Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

Hon. Pascal Yohana Haonga

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Mbozi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia nitagusa baadhi ya maeneo kwa mfano nitagusa eneo la kwanza linalohusu zao la Kahawa, pia eneo la pili nitagusa Korosho na kama muda utaruhusu pia nitazungumzia suala la Maafisa Ugani.

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie kwanza suala la zao la Kahawa, ni kwa muda mrefu sasa bei ya kahawa imekuwa ikishuka miaka hadi miaka na msimu huu kahawa ndio imeendelea kushuka imekuwa bei ndogo kuliko wakati mwingine wowote ule.

Mheshimiwa Spika, jambo ambalo naomba nijiulize kidogo na naomba labda tusaidiane kidogo Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha atusaidie, kwa nini nchi ambazo zinatuzunguka wanaolima kahawa sawa na sisi kwa mfano nchi kama Uganda pamoja na nchi nyingine ambazo zinalima kahawa Kenya na nyingine kwa nini hawalalamiki sana kuhusu suala la bei ndogo ya kahawa? Na ushahidi unaonyesha kwamba hata kahawa ya Tanzania inatoroshwa kupeleka Uganda kwa maana ya Kahawa ya Kagera inapelekwa Uganda, lakini pia kahawa kutoka Kigoma inatoroshwa na maeneo mengine ya mpakani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni kwamba hawa wenzetu kwa sababu tunaamini kahawa inauzwa tuna soko la dunia je wao soko lao liko wapi? Kwa nini kahawa yetu sisi imeendelea kushuka wakati soko la dunia ni moja? Kwa kweli nadhani shida kubwa hapa nayoiona shida kubwa sio soko la dunia hiyo sio shida kubwa, shida kubwa ni utashi wa viongozi wa Serikali hii ya Awamu ya Tano ambao wamepewa dhamana kutuongoza ndio tatizo linaanzia hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo kwa mfano ukiangalia kuna suala la Uganda pale wao hawana kitu kinaitwa vyama vya msingi vya ushirika hawana lakini bei ya kahawa ni nzuri, hawana kitu kinachoitwa hizi tozo karibu zote zimeshaondolewa imebaki tozo moja tu yule anayekuja kununua kahawa analipa ile tozo ya mwisho anapokuwa anasafirisha kahawa anapoondoka, sasa sisi bado kwenye kahawa kuna tozo nyingi sana hili ni tatizo kubwa sana, sasa huyu mkulima wa kahawa kama angeweza kuachwa kwa mfano tukamfutia tozo zote alipe kodi anaponunua saruji kwa sababu ataenda kujenga, alipe kodi anapoenda kununua bati kwa sababu ataenda kujenga, huko ndiko ambako sasa tungeweza kupata kodi kwa njia kama hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nashauri Wizara iangalie namna ya kuondoa tozo na kodi zote kwenye zao la kahawa kama wanavyofanya nchi ya jirani ya Uganda ili mwisho wa siku nchi yetu tuweze kuwasaidia wakulima wa kahawa. Hata eneo tunalolima kahawa ni eneo kubwa sana lakini tija ni kidogo, leo tunaambiwa kwenye takwimu hapa kwamba msimu tulipata zaidi ya tani 60,000 na miaka ya nyuma ilikuwa tani 40 na kidogo 40,000 nakadhalika.

