Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

Hon. Mbaraka Kitwana Dau

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa fursa hii. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Japhet Hasunga kwa wasilisho zuri asubuhi ya leo.

Mheshimiwa Spika, katika ukurasa wa saba wa kitabu cha Mheshimiwa Waziri, kinaelezea kuhusu Tume ya Maendeleo ya Ushirika. Wananchi wa Wilaya ya Mafia wameitikia wito wa kuanzisha Vyama vya Ushirika na Akiba na Mikopo lakini kwa masikitiko makubwa maombi ya Msajili wa SACCOS Haiba SACCOS yamepokelewa na Afisa Ushirika tokea tarehe 18 Machi, 2019 na hadi naandika hapa, Afisa Ushirika Mkoa wa Pwani hajatoa usajili kwa kisingizio cha kuwa anafanya uhakiki wa wanachama.

Mheshimiwa Spika, sheria inamtaka afisa kutoa usajili au kukataa ndani ya siku 60 na muda huo unamalizika kesho, Jumamosi, huku hakuna matumaini yoyote kwa SACCOS hii kusajiliwa. Naomba nichukue fursa hii kumwomba Mheshimiwa Waziri aingilie kati mchakato huu kurahisisha usajili.

Mheshimiwa Spika, ukurasa wa 11 wa kitabu cha Mheshimiwa Waziri unazungumzia upatikanaji wa mbegu bora za mazao. Nikiwa Mjumbe wa Kamati ya Bajeti tulibahatika kutembelea Kiwanda cha Kusindika Mafuta ya Alizeti cha Mount Meru kilichopo Mkoani Singida. Moja ya changamoto kubwa inayokikabili kiwanda hiki ni upatikanaji wa alizeti kutoka kwa wakulima. Uzalishaji wa alizeti hautoshelezi kulisha kiwanda hiki kutokana na wakulima kutumia mbegu duni za kizamani ambazo zinatoa alizeti kidogo kwa ekari moja.

Mheshimiwa Spika, nilete ombi kwa Serikali kuagiza mbegu bora za kisasa kutoka India zenye tija kubwa kwa ekari. Mbegu hizi bora zitasaidia kulisha viwanda vyetu vya ndani na kuondokana na tatizo la kuingiza mafuta ya kupikia kutoka nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Mafia inalima zao la nazi kwa wingi sana. Naomba kuishauri Serikali yangu kutuletea mtaalam wa kilimo na mbegu bora ili zao hili liweze kuwa na manufaa kwa wananchi wa Mafia na nchi nzima kwa ujumla. Nakushukuru na naunga mkono hoja.