Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

Hon. Innocent Lugha Bashungwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Karagwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia hoja ya Waziri wangu wa Kilimo. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyenijalia afya njema nikaweza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuchangia hoja hii. Pia nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu, Rais wa Watanzania, kwa kuniteua, kuniamini na namhakikishia kwamba nitaendelea kumsaidia kwa kushirikiana na Mheshimiwa Waziri wangu na Mheshimiwa Naibu Waziri mwenzangu katika kutimiza majukumu ambayo Mheshimiwa Waziri wetu Japhet Hasunga, anatuongoza katika kuyatimiza. Kwa hiyo, namshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu, namwombea kwa Mwenyezi Mungu amjalie afya njema ili azidi kusukuma gurudumu la Watanzania la maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nimshukuru sana Waziri wangu Mheshimiwa Japhet Hasunga kwa hotuba nzuri iliyosheheni mikakati ambayo tunakuahidi pamoja na Waheshimiwa Wabunge kwamba tutaisimamia katika kuhakikisha inatimiza yale malengo ambayo tumewaahidi. Vile vile nitumie nafasi hii tumshukuru sana Naibu Waziri mwenzangu, pacha wangu, Mheshimiwa Omary Mgumba, kwa ushirikiano anaonipa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimshukuru pia Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu pamoja na Watumishi wote wa Wizara kwa kazi nzuri wanayofanya katika kutimiza majukumu ya Wizara.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kuishukuru sana familia yangu, mke wangu Jennifa Bash, a.k.a mama Araska, pamoja na watoto wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nishukuru sana vilevile michango ya Kamati yetu ya Kilimo, Mifugo na Maji, tunashukuru sana kwa michango yenu mizuri, ushauri na kwa namna ambavyo wanaendelea kutoa ushirikiano kwa Wizara yetu na tunaahidi tutazidi kuwapa ushirikiano kwani Kamati ni extension ya Bunge na Kamati ndiyo think tank inayoshauri Wizara. Kwa hiyo, tunawashukuruni sana kwa michango na ushauri wenu.
(Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii pia kuwashukuru sana Kambi Rasmi ya Upinzani, tumesikia ushauri na maoni yao na naamini watatuunga mkono katika kupitisha hii hoja ili tuweze kwenda kufanyia kazi ule ushauri ambao wameipatia Serikali. Vile vile nitumie nafasi hii kuwashukuru sana Wabunge wote ambao wamechangia hoja yetu ya Wizara, Waheshimiwa Mawaziri, tunawashukuru sana kwa michango na ushauri wetu.

Mheshimiwa Spika, mwisho katika shukurani, nitumie nafasi hii kuwashukuru sana wananchi wa Karagwe kwa namna wanavyoendelea kuniamini na kunipa ushirikiano nami naendelea kuwaahidi kwamba sitawaangusha katika jukumu langu la kuwawakilisha hapa Bungeni.

Mheshimiwa Spika, baada ya shukrani hizo, sasa niende kuchangia kwenye maeneo ambayo yalikuwa cross cutting na nianze na suala la bei za mazao. Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia mazao mbalimbali lakini kwenye suala la bei kuwa chini. Nipende kuwakumbusha tu kwamba suala la bei tunaangalia matokeo, lakini pia lazima tuangalie mchakato unaotupeleka kwenye bei, ni mchakato gani ambao tunatakiwa kushirikiana kuufanyia kazi, ili bei za mazao ya wakulima wetu ziweze kupanda.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia suala la bei, ni suala la factors kadhaa, kuna suala la kodi na tozo, Serikali sikivu ya Awamu ya Tano, katika Bunge hili la Kumi na Moja tayari tumeshatoa tozo na kodi kero nyingi katika mazao. Kwa vile kodi na tozo siyo factor peke yake ambayo inasaidia bei kupanda, Serikali tunaendelea kufanya jitihada kuhakikisha, kupita ushirika, tunazingatia kanuni za ubora wa mazao, tunawapa elimu wakulima ili kupitia ushirika tuweze kusimamia suala la ubora kwa sababu bei, ukiondoa kodi kero na tozo, lakini suala la ubora ni suala muhimu sana katika kuhakikisha mazao yetu yanapata bei nzuri na namna pekee ya kusimamia suala la ubora ni kupitia ushirika.

