Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo Zilizowasilishwa katika Mkutano wa Kumi na Nne na Mkutano wa Kumi na Tano wa Bunge

Hon. Goodluck Asaph Mlinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ulanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo Zilizowasilishwa katika Mkutano wa Kumi na Nne na Mkutano wa Kumi na Tano wa Bunge

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nataka niunganishe kwa kaka yangu, Mheshimiwa Kubenea aliyepita kuchangia sasa hivi kuwa sheria siyo msahafu kwa hiyo muda wowote tukiona haifai tunapiga chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kwa namna ya pekee naomba nitoe nitoe pongezi zangu kwa Mheshimiwa Spika kwa kuunda Kamati hii ya Sheria Ndogo…

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

T A A R I F A

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. naendelea; pongezi zangu kwa Mheshimiwa Spika, kwa sababu kwa kipindi kifupi cha miaka minne nilichokaa kwenye Kamati hii nimeona umuhimu wake jinsi gani ulivyokuwa mkubwa. Sheria ni nyingi mno na zinaumiza wananchi, na ndiyo maana mmeona hata wengine afya zetu zimekuwa ni ngumu kukua kutokana na kazi kubwa ambayo ipo kwenye Kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nianze na Ofisi ya Mpigachapa wa Serikali. Sheria nyingi zimekuwa zikitungwa lakini inatumia muda mrefu sana kufika mpaka zitoke kwa sababu katika Ofisi ya Mpigachapa wa Serikali wanatumia vifaa vya zamani na ni chakavu na watumishi ni wachache. Kwa hiyo, ninaiomba Serikali iweze kuiwezesha Ofisi ya Mpigachapa ili sheria zinazotungwa ziwe zinaweza kutoka kwa wakati kwa sababu kuna sheria zinaweza zikatoka tayari zimeshapitwa na wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nataka nizungumzie, kwa uzoefu niliopata sheria nyingi hazishirikishi wadau vya kutosha. Utakuta taasisi ama halmashauri wanaita wadau wanasikiliza lakini hawazingatii vya kutosha yale maoni. Yaani kana kwamba wanakuwa tayari sheria walishatunga wameshaweka kwenye vichwa vyao kwa hiyo wadau wanakwenda kuwasikiliza kama kukamilisha ratiba. Kwa hiyo, unakuta sheria zinatungwa lakini haziendani na mazingira yaliyopo. Wote mtakuwa mashahidi kanuni za kikokotozi zilivyopita na zikaleta taharuki katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimebaini watendaji wengi wanafanya kazi kwa mazoea, hasa hawa watunzi wa sheria.

Kwa hiyo, wamekuwa wakifanya ilimradi wanafanya, matokeo yake makosa yamekuwa mengi mno katika hizi sheria. Kwa hiyo, Kamati sasa ya Sheria Ndogo imekuwa inafanya kazi ya kutunga sheria, siyo kuzirekebisha, maana yake mnapita neno kwa neno. Kwa hiyo, makosa yamekuwa mengi, makosa mengine ya kiuandishi, mpaka unajiuliza huyu mtunzi wa sheria anajua anakwenda kutumia hii sheria?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria nyingine zimekuwa hazizingatii uhalisia. Kuna sheria moja ya BASATA niliiona inasema katika kila kumbi ya sherehe iliyopo manispaa, tozo ya BASATA ni shilingi 500,000. Sasa unamuuliza aliyepitisha hii sheria anazijua manispaa zetu za Tanzania? Nitolee mfano Singida, Singida hauwezi kwenda ukakuta ukumbi ambao unazidi 500,000, sasa tozo ya BASATA peke yake ni shilingi 500,000, je, unauliza, ukumbi huu sherehe itatozwa kiasi gani. Au sheria nyingine za BASATA zinasema eti kuwa ukitaka kujenga ukumbi wa sherehe popote pale lazima michoro iende ikapitishwe na BASATA wakati wengi wanaotengeneza hizi kumbi za starehe za kufanyia sherehe tunajua wanajenga kwa bahati mbaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria nyingine ambayo niliiona ya hovyo ni sheria ambayo inasema kila msanii ambaye atakwenda kufanya tangazo anatakiwa tozo ya BASATA alipe shilingi milioni mbili. Sasa unauliza; anajua mazingira ya wasanii wetu wa Tanzania? Wengine wanakwenda kufanya matangazo kwa ajili ya kuuza sura, wengine wanakwenda kufanya matangazo kwa ajili ya kupata uzoefu, wengine wanafanya bure ili waonekane; kwa hiyo, sheria nyingi hazizingatii uhalisia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nije kwenye halmashauri…

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

T A A R I F A

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naipokea taarifa yake, lakini bado uhalisia uko palepale. Kwa mfano mimi Mlinga nina kibanda changu pale cha chipsi nataka msanii aje aonekane anakula ili wateja waje, mtaji hauzidi laki tano halafu wanataka nimlipe huyo msanii milioni mbili kwa hilo tangazo, kwa hiyo bado hazizingatii uhalisia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye halmashauri. Sheria nyingi ambazo zinaletwa kwenye Kamati yetu na zinazotungwa katika nchi yetu zinazotoka halmashauri – na hii ni kwa wingi wake – lakini hata hivyo, siyo sababu tosha ya kufanya sheria hizi ziwe na makosa. Tumegundua sheria nyingi za halmashauri ni copy and paste. Yaani mtu anachukua sheria ya Igunga anaenda kui-apply Ulanga, anachukua sheria ya Mpwapwa ambalo ni Jangwa anakwenda kui-apply Gairo au Kilosa. Kwa hiyo, sheria nyingi haziendani na yale mazingira, yaani ni copy and paste. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii napenda kupeleka lawama nyingi katika Kitengo ha Sheria cha TAMISEMI. Wamekuwa hawako makini katika kazi zao, na hata uandishi wa hizi sheria unaweza ukakuta kwenye ganda la sheria wanasema sheria inayohusu Igunga lakini ukienda ndani utakuta ni wilaya nyingine. Kwa hiyo, hata kusoma hawazisomi, siyo kupitia tu kuangalia je, sheria hizi zitaumiza wananchi au hazitaumiza wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba kutoa angalizo; TAMISEMI wangetoa mwongozo kwa hizi halmashauri zote kwa sababu Madiwani wengi kutokana na asili yao ya maeneo wanayotoka wengi hawana uelewa na elimu ya kutosha. Kwa hiyo, wametunga sheria ambazo nyingi zinaumiza wananchi, hiyo inawawezesha hawa Madiwani wajue nini wanakifanya na madhara ya hivi vitu ambavyo wanavipitisha kwa sababu wakishavipitisha kuvirekebisha inachukua muda sana.

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Mlinga.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na nitoe angalizo kwa Mawaziri; msiwe mnasaini sheria hizi bila kuzipitia. Wengi mmekuwa…

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: …mkifanya makosa ambayo yanafanywa na watendaji wetu. Ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)