Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Bernadeta Kasabago Mushashu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. BERNADETHA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kunipa nafasi. Kwanza kabisa naanza kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri kwa hotuba nzuri, lakini vilevile kwa kazi nzuri wanayofanya ndani ya Wizara yao. Kwa kweli, kazi wanayofanya ni nzuri na inaonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bodi ya Utalii ina jukumu la kutangaza utalii na kutangaza vivutio vilivyo ndani ya Tanzania ili kuweza ku-attract watalii wengi waje. Wamefanya kazi nzuri sana, tumeona matangazo kwenye magazeti, kwenye majarida mbalimbali yaliyo ndani na nje ya nchi, tumeona kwenye mikutano wanatangaza, kwenye michezo wanatangaza, kwenye matamasha wanatangaza kwa kweli, wanafanya kazi nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utangazaji huu umeanza kuzaa matunda ndio maana tunaona sasa makundi mbalimbali ya watalii wanaingia kwa makundi kwa maelfu, kwa mamia, ndani ya Tanzania kuja kuangalia vivutio vilivyo kwetu, lakini vilevile imechangia kwenye pato la Taifa kwa sababu, kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri ametwambia kwamba, imechangia kwenye pato la Taifa takribani dola bilioni 2.4.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo kupitia TBC kwa kuweza kuanzisha chaneli ya utalii ambayo inaitwa Safari Chanel, kwa kweli hii ndiyo chaneli yetu ila sasa naomba tuiwezeshe iweze kuonekana hata nje kwa sababu tukiendelea kuiangalia sisi wenyewe, haitatusaidia. Nilikuwa nafikiri tuendelee vilevile kuboresha maudhui ya Safari Chanel ili iweze kuvutia watalii wengi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba tunaonyesha wanyama, mimea, maua na samaki wanaopatikana Tanzania lakini vilevile tuoneshe na hoteli nzuri za kitalii yaliyo ndani ya Tanzania kusudi yule mtalii sasa aone kwamba loh! Kumbe nikienda Tanzania naenda kulala kwenye hoteli nzuri kama hii, tunazo. Vilevile sisi wenyewe tuna utamaduni, ngoma za kitamaduni za kila mahali, tuiweke kwenye ile chaneli kuongeza ule mvuto wa ile chaneli kusudi watu wapende kuiangalia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, tuonyeshe ndege kubwa zinazotua ndani Tanzania; tuonyeshe KLM, Quatar Airways, Emirates, British Airways bila kusahau ndege yetu wenyewe ya ATCL kwamba inaweza kwenda ikabeba watalii na kuwaleta hapa, kwa kufanya hivyo basi tutaweza kupanua wigo na watalii watakuja wengi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kupandisha yaliyokuwa mapori ya akiba ya Biharamulo, Burigi na Kimisi ambayo sasa hivi imekuwa hifadhi inayoitwa BBR na kupandisha Ibanda, Rumanyika na sasa hivi inaitwa Hifadhi ya IR kuwa Hifadhi za Taifa. Kwa sasa mmekata mzizi wa fitina, kwa sababu tulikuwa tunakaa humu Wabunge tunachangia tunasema kwanini inaonekana utalii unakuwa promoted kwenye sehemu moja ya Tanzania ambayo ni kaskazini ilhali vivutio vipo katika sehemu zote? Sasa tunaloona mnaenda kutambua hivi vivutio kuviendeleza na kuendeleza utalii katika Kanda ya Ziwa, tunasema asanteni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hifadhi hizi za BBK na IR zinasambaa kutoka Chato ambayo iko katika Mkoa wa Geita kuja Muleba, Biharamulo, Ngara, Karagwe ambazo zipo katika Mkoa wa Kagera. Je, hifadhi hizi zitaendelea kuitwa kwa majina haya BBK na IR au mna mpango wa kuyapa majina mengine yanayovutia?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujio wa hifadhi una manufaa makubwa sana. Kwanza zipo karibu na mipaka, kule kwetu tunapakana na nchi ya Rwanda na zenyewe hifadhi zinapakana na Rwanda. Mnapoongeza ulinzi ndani ya hifadhi hizi ina maana kwamba masuala ya ulinzi na usalama katika hayo maeneo utakuwa umeimarika, watu wataweza kupita kirahisi bila kuogopa kutekwa. Vilevile uoto wa asili utakapoongezeka, uta-attract mvua kubwa itanyesha, ile milima iliyo ndani ya hifadhi ndiyo itakuwa inatiririsha maji kupitia Mto wa Kagera, Mto Mwisa, Msega kuingia kwenye Ziwa Victoria, kitakuwa ni chanzo kizuri cha maji kuingia ndani ya Ziwa Victoria halafu tunavuta tunapeleka Shinyanga, Tabora mpaka Singida kwa hiyo ni manufaa makubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutakuwa na mimea mbalimbali, samaki wapo mpaka sasa hivi kwenye maziwa mbalimbali yaliyo ndani