Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

Hon. Desderius John Mipata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

MHE. DEUSDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kupata nafasi. Nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uzima, lakini pia niwapongeze Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa hotuba nzuri sana hii waliyotuletea, lakini pia kwa kazi nzuri wanayoifanya. Mchango wangu utakuwa katika maeneo mawili.

Mheshimiwa Spika, la kwanza, ni juu ya upatikanaji wa pembejeo na bei zake, sijaridhishwa sana na jinsi mbolea au pembejeo za kilimo zinavyopatikana kwa wakulima bado kuna changamoto nyingi. Mbolea hazipatikani kwa wakati, pembejeo za mbegu na madawa feki ni nyingi kupita kiasi na wakulima wanakula hasara sana na kwa sababu ni shughuli ambayo na sisi wenyewe tunafanya Wabunge nami ni mmojawapo, nashuhudia kwa ushahidi mimi mwenyewe wakati mwingine unanunua madawa yatafanya kazi na wakati mwingine hayafanyi kazi kabisa. Kwa hiyo bado kuna changamoto kubwa sana katika suala la utafiti na wataalam wetu waweze kufanya kazi vizuri zaidi.

Mheshimiwa Spika, katika maeneo hayo nataka niwe na mchango ufuatao, kwamba, vituo vya utafiti viimarishwe, tusitegemee sana vituo vya utafiti au mbegu na pembejeo za kutoka nje, hizi zinatusumbua na zinaleta hasara kubwa sana kwa wananchi wetu. Pale kwetu Rukwa pale kuna kituo cha Utafiti cha Mirundikwa kina changamoto nyingi sana, tuna ardhi ya kutosha lakini hawana wafanyakazi wa kutosha, hawana fedha, hawana matrekta, wakisaidiwa hawa watasaidia wakulima wa Mkoa wa Rukwa vizuri zaidi.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nafikiri ni muhimu sana katika hii ni pembejeo. Matrekta tumeambiwa yapo hapo Bagamoyo yapo matrekta mengi, lakini hii habari haijafika vizuri kwa wakulima wetu, hawajui, utaratibu uliowekwa na Serikali ni mzuri sana, lakini watu hawana information ya kutosha juu ya namna ya kupata hayo matrekta na kwa utaratibu uliowekwa na Serikali ni mzuri kabisa. Kwa hiyo, bado kuna habari ya hamasa ifike kwa wakulima. Kule kwetu kuna vikundi vingi sana hasa Mkoa wa Rukwa vikundi vingi sana vinajihusisha na kilimo, Nyanda za Juu Kusini kwa ujumla wake, lakini hawajapata habari kwamba kuna trekta zipo ambazo wakijiunga kwenye vikundi vikiandikishwa wanaweza wakapata na wakaboresha kilimo chao. Kwa hiyo niipongeze Serikali kwanza kwa uamuzi huo, lakini natoa wito kwa Serikali wataalam wetu watoe wito na elimu zaidi kwa wakulima namna ya upatikanaji wa hizo trekta ili waweze kunufaika na wazo hili zuri la Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni masoko ya mazao; Nyanda za Juu Kusini sisi ni maarufu wa kulima nafaka, lakini siku zote katika miaka miwili mitatu hii yamekuwa ni mateso. Watu wanalima na wanaendelea kukata tama, kwa sababu hatuoni soko la mazao, tunajua wazi kwamba Serikali si wajibu wake kutafuta kununua mazao ya kilimo kama wanavyotusaidia NFRI lakini ni wajibu wa wataalam wetu kuhakikisha kwamba mazao yanayolimwa na wakulima wetu yanapatiwa masoko nje na ndani ya nchi yake. Hakuna sababu kufunga mipaka, mwaka huu ni mbaya sana, nafaka inaweza kuwa kidogo, lakini wazo watakalokuwa wanalifikiri sasa hivi watu wa Serikali ni kufunga mipaka badala ya kuacha watu wanufaike na uzalishaji ambao sasa umetolewa kwa muda mrefu. Naomba kabisa kabisa mwaka huu msithubutu kufanya jambo hilo. Wawaachie watu wanaofanya kazi waweze kunufaika na mazao yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)