Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote na mimi naomba nichukue fursa hii kumshukuru kwanza Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia kuweza kushiriki vyema katika shughuli hii ya bajeti ya Wizara yetu ya Mifugo na Uvuvi. Pili, nikushukuru kwa kunipa fursa hii ya kuweza kuzungumza hapa na tatu, kwa namna ya kipekee kabisa, nimpongeze na kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuhakikisha kuwa wakati wote anaendelea kutusimamia na kuhakikisha kuwa nchi yetu inasonga mbele kwa yale yaliyokusudiwa katika Taifa letu ya kuwaletea maendeleo Watanzania.

Mheshimiwa Spika, nimshukuru pia Makamu wa Rais na Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maelekezo mazuri anayotupatia wakati wote na kutusimamia katika kuhakikisha tunamsaidia vyema Mheshimiwa Rais wetu. Kwa namna ya kipekee pia nimshukuru Mheshimiwa Waziri wangu Luhaga Joelson Mpina, Makatibu Wakuu wetu wote wawili wa Mifugo na Uvuvi Profesa Elisante Ole Gabriel na Dkt Rashid Tamatamah kwa namna tunavyoshirikiana na watendaji wote pale Wizarani katika kusukuma mbele gurudumu hili la Wizara yetu ya Mifugo na Uvuvi ambayo ni Wizara yenye tija kubwa na inayogusa Watanzania walio wengi na hapa leo Waheshimiwa Wabunge wamethibitisha jambo hilo pia.

Mheshimiwa Spika, pia niendelee kuwashukuru Kamati yetu ya Bunge na Wabunge wote waliochangia katika hoja hii inayotuhusu ya Wizara yetu ya Mifugo na Uvuvi kwa sababu tumepata wachangiaji wengi sana. Hii imetupa moyo mpana sana na kwa niaba ya Waziri wangu ni lazima nitoe shukrani kwa Waheshimiwa Wabunge wote kwa sababu hatukuamini kwamba tungeweza kupata wachangiaji wa namna hii wa kutushauri na kutuelekeza pia vile vile ya namna bora zaidi ya kwenda mbele hatimaye kuyapata matokeo tarajiwa kwa Watanzania.

Mheshimiwa Spika, sasa naomba nijielekeze katika hoja. Hoja zimesemwa nyingi sana na Waheshimiwa Wabunge katika upande wa Mifugo, lakini vilevile katika kupande wa Uvuvi. Nijielekeze kidogo katika upande wa Uvuvi; jana katika miongoni mwa wachangiaji waliochangia na mmoja leo amerudia kuonesha kuwa katika kipindi chote tulichohudumu Serikali ya Awamu ya Tano, haijafanya jambo lolote katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi katika sekta hii ya Uvuvi.

Mheshimiwa Spika, nataka niwaambie Waheshimiwa Wabunge kwamba watembee kifua mbele, yako mambo ya msingi tuliyoyafanya na mimi ninayo Ilani ya Uchaguzi hapa na nitaeleza baadhi ya mambo ambayo Serikali ya Awamu ya Tano imeyafanya. Wabunge waliopata nafasi na kusema kwamba hakuna kilichofanyika, kwanza nianze na ibara hii ya 27 ya Ilani yetu ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, eneo la (p); kuendelea kupambana na uvuvi haramu ili uvuvi uwe endelevu na wenye tija. Jambo hili Waheshimiwa Wabunge wengi wanaweza kuwa wasijue kuwa limeandikwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Spika, Chama cha Mapinduzi kinataka samaki tulionao leo tuendelee kuwa nao kesho na hata vizazi vyetu vikute samaki hawa na ndiyo maana kikaelekeza Serikali yake kwamba tulinde rasilimali zetu hizi. Sisi tumeifanya kazi hii kama ni kazi ya kipaumbele katika kulinda rasilimali za nchi yetu ziinufaishe nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, nataka nikuhakikishie wewe mwenyewe na Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote, jambo hili limeleta tija kubwa sana. Uvuvi haramu kwa upande wa bahari ya hindi ulikuwa umekithiri, ulikuwa ni uvuvi wa mabomu, leo katika upande wa bahari ya hindi hauwezi kusikia bomu linapigwa kuanzia Tanga MOA, hadi Mtwara kule Msanga Mkuu hakuna bomu linalopigwa. Tumedhibiti kwa zaidi ya asilimia 99, hakuna bomu linalopigwa na Watanzania wa upande wa huko pwani wameanza kusahau habari ya bomu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haya ni mafanikio makubwa bomu liliua watu, bomu lilitishia hata usalama wa baadhi ya miundombinu yetu ikiwemo hata bomba letu la gesi linalotoka Songosongo kuja Somanga kwa ajili ya gesi inayoenda kuzalisha umeme pale Kinyerezi, sisi tumeweza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine mmoja kati ya wachangiaji jana alikuwa anazungumzia juu ya ujenzi wa bandari ya uvuvi. Katika kazi tuliyoifanya kipindi hiki ni kufufua shirika letu la TAFICO, hii ni hesabu nyepesi sana tu. Tumenunua ndege, tusingeenda kununua ndege, isipokuwa kwanza tuwe na shirika imara la kuzisimamia zile ndege, ndiyo maana tukaimarisha ATC, hatuwezi kwenda kununua meli, nani atakayezisimamia zile meli, ndiyo maana tukasema ni lazima tufufue TAFICO. Ufufuaji wa TAFICO ndiyo utakaokwenda kusimamia zile meli tunazozitegemea kuzinunua.