Mheshimiwa Spika, lakini ukiangalia Uganda wanalima zaidi ya tani wananapata zaidi ya tani 300,000 wanapolima mara moja zaidi ya 300,000 tunaingia mara sita kwa Uganda, kwa hiyo tija kwenye zao la kahawa pia hapa kuna shida, tuna mashamba makubwa lakini tija ni ndogo. Kwa hiyo, ni vizuri tukatafuta muarobaini kwa nini wenzetu ambao wanalima kahawa wana mashamba madogo kuliko ya kwetu lakini wanapata kahawa nyingi kuliko sisi shida iko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaomba nizungume jambo la pili ambalo ni jambo la kuhusu suala la korosho. Aliyevuruga suala la korosho au biashara ya korosho huyu tumchukulie kama alivyokuwa wahujumu uchumi wengine, kwa sababu leo ukiangalia zao la korosho kwa takwimu ambazo tunazo mwaka jana korosho fedha za kigeni tuliingiza dola za Marekani milioni 367 ukichukua zao lililofuatia lilikuwa ni Tumbaku ambalo lilikuwa ni dola za Marekani milioni 222, na kahawa ilikuwa dola za Marekani milioni 134, lakini ukichukua mazao yote kama Karafuu, Katani, Chai, Pamba unaona mazao yote haya ukijumlisha bado hayawezi kufikia kwenye zao la korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa leo tunaweka watu kwenye magereza zetu tumewajaza watu ambao wanasema ni wahujumu uchumi kwa vitu vidogo lakini kuna watu waliochezea zao la korosho tunacheka nao, tunakula nao, tunakunywa nao, tunawaangalia. Leo tulitegemea kwamba watu hawa wangekuwa magereza lakini tunacheka nao tunawaangalia tu. Sio mtabiri wala sio Nabii kama Mbunge wa Arusha Mjini Mheshimiwa Lema lakini Rais ajaye sijui atakuwa nani aidha upande wa CCM au CHADEMA au CUF ninaamini atakuja kufanya jambo kwa sababu naamini kwa upande huu kipindi hiki ni kwamba ni nani amfunge paka kengele inawezekana ndio shida inaanzia hapo. Lakini kwa hawa wanaotuingizia hasara Taifa letu kwa kweli lazima wachukuliwe hatua kama wahujumu uchumi wengine ambavyo wamekuwa wakifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo zao hili tumepoteza export levy mwaka jana ilikuwa zaidi ya bilioni 300 export levy leo hatujapata hata shilingi hatujapata kwenye export levy kwa sababu ya watu wachache tu walioamua kutufanyia mambo ambayo kwa kweli sio mazuri hata kidogo. Leo halmashauri zinazolima korosho Tandahimba maeneo yote yanayolima korosho hawajapata ushuru unaotokana na zao la korosho. Leo halmashauri hizi zinaendaje kuendesha mambo yao? Kwa sababu kuna watumishi ambao wanaajiriwa na halmashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo tunaambiwa kwamba hawatapewa fedha kwa maana ya ushuru wa korosho maana yake hawa watu wameporwa ushuru wa mabango, wameporwa ushuru wa majengo, leo unaenda kuwapora na ushuru wa korosho tafsiri yake ni kwamba hizi halmashauri zinaenda kufa, sasa kama zinaenda kufa mwisho wa siku itakuwa sasa mwisho wataenda kuzifuta tu kwa sababu sasa hivi shida kuendesha mambo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo bado nisisitize kuna hana najua Mheshimiwa Waziri wewe ni mgeni lakini kuna haja ya waliohusika wote waweze kufunguliwa kesi za uhujumu uchumi ili mwisho wa siku tuweze kupeana adabu na mwisho wa siku mambo yaweze kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho ambalo noamba nizungumzie kidogo ni suala la kuhusu Maafisa Ugani, kwa takwimu tulizo nazo Tanzania tuna vijiji zaidi ya 15,000 vijiji tulivyokuwa navyo lakini Maafisa Ugani ambao tunao ni 7,974. Juzi hapa uliongea kwamba unapozungumzia kwa mfano suala la uchumi wa viwanda huwezi ukaiacha kwa mfano Bandari ile ya Bagamoyo ukaiacha ni sawa na ng’ombe anakuwa nyuma halafu mkokoteni unakuwa mbele, wakati ng’ombe anatakiwa akae mbele avute mkokoteni. (Makofi)

Sasa leo kama inafika mahali Maafisa Ugani wako wachache namna hii ambao ni 7,964 tu, lakini na vijiji zaidi ya elfu 15 ni sawasawa na mfano uliotoa ule kwamba, unapeleka mkokoteni mbele halafu ng’ombe wanaovuta wanakaa nyuma. Sasa jambo hili Mheshimiwa Waziri atueleze wakati atakapokuwa anahitimisha, je, wana mpango gani kuhusu kuajiri Maafisa Ugani? Kwa sababu, hatuwezi Maafisa Ugani ni wachache. Hata hawa waliopo utakuta yuko mmoja, huyohuyo wanampa kazi ya utendaji, mara watampa sijui kazi ya nini; hawa ni wacache, lakini wanapewa na majukumu mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, hawa Maafisa Ugani waliopo tunaomba waweze kuajiriwa na wengine ili wawe wengi zaidi, lakini pia waweze kupewa motisha. Leo maeneo mengine ya nchi ambazo zimeendelea huko ambazo ziko serious kwenye masuala ya kilimo Maafisa Ugani hawa amepewa angalau mtu anapewa, hata kama hawezi kupewa gari, basi mpe hata pikipiki ili aweze kufanya kazi kwenye mazingira mazuri. Maana kilimo chetu sasa tunakitegemea kwamba, inapofika mwaka 2025 twende kwenye uchumi wa kati, hatuwezi kuwa na uchumi wa kati ikiwa Maafisa Ugani ni wachache namna hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine kwenye kilimo ambalo naomba nigusie, ni kilimo cha umwagiliaji. Mwaka jana, bajeti ambayo tunaenda kuimalizia sasa kwenye suala la umwagiliaji, tulitenga kama bilioni 24 hivi, lakini mwaka huu tumetenga bilioni nane tu; tunawezaje kuwa na nchi ya viwanda kama tumetenga bilioni nane kwenye umwagiliaji? (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumza)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Haonga.

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kuunga mkono hoja ya Upinzani.