ya hifadhi; Burigi, Ngoma, Nyarwamba, Kasinga, Nyamarambe na Victoria yenyewe ambao ni wa aina yake, ni adimu. Kwa hiyo, hii itavutia watu ambao wanaotaka kufanya masomo na utafiti watakuja Mkoa wa Kagera, watakwenda Mkoa wa Geita kwenda kujifunza. Ujio huu wa Hifadhi za Taifa utawapa vijana wetu ajira mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Maombi kwa Serikali. Kuna vikundi vya vijana; kwa mfano pale Muleba kuna kikundi cha vijana wanatengeneza vinyago, pale Ngara kuna kikundi cha wakina mama wanatengeneza table mats na vitunga mbalimbali, kuna watu Karagwe kule wanatengeneza vitunga, mikeka pamoja na Misenyi; tunaomba wawezeshwe, wapewe mitaji, wafundishwe ujasiriamali kusudi watengeneze vitu vizuri zaidi vitakavyokuja kuwapendeza hao wajasiamali na waweze kuvinunua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuboreshe miundombinu ya barabara zinazozunguka zile hifadhi pamoja na ndani. Kiwanja cha Ndege cha Chato pale, Kiwanja cha ndege cha Bukoba Mjini viendelee kuboreshwa, viwekewe taa kusudi sasa watalii wanaoingia kupitia Uganda, Rwanda na Burundi waweze kutua wakati wowote usiku na mchana na kufanya utalii ndani ya maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tuendelee kuwavutia wawekezaji; hii ni fursa kwa watu wa Mkoa wa Kagera na Mkoa wa Geita, tuone sasa hapa kuna fursa ya uwekezaji, twende tujenge hoteli, tutengeneze zile fukwe zipendeze, tuandae hoteli na mahali pa kulala watalii hao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mikoa ya Kagera na Geita ina urithi mkubwa wa historia ya Machifu Abakama, Ebikale; tunachoomba ni kwamba sasa twende tuyatambue maeneo haya yaendelezwe, inaweza ikawa kivutio kimoja wapo cha utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi kubwa ninaloomba, kwenye vijiji hivi na kata zilizokuwa zinazozunguka, hizi sasa ambazo zitakuwa hifadhi, watu hawa wamezoea kuingia kwenye hifadhi kukata miti kwa ajili ya kuni, kutengeneza mkaa na kuwinda, kuna haja ya kwenda kufanya mafunzo na ushawishi wa kutosha ili watu hawa waweze kuelewa umuhimu wa uhifadhi na hifadhi hizi. Mkishafanya hivi ina maana kwamba hawa watu wenyewe sasa ndiyo watakuja kuwa walinzi namba moja ya hifadhi hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri, Wizara, TANAPA, Ngorongoro Conservation Authority, TAWA, TFC na wadau wengine kwa kudhibiti ujangili. Wanyamapori walikuwa wanatoroshwa lakini sasa hivi hali imetulia, nawapongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tembo ni rasilimali ambayo tumepewa na Mwenyezi Mungu, inabidi tuitunze kwa ajili ya vizazi vijavyo lakini na kwa ajili ya dunia nzima. Mnamo mwaka 2009 inasemekana ndani ya Tanzania kulikuwa na tembo takriban 110,000 lakini wakaendelea kuuwawa kikatili na ujangiri na nini na kutoroshwa, ilipofika mwaka 2014 tulikuwa na tembo 43,000 tu kwa hiyo asilimia 60 yote walishauwawa. Lakini nawapongeza sana Wizara, Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri mmefanya kazi nzuri, mikakati mliyoweka na ulinzi mlioweka, sasa hivi tembo wameanza kuongezeka na tunaona data zinasema hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo linalojitokeza sasa hivi, tembo hawa wanahama kutoka kwenye makazi yao, wanakwenda kwenye makazi ya binadamu, wanafanya uharibifu kubwa, wanaharibu mazao ya wananchi lakini wakati mwingine wanaua hao wananchi. Nilikuwa napenda kujua je, Serikali imefanya utafiti kujua kwa nini hili tatizo ndiyo linajitokeza? Kwa nini tembo wameamua kuhama kutoka kwenye maeneo yao wanakwenda kwenye maeneo ya binadamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, mtu akiharibiwa mazao yake au akauwawa na tembo, fidia inasemaje? Mheshimiwa Waziri nilikuwa naomba ukija kuhitimisha utueleze. Vilevile Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba haya mambo sasa hayajitokezi tena, tembo wakae hukohuko kwenye mbuga/mapori kusudi wasiwaingilie binadamu, binadamu waendelee kufanya kazi zao? Sasa hivi ukiona sehemu mbalimbali wanaonesha kwamba hata watoto wanaogopa kwenda shule kwa sababu ya hawa tembo wanaohama na kuwafuata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa nasema Wizara hii ina majukumu makubwa sana, inabidi iongezewe bajeti ili waweze kuboresha utalii na utalii utaweza kutuletea Pato kubwa la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)