Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. James Kinyasi Millya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Simanjiro

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Spika, nami nimshukuru Mungu kwa nfasi hii, lakini kipekee kwa sababu ndiyo nasimama kwa mara ya kwanza tangu tumpoteze Mheshimiwa Mzee Mengi, marehemu, niendelee kumuombea Mungu ailaze roho yake pema peponi. Alikuwa kiongozi mzuri sana.

Mheshimiwa Spika, niwapongeze watumishi wa Wizara wamefanya kazi nzuri sana. Mheshimiwa Mpina alipita juzi Simanjiro na akongea na wafugaji halafu akakagua baadhi ya mabwawa yetu na Mheshimiwa Waziri ukasema utasaidia fedha kwa ajili ya kuboresha yale mabwawa. Mimi kama Mbunge wa eneo hilo nikushukuru, lakini niishukuru Serikali yangu sana kwa kuwajali wafugaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimshukuru Katibu Mkuu wa Wizara hii, Profesa Ole-Gabriel. Siku fulani mifugo ya Simanjiro ilikamatwa kwenye Pori Tengefu la Mkungunero, yeye na Naibu Waziri, Mheshimiwa Ulega, walikuwakilisha vizuri, walitusaidia ng’ombe 540 na punda 10 wakaondoka mikononi mwa hifadhi, kwa negotiation za Wizara, na mimi kama Mbunge ambaye napenda kushukuru kwa yale ambayo yamefanywa na Serikali ninawashukuru sana yeye pamoja na viongozi wa TAMWA kwa ujumla na viongozi wa Wizara ya Maliasili, wametusaidia na mifugo ile iko huru. Ninawashukuru na wafugaji wa Simanjiro wanawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimshukuru Mheshimiwa Rais, tuendelee kumpa moyo sana kwa kazi kubwa anayowasaidia wafugaji. Wafugaji wengi wako hapa, kwenye hizi gallery zote wafugaji wapo. Mheshimiwa Rais ametamka kwamba wakati tunapata uhuru wa nchi yetu taifa lilikuwa na wakazi na Watanzania milioni tisa tu na mifugo ni michache, tumeongezeka kwa takribani milioni 55. Baada ya kuona haja hiyo, ameona yale maeneo ambayo wahifadhi hawayatumii kwa ajili ya mbuga za wanyama amesema kwa upendo mkubwa wa wafugaji yagawiwe, ifanyike timu maalum ya Mawaziri imepita ili wafugaji wapate maeneo hayo. Huu ni upendo gani kwa mkuu wetu wa nchi, anatupenda sana. Mimi kama mfugaji na Mbunge anayetokana na CCM nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, wafugaji wamelipokea hili kwa mikono miwili. Anapenda na wafugaji wako na yeye siku zote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine; kuna ugonjwa unaitwa ugonjwa wa ndigana. African Union miaka fulani pale Adis Ababa waliamua kujenga kiwanda cha kuzalisha dawa ya ndigana pale Malawi; lakini hapa nchini mtu aliyepewa tenda hiyo ni mtu anaitwa Dokta Mbwile. Ninapoongea leo mifugo katika Ukanda wote wa Simanjiro, Arusha, Manyara wanakufa kwa sababu dawa hii haipo sokoni. Wizara sijui mmetumia hekima gani, mnatoa tenda hii kwa mtu mmoja tu nchi nzima. Niiombe Wizara kama ushauri hii tenda igawiwe kwa watu wengine kwa sababu, ule ugonjwa ukimshika ndama au ng’ombe haiwezekani kumtibu tena. Ninawaomba mfikirie namna ya kuongeza wadau wa kuchukua dawa hii kutoka Malawi wailete Tanzania.

Mheshimiwa Spika, la pili; maeneo ya wafugaji ni maeneo makame sana, yanapokea mvua kidogo kila mwaka. Namna pekee ya kuwasaidia wachungaji na wafugaji kwa ujumla nchi hii ni kuanzisha mabwawa makubwa.