Mheshimiwa Spika, kuna takwimu zinaonesha kwamba hata kwenye upande wa pamba, upande wa kahawa, upande wa chai, ushirika ume-prove kwamba ndiyo namna bora ambayo tunaweza tukasaidia kuwaelimisha wakulima wetu wazingatie ubora ili mazao haya tunapoyapeleka kwenye masoko, suala la ubora au quality liweze kuwa zuri na kuweza ku-attract bei ya mazao yetu. Kwa hiyo, ushirika katika models ambazo zipo za kusaidia wakulima wadogowadogo katika peasant setting, ushirika ndiyo ume-prove kuwa mfumo mzuri ambao tunaweza tukautumia kuwasaidia wakulima wakazingatia suala la ubora.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge concern yao kubwa ni kukosa uadilifu na utawala bora katika mfumo wa ushirika na sisi Wizara tuwahakikishie, hili ni jukumu ambalo wametupa, tutaendelea kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha tunapata viongozi wazuri katia AMCOS zetu, tunapata viongozi katika Unions zetu ili viongozi hawa tuweze kuwasimamia na kupita huu mfumo wa ushirika, tuweze kuzingatia ubora wa mazao ili mazao haya yanapokwenda sokoni yaweze kupata bei nzuri.

Mheshimiwa Spika, katika bei pia kuna suala la supply and demand, yaani unapopeleka zao sokoni, inategemeana na wingi wa mazao uliyokuta katika soko ukoje. Hilo suala liko nje ya mkakati kwa sababu ni exogenous factor lakini tunaendelea kujitahidi kupitia kuzingatia ubora na katika ushirika, tunataka kuhakikisha tunasheheni mambo mengi, si tu katika kuzingatia ubora, lakini ushirika utatusaidia kupata takwimu, kwa sababu wakulima wanakuwa organized katika mfumo AMCOS, ni rahisi sana kujua AMCOS x katika wilaya fulani ina wakulima wangapi. Kwa hiyo, kama ni suala la pembejeo, kama ni suala la mafunzo ya uzingatiaje wa kilimo bora, kupita ushirika, kwa sababu tunaweza tukapata takwimu kirahisi, itatusaidia sana kwenye mambo ya kutoa extension services kwa ajili ya wakulima wetu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hii ni sababu nyingine ambayo inaonyesha kwa nini ushirika ni mfumo mzuri, kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge, tuwaombe waendelee kutupa ushirikiano katika suala zima la kuboresha ushirika kwa sababu kuna faida nyingi ambazo tunaweza tukazipata katika kuhakikisha tunalinda na kuboresha maisha ya wakulima wetu.

Mheshimiwa Spika, pia katika ushirika, mikakati ambayo hotuba ya Mheshimiwa Waziri imesheheni likiwemo suala la bima za mazao, ni rahisi sana kutoa huduma hii katika mfumo wa ushirika ambao umekuwa organized vizuri. Pia hata suala la mambo ya kangomba, butula, baada ya kuwa na ushirika imara, ni rahisi ndani ya AMCOS au Union, kukawa kuna Mfuko au SACCOS, ambayo itasaidia kutoa advance kwa wakulima wetu wakati wa kulima ili mkulima huyu asiingie katika majaribu ya kukutana na mtu ambaye anataka amnyonye kwa sababu ya shida.

Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge, hata rafiki zangu akina Mwambe ambao wanasema tuhalalishe suala la mfumo wa kangomba, tunaweza tusihalalishe mfumo wa kangomba, lakini katika kuimarisha ushirika, tukaweka mfumo wa SACCOS ndani ya AMCOS, kutoa advance kwa wakulima ili waweze kuondokana na zile changamoto na shida ambazo zinawapeleka kwenye kangomba, butula, na mambo ya namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo ningependa kulichangia, limejitokeza sana katika michango ya Waheshimiwa Wabunge ni suala zima la uzalishaji na usambazaji wa mbegu. Hotuba ya Mheshimiwa Waziri kama mlivyoona, sisi Serikali tumejipanga kuhakikisha tunakuwa tuna mkakati ambao pia tunausimamia kuutekeleza na mkakati huu ni kuhakikisha, sasa hivi tatizo lililopo ni kwamba, mzalisha mbegu na mkulima wanategemea mvua wote kwa wakati mmoja. Mkakati wa Serikali, ni kwamba, huyu anayezalisha mbegu ASA, TARI, wakati wa kiangazi, tutatenga fedha kwa ajili ya kumwezesha TARI na ASA waweze kuzalisha mbegu wakati wa kiangazi ili mbegu hizi ziwepo, ziwe tayari wakati wa msimu mkulima anapozihitaji.

Mheshimiwa Spika, tukifanya hivyo, tutaondokana na hii changamoto ambayo Waheshimiwa Wabunge walio wengi wameichangia kwamba mbegu hazipatikani, zilizo bora, zinazostahimili ukame, zinazostahimili magonjwa, lakini tuna Taasisi ya ASA na TARI ambazo Serikali itatenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha wakati wa kiangazi wanatumia pivot irrigation badala ya kusubiri mvua ili mbegu ziwe tayari mkulima wetu mvua inapoanza basi aweze kupata hizi mbegu. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge waunge mkono hoja hii ya Mheshimiwa Waziri wetu kwa sababu mambo haya yote baada ya kupitisha tutakwenda kwenye utekelezaji wake.

