Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

Hon. Victor Kilasile Mwambalaswa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia kwenye hoja hii ambayo iko mbele yetu. Napenda kuwapongeza Mheshimiwa Waziri na Manaibu Waziri, Katibu Mkuu, Watendaji wote kwa kuitayarisha hoja hii vizuri sana.

Mheshimiwa Spika, nataka niongelee zao la tumbaku peke yake. Nchi ya Malawi ilikuja Tanzania kuja kuomba mbegu ya tumbaku mwaka 1966, ilichukua mbegu kwetu, sasa hivi Malawi wanazalisha tumbaku karibu kilo milioni 200; sisi ambao walichukua mbegu kwetu tumewahi kufika mwaka 2010, tulifika kilo milioni 120, sasa mwaka huu tunategemea kilo milioni 54 kutoka kwenye milioni 120 mpaka kilo 54. Kuna tatizo gani? Kwa nini uzalishaji unashuka namna hii wakati ardhi tunayo Watanzania? Watu ni walewale na watu tunaongezeka?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ningetegemea kwamba, uzalishaji ungekuwa unaongezeka, uzalishaji unashuka, ina maana kuna tatizo tena tatizo kubwa. Namuomba sana Mheshimiwa Waziri na timu yake, naomba tutumie Chuo Kikuu cha Sokoine, tutumie SUA; wenzetu Afrika hii, wenzetu duniani wanatambua umuhimu wa wataalam waliopo hapo Sokoine. Wanawaita, wanakwenda Ethiopia, wanakwenda Southern Africa huku kwenda kutoa taaluma yao. Naomba tutumie Chuo Kikuu cha Sokoine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano kuna miradi mingi ambayo huko Wizarani wamepata fedha kwa mfano Miradi ya Sumu Kuvu ambayo wameipata. Wawatumie wataalam wa Chuo Kikuu cha Sokoine ili tuweze kujua kwenye tumbaku kuna tatizo gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zao la tumbaku mwaka huu, Mheshimiwa Waziri anajua, kuna makampuni ambayo, tuna makampuni kama manne au matano ambayo yananunua tumbaku hapa nchini. Kampuni moja imeamua kujitoa, nadhani limetoa nia ya kujitoa, kwa hiyo, hawajatoa makisio mpaka sasa. Kwa hiyo, kuna Vyama vingi vya Msingi Wilayani Chunya, Tabora, Mpanda, Songea ambavyo havina kwa kuuza tumbaku ya mwaka kesho. Mheshimiwa Waziri anajua, naomba isije ikawa korosho ya pili, naomba Mheshimiwa Waziri achukue hatua stahiki tupate kampuni nyingine za kuja kununua tumbaku kwa wakulima ili tuweze kuinua kipato cha wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja. (Makofi)