Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Kuridhia Mapendekezo ya Ubadilishaji Hadhi Sehemu ya eneo la Pori la Akiba la Selous kuwa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere

Hon. Hawa Abdulrahiman Ghasia

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mtwara Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Azimio la Kuridhia Mapendekezo ya Ubadilishaji Hadhi Sehemu ya eneo la Pori la Akiba la Selous kuwa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika azimio hili la kupandisha hadhi Pori la Selous kuwa Hifadhi ya Taifa. Niipongeze Serikali, nimpongeze Mheshimiwa Rais na nimpongeze Waziri pamoja na Kamati ya Maliasili kwa kuridhia pori hili kuwa hifadhi.

Mheshimiwa Spika, ni muda mrefu sana ambapo hili ombi lilikuwa linaenda linarudi, linaenda linarudi kwamba, Selous iwe hifadhi na sio Pori la Akiba. Kwa kuifanya kuwa hifadhi tutakuwa tunaiihifadhi zaidi Selous kuliko ambavyo sasa hivi liko pori ambalo uwindaji wa kitalii ndani yake mle unaruhusiwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nipingane na Mheshimiwa Msigwa ambaye anasema hatujatoa taarifa UNESCO kwa sababu eti kuhifadhi tunahitaji ushirikiano wa kimataifa. Ndio tunahitaji ushirikiano wa kimataifa, lakini tunachokifanya sisi ni kupandisha hadhi, ina maana tunaendeleza uhifadhi zaidi, daraja kama ni uhifadhi tunaenda daraja la juu zaidi kuliko tulipo, tunachokifanya ndicho UNESCO inachokitaka. Tungeomba kibali cha UNESCO kama tungekuwa tunashusha hadhi kutoka kwenye pori na kuwa eneo la kawaida tu ambalo mtu yeyote anaweza akafanya kitu chochote.

Mheshimiwa Spika, niendelee kuunga mkono hili wazo na niiombe Wizara ya Maliasili na Utalii suala hili la kupandisha hadhi Pori la Selous kuwa hifadhi liende sambamba na kutangaza vivutio vingine vilivyopo Kusini mwa Tanzania ikiwemo beach nzuri za Msimbati ambazo unaweza ukaenda na gari lako na ukaendesha kama ambavyo unaweza ukaendesha kwenye barabara yoyote ya lami kwa speed yoyote unayoitaka.

Mheshimiwa Spika, pwani hizi ziko chache sana duniani na kwa Afrika nadhani ni moja tu ambayo inapatikana Msimbati na pia tunayo hifadhi yetu kule ya Ruvula ambayo inazo bustani nzuri sana chini ya ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa vile umenipa dakika tano, naunga mkono Azimio la Kupandisha Hadhi Selous kuwa Hifadhi na pia tuiombe Serikali basi itangaze ukanda wote wa Kusini, ili watalii wakija Selous wawe na maeneo mengi zaidi, awe akifika Kusini awe amejitosheleza kwa kila kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)