Mheshimiwa Spika, wakati wa uhuru kulikuwa na mabwawa, natoa mifano miwili, Kata ya Narkawo na Kata ya Komolo pale Skuro; mabwawa ambayo Mheshimiwa Waziri wa Mifugo ulitembelea; ni mabwawa makubwa ambayo Mheshimiwa Nyerere, Baba yetu wa Taifa aliyaanzisha kwa ajili ya kuwasaidia wafugaji. Kwenye maeneo mengi ya wafugaji ardhini hakuna maji, mtusaidie tupate mabwawa makubwa kila eneo ili wafugaji wapate nafuu ya adha ya ufugaji wao.

Mheshimiwa Spika, lingine ni migogoro ya wafugaji. Migogoro hii imekuwa kero. Nimesoma jitihada za Wizara, wamefanya vizuri, maana wametembelea Wilaya za Uvinza, Kasulu, Kibondo, Katavi, Kalambo, Nkasi na Sumbawanga. Niombe, nchi hii migogoro ya wafugaji na wakulima mingi imekithiri eneo la Morogoro; mtusaidie sana Morogoro, muipe kipaumbele Morogoro. Na kwa sababu nimeona mmewashirikisha akina nani, niombe Kanisa la Kilutheri la Kiinjili la Tanzania pale Morogoro mlihusishe. Kuna Askofu mmoja pale anaitwa Askofu Mameo; ni mtu mwema anaweza kuisaidia Serikali kwa ajili ya kutatua tatizo hili la wafugaji na wakulima.

Mheshimiwa Spika, jana nimefarijika sana nimeongea na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kilimo na yeye anasema yupo tayari kuingia Morogoro kwa sababu ni mkazi wa Morogoro na kusaidia migogoro hii kwisha. Kwa hiyo, shirikianeni na Naibu Waziri wa Kilimo yuko tayari kusaidia sana.

Mheshimiwa Spika, lingine; Ranchi za Taifa kwa awali kabisa zimechukuliwa kutoka kwa wafugaji. Leo hii kwa takwimu Ranchi za Taifa zinamiliki hekta laki mbili kwa mifugo elfu 30 tu. Kwa sababu kuna ranchi nyingine hazitumiki na Serikali wafikirie namna gani ya kuwagawia wafugaji, lakini wangalie, waweke angalizo moja, wasiwape watu wenye nguvu tu, wachukueni wafugaji wa kawaida wagawiani ranchi hizi. Kuna Kilimanjaro kule, kuna hapa Mpwapwa, kuna nyingine Kanda ya Ziwa. Mtusaidie wafugaji ili tuondokane na hizi shida na kumsaidia Mheshimiwa Rais ili hatimaye tusipate shida ya mifugo.

Mheshimiwa Spika, Kuhusu Suala la Maziwa. Ninaipongeza sana Wizara kwa kuamua kulinda viwanda vya ndani. Leo hii pale Arusha ukijaribu kununua Brookside au maziwa ya Afrika ya Kusini ni bei ghali sana. Kwa hiyo Wizara nia yake na Serikali ni kukuza viwanda vya ndani. Nimeona maziwa yetu ya Azam, maziwa yetu ya Tanga Fresh, kama Mheshimiwa Rais alivyotembelea, yanaanza kupata soko kwenye nchi yetu. Endeleeni hivyo hivyo tuwaunge mkono wazalishaji wa maziwa, nendeni chini muwagundue wengine ambao wanataka kuanzisha biashara hii wapeni support.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo niombe linguine. Juzi nimeona clip moja, na mimi nilisema mara nyingi sitaki kuongelea upinzani sana, lakini mara nyingine wanapoanza kufanya siasa za ajabu inabidi mtu uondoke kwenye mstari ambao hukutaka kuukanyaga. Nimemwona Mwenyekiti wa Taifa wa Chama kinachoitwa CHADEMA. Mheshimiwa Mzee Lowasa alipoondoka na kurudi nyumbani kwake CCM aliwashukuru CHADEMA na akanyamaza; lakini cha ajabu sana Mzee Mbowe juzi anasema Lowasa ameondoka na mke wake peke yake. Ninaomba apate ujumbe mzuri huu, kura za Serikali za Mitaa mwaka huu mtaona jibu lake, kwamba CCM imara ile ambayo tunaijua kuanzia miaka ya elfu mbili, sabini, sasa mtaiona. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Ole-Millya. Nakushukuru sana asante.

MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Spika, na naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)