Mheshimiwa Spika, nataka niwapeni habari njema TAFICO imefufuka tena mwanamama mmoja mahiri tumempa kazi ya kuhakikisha TAFICO inafanya vyema. Tumetambua mali zote za TAFICO na TAFICO sasa ipo na imeanza kazi na tayari tuna uhakika wa kupata takriban kiasi cha shilingi bilioni nne kununua meli, meli ambazo zitafanya kazi ya kuvua katika maji yetu ya ndani kwanza, tunafanya hivyo kwa nini?

Mheshimiwa Spika, tunafanya kwa sababu tunataka tuioneshe dunia kwamba tunazo rasilimali, tuwavute wawekezaji, watu walikata tama, hawawezi kuamini kwamba hapa katika maji yetu sisi wako samaki, mwekezaji wa kuweka kiwanda au mwekezaji wa kuleta meli haji tu bila ya kuwa na uhakika wa kuweza kufanya investment ile ambayo anaweza kwenda kuifanya pale.

Mheshimiwa Spika, sisi tumetengeneza mkakati na hivi leo TAFICO inatengeneza business plan ya kisasa ambayo itakwenda kuhakikisha kuwa inaingia hata mikataba. Tunao Wakorea, wameonesha nia ya kushirikiana na TAFICO na tutakwenda kujenga bandari ya uvuvi. Hao Wajapan pia vile vile wameonesha nia ya kushirikiana na TAFICO ambayo itaenda kutuletea tija katika shughuli hizi za uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika Ilani pia ya Uchaguzi imetuelekeza juu ya kuhakikisha kuwa tunalinda matumbawe yetu, maeneo ya mazalia ya samaki kwa upande wa kule pwani, hili tumefanikiwa. Kwa nini tumefanikiwa? Upande wa kule pwani tumedhibiti, watu wa Kilwa hapa kama wapo wananisikia na watahakikisha kwamba jambo hili ni la ukweli wa kiasi gani. Pale Kilwa tumedhibiti miamba yetu. Pweza walikuwa wakipatikana kwa uchache sana, pweza ni biashara ambayo inauzwa ndani, lakini tuna-export pia vile vile kwa kupitia mradi maarufu wa SWIOFISH, tumefanikiwa kudhibiti na sasa wanapata mazao ya kutosha watu wa kule pwani kwa ajili ya kuweza kuinua maisha yao, hiyo ni kazi yetu sisi.

Mheshimiwa Spika, Ilani imetuelekeza pia vile vile tutengeneze matumbawe yasiyokuwa ya asili ambayo tumeyatengeneza pale Bagamoyo na kule Nungwi, tumepeleka ya kutosha, hizi zote ni kazi tulizozifanya.

