Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Hasna Sudi Katunda Mwilima

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia kwenye Wizara hii muhimu sana, Wizara inayoshughulika na masuala ya uvuvi pamoja na mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jimbo langu mimi asilimia kama 70 hivi au 65 wanajihusisha na masuala ya uvuvi; lakini hapo hapo tena asilimia hiyo hiyo au zaidi wanajihusisha na masuala ya mifugo. Kwa hiyo nitachangia mambo yote mawili; lakini kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri na timu yake yote ya Wizara kwa namna ambavyo wameweza kuwasilisha taarifa ambayo inatupa matumaini. Nina imani wavuvi na wafugaji wanaweza wakaona mwanga mpya unaotaka kuja katika Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na suala la uvuvi. Kulifanyika operesheni kwenye Ziwa Tanganyika, wavuvi wetu wakatupigia simu Wabunge na mimi nikamuona Waziri pamoja na Naibu Waziri. Nitoe shukrani zangu za dhati kwamba jana walitupa nafasi ya kuwasikiliza wavuvi zaidi 35 kutoka Ziwa Tanganyika, na tatizo kubwa ilikuwa ni uvuvi kwa kutumia ring net.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru kwamba jana tulimaliza mazungumzo salama, lakini bado wale wavuvi wanahitaji kurudishiwa nyavu zao saba ambazo zilishapimwa kwenye ile operesheni ya kwanza na zikaonekana zinafaa. Nashukuru kwamba Mkurugenzi amewaita kesho asubuhi saa mbili ili aweze kukutana nao. Sasa naomba nyavu zao zirudishwe, mashine zao zirejeshwe kwa sababu ndicho wanachokitegemea kupata kipato kwa dhana hizo zilizoshikiliwa nje ya utaratibu na nje ya Sheria ya Uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimzungumzie, Mheshimiwa mwenzangu amesema siyo vizuri kumtaja mtu mimi naomba nimtaje. Namtaja kwa sababu Mheshimiwa Tizeba aliyekuwa anamlenga ni yuleyule mama anayeitwa Judith ambaye leo mmetuletea kwenye Mkoa wetu wa Kigoma. Wabunge wote hapa nyuma, Mbunge wa Ukerewe, Mbunge wa sengerema, Mbunge wa wapi sijui wote wanazungumza kuhusiana na huyu Mama Judith. Huyu mama anaripoti kila mwezi TAKUKURU kutokana na madudu aliyoyafanya Mwanza. Leo mtu anayeripoti TAKUKURU kwa madudu aliyoyafanya Mwanza mnatuletea Kigoma kuja kuua uvuvi na wanachi wanategemea hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri mimi nakufahamu, wewe ni msikivu na ndiyo maana ulitupa nafasi ya kutusikia pale Wizarani jana; huyu mama tafuta pa kumpeleka siyo Kigoma, Kigoma hatumtaki. Kama alitoka Mwanza akaletwa Kigoma na Kigoma hatumtaki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu gani, anakamata hizo ring net…..

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Heche.

T A A R I F A

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumpa dada yangu Hasna taarifa hivi ule utaalam wa Kigoma siku hizi hawatumii mpaka…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Hasna umemsikia? Taarifa yako haijasikika Mheshimiwa Hasna endelea.

MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Heche huwa anapenda kila nikisimama kunipa taarifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, muda wangu hizo dakika kidogo naomba zilindwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu mama ametumwa kutekeleza kazi kwa mujibu wa sheria lakini amefika kule anaharibu utaratibu mzima wa uvuvi kwenye ziwa lote la Tanganyika, kwa maana ya Kigoma, Katavi na eneo kidogo la Rukwa. Jana amewaita baadhi ya wavuvi wa Kigoma Mjini wakiongozwa na mtu anaitwa Francis Kabure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu Francis ni Mrundi, mimi nimepiga simu Kigoma nikauliza huyu mtu ni Mtanzania, wananiambia ameshaomba uraia zaidi ya mara tatu bado hajapewa uraia. Mheshimiwa Waziri swali langu hivi Sheria ya uvuvi inasemaje kuhusiana na mtu ambaye si raia na anapewa cheo cha kupambatizwa kwamba yeye ndiye Mwenyekiti wa Wavuvi Mkoa wa Kigoma kachaguliwa na Judith kwa maslahi yapi? na amemleta mpaka Dodoma na ushahidi tunao na jana amekaa kikao na Mkurugenzi wa Uvuvi. Japo Mkurugenzi ni haki yake kuwasilikiza hilo mimi siwezi kuhoji, lakini je, ana maslahi gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri huyu mama hatumtaki tunaomba utuondolee pale Kigoma, tafuta pa kumpeleka. Kwanza hana sifa ya kuendelea kuwa msimamizi iwe Nyasa, iwe Victoria iwe Tanganyika kwa sababu tayari anashutuma za rushwa ndani yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hili niendelee kuishukuru pia Wizara. Jana tulikuwa tunazungumzia masuala ya tozo; suala hili la uvuvi linatozo nyingi sana. Naomba Mheshimiwa Waziri kwenye mabadiliko ya kanuni ujaribu kuangalia kidogo hizi tozo mvuvi analipa, mtumbwi unalipwa, akisafirisha dagaa analipa. Jaribu kuziweka iwe ni win situation, Serikali mpate na sisi pia tupate.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie mifugo kwa haraka haraka kabla kengele nyingine haijapigwa. Kuna suala hile…..

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Hasna kengele ya pili hiyo nakuachia kidogo umalizie, hii ni ya pili.

MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru naomba suala moja tu la Mwanduhu Bantu. Nimeona hapa Mheshimiwa anaonesha Uvinza kuna ekari kama 49 kwa ajili ya kugaiwa wafugaji. Mheshimiwa Waziri ulikuja ukatoa maelekezo eneo la Mwanduhu Bantu umeriridhia tuendelee nalo kama halmashauri tugawe vitalu, wafugaji wagawiwe na wakulima wagawiwe. Naomba utakapokuja kuwasilisha kesho uweze kutupa tamko rasmi, ni lini sasa umeturuhusu ili tuweze kupata mapato haya na wewe pia Wizara yako itapata mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya naendelea kumpongeza Waziri, Naibu Waziri, Makatibu Wakuu wote pamoja na Mkurugenzi wa Idara hii ya Uvuvi, ahsante sana.