Mashirika haya. TANAPA sasa hivi inaweza kutoa milioni 37 ndani ya Serikali kama ruzuku, na bilioni 20 kusaidia miradi mbalimbali kwa Tanzania hii. Pia Ngorongoro ni hivyo hivyo, wameweza kupeleka Serikalini; wamevuka malengo wamepeleka bilioni 22. Mashirika mengi yanachukua ruzuku ya Serikali lakini hawa wameweza kutengeneza mifumo mizuri ambayo Serikali badala ya kuwalipa wao, wao wanaipelekea pesa za ruzuku ili kuuendesha utalii na uweze kuwa endelevu na nchi kupata uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ingekuwa nchi nyingine hawa watu wangepewa nobel, na mimi bila kusema chochote nasema ninawapongeza. Kwa niaba ya walemavu wenzangu na baadhi ya walemavu wenzangu na baadhi ya wapenda maendeleo ya utalii nasema Ngorongoro kwa kupitia Manongi na Mr. Kijazi, Mungu awabariki. Wanakaribia kustaafu, na kama wanastaafu wawaandae vijana ambao watashika ule mfumo usiharibike. Ule mfumo ulioko kule umeifanya sasa hivi Serikali inapata mapato yake bila kuwa na matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto zilizokuwepo; kuna changamoto ambayo ng’ombe ukimkamua sana huyu ng’ombe ataharibikiwa. Wakiondoka Kijazi na Manongi tunaweza tukaiona TANAPA na Ngorongoro zinakufa. Serikali naomba isimame.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Wizara ya Fedha kuna tozo zinatozwa ambazo zinazifanya taasisi hizi zisijiendeshe. Wanahitaji barabara wanahitaji mifumo ya maji, wanahitaji mifumo ya mawasiliano wanahitaji kupata mishahara kwa wafanyakazi. Sasa Serikali inayotusikiliza, wanasema Serikali sikivu na mimi nasema ndiyo; naomba wawaangalie na hizi tozo zilizopo mziangalie kwa makini msije kuiue TANAPA na Ngorongoro ili baadaye mashirika haya yapewe ruzuku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakuja kwenye hoja ya pili. Kuna uchonganishi; unazungumzia mikoa ya kusini ni Lindi, Mtwara Ruvuma, ukizungumzia Nyanda za Juu Kusini ni Iringa, Mbeya Katavi na Sumbawanga; na hii imekuwa ni mazoea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umekuja mradi wa SAGCOT (Southern Agricultural Corridor of Tanzania) Lindi, Mtwara Ruvuma hatumo. Mradi huu umepita, watu wamenufaika, mikoa imenufaika sisi hatukunufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umekuja mradi wa World Bank kuna haja gani kusema mikoa ya Kusini? Definition ya Mikoa ya Kusini iko wapi ilhali Lindi na Mtwara hatumo? Ina maana mmetuweka sisi kikaangoni tukingojea mikoa mingine ikipata maendeleo sisi tukiendelea kuswaga kuwa masikini na ilhali tunaongoza kwa utalii mkubwa kuliko mikoa mingine yoyote? Nataka niiorodheshe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Pesa ya Kilwa ya mwaka 1000 leo imeonekana Australia nchi ilipokuwa inajitegemea. Katika urithi wa dunia Kilwa iko namba 21, lakini katika urithi wa dunia huu utashangaa katika mradi wa kusini Lindi, Kilwa, Mtwara Ruvuma mpaka Namtumbo hazimo. Sasa tunafika mahali tunajiuliza hawa wataalam nafikiri wanatufanya sisi tuwe na chuki na mazingira haya. Haiwezekani leo utalii mkubwa wa Selou, maana Selou kutokea Kingupila kwenda Lindi tunachukua two third; Matambwe iko Morogoro na Morogoro iko Mashariki hivyo usichanganye na Kusini. Hivyo kama unaipeleka Matango, Udzungwa na Mikumi haiko Kusini kabisa. Leo tutajivunia nini Kusini na utalii wa Kusini? Hatumo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vivutio vikubwa vilivyokuwa kusini, kwanza corridor ya Selous Niassa, Mozambique, ile corridor ni ya tembo, mbwa mwitu, samba nyati. Nimepiga kelele mpaka leo sioni kama kuna majibu ya kueleweka. Lakini nilikwenda mimi; niishukuru taasisi ya GIZ ilinipa nafasi ya kutembelea na baadhi ya waandishi wa habari; zile corridor wanazopita tembo tayari wafugaji ambao wametolewa Ihefu wamevamia; na baada ya kuvamia mnataka kuhalalisha ili viwe vijiji vya asili; maeneo wanapita tembo unahalalisha kuna nini hapo? Tunaji-contradict.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ninaomba ujumbe huu ninaotoa sasa hivi umfikie Mheshimiwa wangu Rais kwa vile jamaa zake ndio wanafujo ya kupeleka mifugo katika maeneo hayo na wanaingia na magobole. Hivyo tutakapowamaliza hawa tembo na simba utalii utakwisha. Simba anatoka Mozambique anaingia Selou anaingia Tunduru, anaingia Masasi, anaingia Masasi Liwale, anaingia Matambwe, anaingia Mikumi anaingia Kilosa, anaingia Mkungunero, anateremka Ngorongoro, anakwenda Serengeti anakwenda Maasai Mara. Njia hizi mkiziharibu hawa wanyama watapita wapi? Binadamu wamevamia haya maeneo na katika kuvamia maeneo haya ilikuwa only 20 percent ya hifadhi katika Tanzania inakwenda kwa wanyama. Sasa hivi tumepunguza na tuko chini ya 15 percent. Tukizidi kupunguza tunaisaidia nchi au tunaiharibu nchi. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante kwa mchango wako mzuri.