Mheshimiwa Spika, Ilani katika eneo (d) linatuelekeza sisi kuimarisha Masoko yetu ya Feri na kuimarisha Masoko yetu ya Kirumba. Katika jambo tulilofanikiwa ni hilo, tumeimarisha Soko letu la Feri na tumeimarisha Soko letu la Kirumba. Kirumba kabla sisi hatujaingia katika kupewa dhamana hii na Mheshimiwa Rais, nataka niwahakikishie ni eneo ambalo lilikuwa linakwenda vizuri, lakini sivyo kama tunavyokwenda hivi leo. Kirumba sasa inakusanya kwa mwezi mmoja milioni 600, eneo ambalo tulikuwa tunakusanya milioni 30; kutoka milioni 30 mpaka milioni 600 kwa mwezi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hi kuwashukuru na kuwapongeza sana watendaji wote, Mheshimiwa Mbunge wa Ilemela Dkt. Angelina Mabula na wengine wote pale Mwanza kwa namna walivyotuunga mkono katika kuhakikisha Soko la Kirumba linafanya vizuri. Soko la Kirumba limetengenezewa mzani wa kisasa, unapima mazao yetu yote yanayoingia pale. Tulikuwa tunapoteza pesa nyingi sana kama Serikali, hivi leo tunafanya vizuri. Pale feri tunafanya ukarabati mkubwa sana, tunapeleka zaidi ya bilioni 1.5 pale kulifanya Soko la Feri liwe soko la kisasa, nani anasema Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi haijatekelezwa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo nilimtaka awepo hapa ili nimwoneshe kwa namna gani, kazi kubwa tuliyoifanya. Wabunge wa Chama cha Mapinduzi litakapokuja suala la Uvuvi, nawaomba watembee kifua mbele, Serikali ya Awamu ya Tano ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imefanya kazi kubwa na itaendelea kufanya kazi kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, upande wa mifugo, nataka nikuhakikishie kwamba tumefanya kazi kubwa. Jambo moja amelisema jana Mheshimiwa Mbunge Jackline Msongozi, naomba niende na hilo tu, mwaka 2016/2017, wakati Mheshimiwa Rais anakwenda kutembelea pale Tanga alipita katika Kiwanda cha Tanga Fresh akaona liko tatizo la ardhi na mtaji wao ni mdogo, akawawezesha. Wale watu wa Tanga Fresh hawakuwa wanazalisha maziwa ya long life, hivi leo wanazalisha maziwa ya long life, tunajivunia, hata maziwa ya kutoka nje yasipokuwepo Tanga Fresh na ASAS wote tumewawezesha sisi. ASAS wamewezeshwa kupitia ubunifu, ubunifu uliofanywa na Waziri wangu Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina, tumeanzisha dawati la sekta binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, dawati la sekta binafsi tumelizindua sisi wenyewe mwaka jana mwezi wa 10, limeleta tija kubwa, limesaidia viwanda vya nchi hii, limesaidia wavuvi wa nchi hii, tuna ushirika leo. Ushirika unajibu Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, ushirika pale Kikumba Itare tumewapelekea milioni tano, nimekwenda kukabidhi mimi mwenyewe. Pale Igombe, Mwanza tunawapelekea milioni tano, anakwenda kukabidhi Mheshimiwa Waziri. Tumepeleka kila mahali, tunainua ushirika na kama haitoshi tumepeleka hata pembezoni ambako wanakwenda kufanya mabwawa, pale Peramiho kwa Mheshimiwa Jenista tumekwenda kuwasaidia waweze kuanzisha mabwawa ya ufugaji wa samaki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeanzisha Chama Kikuu cha Ushirika katika nchi ambacho kinawaunganisha wavuvi wote kwa lengo na nia tuwakopeshe zana za uvuvi, tuwasaidie wakopeshwe pesa na mabenki waweze kupata tija ya kazi yao wanayoifanya.

Mheshimiwa Spika, naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wote kazi inaendelea na sisi hatutakata tamaa katika kuhakikisha kazi hii tuliyopewa ya kulisogeza Taifa letu mbele, ya kumuunga mkono Mheshimiwa Rais, hatutarudi nyuma, tutaendelea kusonga mbele, upungufu ule mliotueleza sisi kama wanadamu tutaufanyia kazi katika kuhakikisha kuwa Taifa letu linasonga mbele katika rasilimali zake hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa muda huu wa kuweza kuchangia. (Makofi)