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu ambalo napenda kulizungumzia ni suala la masoko kwa sababu ni mtambuka, linahusu mazao yote ya kimkakati na mazao mchanganyiko. Tayari, chini ya uongozi wa Waziri wetu Mheshimiwa Japhet Hasunga, tumeshakaa na wenzetu upande wa Wizara ya Viwanda, ku-link kilimo na viwanda. Tumekaa na breweries, kwa sababu breweries nyingi zinatumia ngano, zinatumia mahindi, zinatumia mtama na zinatumia zabibu. Tumekaa nao na hivi ninavyozungumza tunakaribia kusaini partnership ambayo mahitaji yao wameshayabainisha na tumewaomba wa-project kwa miaka mitano, kama ni zabibu watahitaji kiasi gani, kama ni mtama watahitaji kiasi gani, kama ni mahindi watahitaji kiasi gani ili tuweze kwenda kwa wakulima sasa katika wilaya na mikoa ambayo inalima haya mazao kwa wingi na kuhamasisha kwamba, limeni kwa sababu soko lipo na ni la kiasi hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, breweries tumeshakaa nazo, na tumeshakaa hata na viwanda ambavyo vinatengeneza soft drinks. Ukiangalia maembe, machungwa, wana import concentrate kutoka nchi za jirani na wakati wakulima wetu ukienda kule Tanga, wakati wa msimu machungwa yanaoza. Kwa hiyo, tumeshakaa na hizi soft drinks, viwanda vinavyotengeneza soda hizi na sasa hivi kwa sababu ya watu kuzingatia afya, viwanda hivi vinaanza kutengeneza juice sambamba na distribution ya soda. Sasa zile juices ambazo wanatengeneza zenye flavor ya pineapple, zenye flavor ya mango, zenye flavor ya orange, wanaagiza concentrate. Sasa sisi tunataka kwa sababu tumeshakaa nao, tujue mahitaji yao, twende tukahamasishe kilimo cha maembe, kilimo cha machungwa, kilimo cha nanasi ili badala ya ku-import concentrate, viwanda hivi viwe vinanunua malighafi hii ya wakulima hapa hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, lakini sambamba na hilo, tayari Wizara yetu tumeshakaa na hawa International off-takers, ninyi mashahidi, tulikaa na WFP, (Word Food Program), tumeingia nao mkataba wa muda mrefu kupita NFRA watakuwa wanakusanya mahindi na sasa hivi si mahindi tu, ukienda South Sudan wanahitaji mtama.

Kwa hiyo pia kupitia NFRA tutakuwa tunawahamasisha wakulima walime mtama halafu NFRA au aggregate, lakini WFP anakuwa anachukua hapa Tanzania kupita NFRA na wanunuzi binafsi, kupeleka kwenye nchi ambazo hazina ardhi yenye rutuba, hazina amani kama Tanzania. Kwa hiyo, sasa ni muda sahihi wa kuhakikisha wanaunga mkono bajeti ya Kilimo ili tuweze kuipeleka kwenye utekelezaji na kuchukulia hii geographical comparative advantage tuliyonayo katika nchi za Afrika Mashariki na SADC kwa sababu tunaweza tukazalisha kwa kiasi kikubwa na tukaweza kuondokana na hii changamoto ya wakulima wetu kulima, lakini masoko yakawa yanakosa.

Mheshimiwa Spika, tunawahakikishia Waheshimiwa Wabunge wakiunga mkono bajeti hii haya mambo yote tunayowaambia tutaweza kupeleka kwenye utekelezaji na matokeo makubwa watayaona kwa muda mfupi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala ambalo Mheshimiwa pacha wangu Mheshimiwa Omary Mgumba amelizungumzia, tukizungumzia mambo ya umwagiliaji mara nyingi tunafikiria ujenzi wa mabwawa makubwa, fedha nyingi, lakini niwaombe Waheshimiwa Wabunge, kama alivyosema Mheshimiwa Mgumba, kupitia halamshauri zetu…

SPIKA: Dakika moja umalizie.

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Spika, nashukuru. Suala la mabwawa kwa mfano kwenye mpunga, hauhitaji skimu kubwa, tunaweza tukaangalia jinsi ya ku-rain harvest, yaani kwa uchimbaji mdogo tu unakinga unapata maji kwa ajili ya kilimo cha mpunga na mazao ya bustani badala ya kusubiri kwamba mpaka mradi mkubwa uje uletwe na Tume wa Umwagiliaji kwenye wilaya husika, sasa sisi ndani ya Serikali tutakaa na halmashauri, Wakuu wa Mikoa, kuhakikisha suala la rain harvest linakuwa sambamba na uchimbaji wa mabwawa tunayozungumzia.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na naunga mkono hoja. (Makofi)