Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi)

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana; kwanza naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapambano dhidi ya uvuvi haramu; nichukue nafasi hii kuipongeza sana Wizara, Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana, Naibu Waziri na delegation yake yote, hongereni sana kwa kazi nzuri ya mapambano dhidi ya uvuvi haramu. Mapambano haya yameleta tija sana katika nchi yetu lakini pia niwapongeze sana kwa kuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato, asilimia 150 haijapata kutokea, hongereni sana. Wizara ina vijana makini wanafanya kazi kwa weledi na ndiyo maana Wizara inaoneka sasa ina uchechemuzi, mambo yanaenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika tano ni chache sana lakini naomba kwa ruhusa yako utaniongeze kidogo ili niweze kumalizia. Niwashauri sasa Mheshimiwa Waziri na delegation yake, wazingatie sana ushauri ambao Waheshimiwa Wabunge wanautoa humu ndani dhidi ya mapambano ya uvuvi haramu. Ushauri huu utawasaidia sana kuboresha na kuongeza tija katika Sekta hii ya Uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye Ziwa Nyasa; kupitia suala la uvuvi haramu kwa maana ya ushauri ambao nataka kuutoa. Uvuvi haramu pia umeathiri sana katika Ziwa Nyasa, ndugu zetu wavuvi katika Ziwa Nyasa wamepata shida kwenye suala la nyavu, nao pia wamechomewa nyavu. Kwa hiyo, niombe wale wavuvi wamechomewa nyavu kupitia zao la samaki, lakini pia zao mahsusi sana la samaki anaitwa kituhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kituhi ni samaki mdogo sana, mtamu na mwenye virutubisho vingi sana, lakini huyu kituhi kwa umbile lake ni mdogo, ndivyo alivyo. Ni sawasawa na binadamu na sisi nao tuna maumbile tofauti tofauti, huwezi kwamba huyu ni mfupi, basi ni mdogo basi siyo binadamu kamili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka niseme samaki anayeitwa kituhi ni mfupi anafikia inchi karibu mbili au tatu. Kwa hiyo, sasa imekuwa ni shida, wavuvi wemechomewa nyavu na kwamba samaki huyu hawezi kuvuliwa. Sasa nataka niseme hivi Mheshimiwa Waziri kwamba naomba atambue wazi kwamba yule samaki hivyo alivyo ndivyo alivyo, kwa hiyo, naomba arudi Ziwa Nyasa akafanye mambo ambayo yatakuwa yanaleta uzalishaji wenye tija katika Ziwa Nyasa. Pia kutokumvua huyu samaki maana yake Mheshimiwa Waziri na delegation yake wanataka sisi Wangoni tuwe wadumavu. Samaki huyu anatusaidia sana kutustawisha kama mnavyotuona katika Bunge hili tumestawi na tumenawiri barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la josho katika Kata ya Linga, naomba Mheshimiwa Waziri atume watu wake kule katika Kata ya Linga kuna wafugaji wengi lakini hakuna josho, tunataka...

MWENYEKITI: Nimekuongezea dakika mbili.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba pia tupate mabwawa ya ufugaji wa samaki. Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake, kule Ruvuma kuna mama zao na vijana wenzao, wanahitaji kuwekeza kwenye mabwawa ya samaki. Tunawaomba sana waje wafanye uwekezaji kule wawasaidie ili waweze kufanya uwekezaji kwenye mabwawa ya samaki. Pia, walete ng’ombe na sisi tunahitaji kufuga, walete ng’ombe sisi tutawasimamia na umeme sasa hivi wa gridi upo, hivyo tunahitaji kuweka viwanda ili tufanye uchakataji kwenye viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa ziara yake aliyoifanya Mkoani Tanga kwenye Kiwanda cha Tanga Fresh. Alipofika kule alikuta kuna changamoto kubwa sana ambayo ilikuwa ni kikwazo kikubwa sana cha kukuza uzalishaji katika kiwanda kile hasa kwenye uzalishaji wa maziwa ambayo ni UHT, haya maziwa ni mazuri lakini pia yana uwezo wa kutunzika kwa muda mrefu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Rais alichokifanya alikwenda kuondoa changamoto ya suala la ardhi kwenye kiwanda hicho, akatoa maelekezo ardhi ile wakaipata na wakaenda kukopa wakapata bilioni 10. Sasa hivi wamefanya uwekezaji mzuri na leo kila Mbunge hapa alishika kamfuko amepata maziwa, Magufuli oyee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakwenda kwenye Kiwanda cha Asas, nao pia niwapongeze sana kwa uzalishaji mzuri sana wa maziwa ya UHT. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze Wizara kwa kusimamia kuhakikisha kwamba kunakuwa na viwanda vya uchakataji wa nyama; Kiwanda cha Kibaha na Longido, hongera sana wako vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba niseme hivi, nawapongeza tena kwa kuhakikisha kwamba wanaweka mkataba kati yao na nchi ya Misri, Misri wanakuja kuchakata hapa nyama lakini pia Misri wanakuja kuwekeza kwenye ngozi, tutapata ngozi zetu lakini pia tutaweza kutengeneza mikoba, mikanda na mambo mengine… (Makofi)

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu…

MWENYEKITI: Ahsante sana, Mheshimiwa Jacqueline.

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama wenzetu Ethiopia wameweza…

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: …kama wenzetu Ethiopia wameweza, sisi tunashindwaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno haya nakushukuru sana, naomba…

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Jacqueline.

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ametushtua anasema UTI, kuhusu utaratibu.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, nani kama Dkt. John Joseph Pombe Magufuli. Waheshimiwa Mawaziri oyeee. (Makofi)