Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Frank George Mwakajoka

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Tunduma

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia. Wabunge wote ambao wamezungumza ndani ya Bunge asilimia kubwa wamejaribu kuzungumzia hali halisi ambayo inajitokeza kwa wananchi wetu hasa ambao wanajishughulisha na suala la uvuvi na ufugaji.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na malalamiko makubwa sana; kwa mfano, Tunduma pale leo, tangu juzi, jana, leo, pamoja na mimi kukutana na Mheshimiwa Waziri na kujaribu kumweleza, lakini hali kwa kweli Tunduma ni mbaya sana. Sasa hivi Wananchi takribani 20 walikuwa wamekamatwa na wamewekwa ndani, ambao wanajihusisha na biashara ya samaki na dagaa. Vilevile wananchi hawa wanadaiwa dola 1.5, lakini pia waepigwa faini zaidi ya milioni mbili, milioni moja na nusu, sababu kwa nini wanafanya biashara na wageni ambao wanatoka Congo na wageni ambao wanatika Zambia. Jambo hili kwa kweli limetusikitisha sana.

Mheshimiwa Spika, na mwaka uliopita tulijaribu kumweleza hata Mheshimiwa Waziri; kwamba sheria hizi ambazo zimeonekana zinaleta unyanyasaji sana kwa wananchi na zinarudisha nyuma juhudi za wananchi ambao wameamua kufanya biashara ya samaki na dagaa tulimwomba azilete Bungeni ziweze kufanyiwa mabadiliko. Kwa kweli sheria hii imekuwa ni kikwazo kikubwa sana kwa wafanyabiashara.

Mheshimiwa Spika, na ukijaribu kusoma hata Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, ukisoma Kifungu cha 27 Kifungu Kidogo cha (n), Ilani inasema itawawezesha wavuvi wadogowadogo pamoja na wafanyabiashara kuhakikisha kwamba wanafnya shughuli zao vizuri bila kubughudhiwa na ikapunguza pia tozo mbalimbali ambazo zimekuwa ni kikwazo kikubwa kwa wavuvi hawa pamoja na wafanyabiashara wadogo.

Mheshimiwa Spika, lakini huwezi kuamini, sasahivi imekuwa ni kero Kanda ya Ziwa huko watu wanalia, lakini bado maeneo ambayo wanakwenda kufanya biashara. Kwa mfano Bahari Kuu, ukienda eneo la Pwani pamoja na Zanzibar wanapokuja kufanya biashara hizi imekuwa ni tatizo kubwa, lakini mpaka wawekezaji. Kwa mfano kwenye Mji wa Tunduma kulikuwa na eneo zuri kabisa la uwekezaji watu wanatoka Zambia, Congo, Angola na maeneo mengine walikuwa wananunua samaki pale, lakini leo huwezi kukuta watu wanakuja kununua pale. Sasahivi atu wanakimbiakimbia wanakamatwa, wavuvi wetu pamoja na wanaoleta dagaa pale na samaki, lakini pia wafanyabiashara wa pale wanakamatwa hovyo hovyo. Sasa tunataka kumuinua Mtanzania wa namna gani? Tunataka kumwinua masikini wa Kitanzania wa namna gani?

Mheshimiwa Spika, kama mtu anajiwezesha mwenyewe anakwenda anatafuta mtaji anaamua kufanya biashara ya samaki, anaamua kufanya biashara ya dagaa, lakini anakuwa ananyanyasika katika nchi yake anashindwa kufanya biashara hii; hivi Serikali ya Chama Cha Mapinduzi ndivyo ilivyojiandaa namna hii?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi naomba sana, kwa kweli jambo lililotokea Tunduma ninaomba Mheshimiwa Waziri alishughulikie haraka iwezekanavyo kwa sababu limeleta tatizo kubwa, limeleta tafrani kubwa. Wananchi wameshindwa kukaa, wananchi wameshindwa kufanya biashara na wageni ambao waliokuja kufanya biashara pale sasa wameamua kuondoka; sasa tunajenga nchi au tunabomoa nchi?

Mheshimiwa Spika, na leo tunakuwa humu ndani ya Bunge tunasema kila wakati kuwa tunahitaji wawekezaji waje katika nchi hii kuja kuwekeza; kama wafanyabiashara wa ndani wananyanyaswa wanashindwa kufanya biashara, hivi wawekezaji kutoka nje wanatoka wapi? Hiki ambacho tunakizungumza hakina uhalisia kabisa. Kwa hiyo, mimi nomba sana wafanyabiashara wangu kwenye Mji wa Tunduma, Mheshimiwa Waziri aweze kutoa maelezo ni namna gani wafanyabiashara hawa wataachiwa kutoka ndani, lakini pia hizi faini ambazo zinapigwa, milioni mbili, milioni tatu, wanapigwa wajasiriamali wadogo kabisa, maana yake nini katika Taifa hili? Kwa kweli, kumekuwa na tatizo kubwa sana kwenye Mji wetu wa Tunduma, lakini pia sheria hizi za uvuvi imekuwa ni unyanyasaji mkubwa sana kwenye Taifa hili.

Mheshimiwa Spika, lakini jambo lingine, ukisoma kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, waliahidi kwamba mpaka miaka mitano inakwisha watahakikisha kwamba wananunua meli tano za uvuvi, lakini mpaka leo hakuna meli hata moja iliyonunuliwa na bado mwaka mmoja. Sijui tafsiri yake ni nini; kwamba Ilani ya Chama Cha Mapinduzi haitekelezeki au Ilani imeachwa kama ambavyo ilikuwa inadanganya wananchi wapige kura halafu baadaye waachwe? Kwa sababu tulikuwa tumeambiwa katika ilani, ukisoma kulikuwa na meli tano zilitakiwa zinunuliwe, lakini hata meli moja haijanunuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia huwezi kuamini katika taifa hili tuna utajiri mkubwa sana wa samaki, lakini kitu kinachoendelea samaki wanaoagizwa nje kila mwezi wana thamani ya bilioni 56, kila mwezi ambayo ni sawa na dola milioni 25. Pia kwa mwaka mzima tunatumia fedha bilioni 672 kuagiza samaki nje ilhali tuna maziwa na bahari yetu tunakoweza tukapata samaki kwa wingi. Sasa Serikali lazima ijaribu kuangalia, tunapoteza fedha nyingi kwenda kununua samaki nje, tunanunua China, tunanunua Vietnam, lakini samaki tunao; tuna maziwa, tuna bahari, lakini tunakwenda kununua samaki nje. Jambo hili Serikali iliangalie kwa umakini sana; kwa sababu kama tutaendelea kufanya haya tafsiri yake ni kwamba, tutakuwa hatulitendei taifa hili haki.

Mheshimiwa Spika, lakini pia tumesikia taarifa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, tumeona kabisa wanasema kwamba maduhuli yamepanda sana, lakini ukweli maduhuli haya ni mateso makubwa kwa Watanzania ambao walitegemea neema na nuru kutoka kwenye Serikali hii. Hali ni mbaya sana, Kanda ya Ziwa huko kuna watu wamefilisika kabisa, Kanda ya Ziwa huko kuna watu wamekimbia nchi hii kwa sababu tu ya sheria ambazo tumezipitisha ndani ya Bunge hili. Ninaomba sana sheria hizi zibadilishwe kwa sababu sisi ni Wabunge tunatunga sheria, sheria hizi zikibadilishwa ziwe rafiki kwa Watanzania ambao wamejiingiza kwenye sekta ya uvuvi pamoja na ufugaji. (Makofi)