Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Kufuta Hasara itokanayo na Maduhuli ya Madeni ya Nyuma ya Ada na Leseni za Magari, Riba na Adhabu kwa kipindi kinachoishia tarehe 30 Juni, 2019

Hon. Godbless Jonathan Lema

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Arusha Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Azimio la Kufuta Hasara itokanayo na Maduhuli ya Madeni ya Nyuma ya Ada na Leseni za Magari, Riba na Adhabu kwa kipindi kinachoishia tarehe 30 Juni, 2019

MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwa kuanza nianze na alipomalizia Mheshimiwa Mbunge tumweleze kwa nini Kambi Rasmi ya Upinzani tuna mashaka. Mimi ni Mbunge awamu ya pili ndani ya Bunge hili na miaka yote yalipokuja masuala yanayohusu pesa nyingi kama hizi tulitilia mashaka suala la Meremeta, Kagoda, Escrow na IPTL. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni Wabunge wa upande huo huo walisimama wakasema IPTL ile pesa ilikuwa ni pesa ya watu binafsi na Mheshimiwa Rais akaongea na Wazee wa Dar es Salaam akawathibitishia kwamba wakati huo Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete kwamba ile pesa ilikuwa ni pesa ya watu binafsi haihusiani na Serikali. Leo tunavyoongea Wakurugenzi wa IPTL wako Magereza kwa zaidi ya miaka miwili kwa pesa ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani ilitilia mashaka na mashaka hayo yakapuuzwa ndani ya Bunge na leo kuna watu wanaitwa wezi, wamepewa kesi ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha na wanaendelea kuteseka Magereza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, uzuri jana Mheshimiwa Rais amesema walaaniwe wale wanaowaweka wenzao Magereza muda mrefu. Nami naunga mkono Azimio la Mheshimiwa Rais, kwamba walaaniwe wanaosababisha watu kukaa Magereza muda mrefu, hata kama Mheshimiwa Mbowe alaaniwe na hata kama ni Rais mwenyewe ama ni DPP ama ni wewe Mheshimiwa Spika ama ni mimi tulaaniwe wote tunaosababisha watu kukaa Magereza muda mrefu kwa kesi za kubambikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, najenga kwanza hoja kwa nini mashaka yetu ni ya msingi kwenye pesa kama hizi. Hii Sheria tulipitisha mwaka 2016/2017 ilikuwa ni Sheria ya kuondoa Motor vehicle license kutoka kwenye kulipia dirishani kwenda kwenye mafuta. Sasa wasiwasi wetu nasema uchaguzi ni kesho kutwa na tunaona mnavyolilia hela kwa Mabeberu, sasa tunasema pengine hizi pesa wanataka kwa ajili ya uchaguzi ziwasaidie, pengine hizi pesa kwa sababu Stigler‟s Gorge imewekewa mguu sasa pengine wanataka pesa kwa ajili ya kusaidia mambo yao…

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. GODBLESS J. LEMA: Mmeanza?.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Lema kuna taarifa, Mheshimiwa Goodluck Mlinga.

T A A R I F A

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe taarifa mzungumzaji anayezungumza kweli tunakubali Mheshimiwa Lema ni Mbunge wa awamu ya pili, lakini katika rekodi zangu hapa zinaonesha muda mwingi alikuwa akitumikia adhabu za Bunge na muda mwingine alikuwa jela kwa hiyo hana uzoefu wa kukaa ndani ya Bunge muda mrefu. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Lema…

MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Naibu Spika, napokea taarifa na wale wale wanaosababisha wenzao wafukuzwe Bungeni kwa kuonewa twende kwenye Azimio la Rais na wenyewe walaaniwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wale wote ambao wanasababisha wenzao wateseke, waondoke ndani ya Bunge lile lile, yaani mtu yeyote anayeonea alaaniwe. Kwa hiyo napokea taarifa yake na tukubaliane kwamba na wenyewe wale kama walihusika kwenye Kamati kama ni Kiti kumwonea mtu walaaniwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nasema hivi haya …

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Lema kwa sababu wewe huwa unasoma sana Biblia, hiyo laana lazima uiweke mazingira ambayo hata wewe mwenyewe unayesababisha watu wengine wafanye maamuzi na wewe ikupate, kwa hiyo usiwe mtaalam wa kugawa laana halafu wewe mwenyewe hutaki ikupate. Kwa hiyo na wewe mwenyewe pia ikupate kwa yale ambayo unasababisha watu wafanye maamuzi ya kukuweka ndani maamuzi ya kukutoa nje, yote hayo pande zote mbili inakuwa inapendeza zaidi. (Makofi)

MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi kama ni sababu ya watu kupata tabu nilaaniwe na wewe kama ni sababu ya kufukuzwa watu Bungeni, ulaaniwe, haina shida. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ninachosema tunajenga haya mashaka na Waheshimiwa Wabunge watuelewe, haya mashaka tunayajenga kwa sababu moja tu ya kwamba hili Azimio linakuja wakati Assad kaondolewa Ofisini na sisi tuna mashaka makubwa sana na Bunge hili lilikuwa na imani Profesa Assad. Sasa tunasema hizi pesa ni nyingi sana isije ikawa baada ya Bunge hili ama Awamu ya Utawala wenu akatokea Rais mwingine akaandika kitabu kama alivyoandika Mheshimiwa Mkapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mkapa ameandika kitabu amefanya confession, lakini Taifa limeumia Taifa limepata hasara, sasa wasiwasi wangu nina …

MHE. PETER J. SERUKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa …

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Lema kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Peter Serukamba.

T A A R I F A

MHE. PETER J. SERUKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kumpa taarifa Mheshimiwa Godbless Lema, taarifa hii ambayo tunaiongelea ambayo ni Ripoti ya CAG aliyeisaini ni Profesa Assad. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Lema kabla sijakuuliza kama unaipokea taarifa hiyo umemtaja hapa Mheshimiwa Rais Mstaafu Mkapa kwamba kwenye kitabu chake kuna jambo amelisema ambalo unaona nchi imeteseka sasa ili uweke kumbukumbu vizuri za Bunge, uwe umelisema na lenyewe maana hicho kitabu hata sisi wengine pia tumesoma ili kumbukumbu zikae sawasawa, maana zisije zikakaa kwamba Mheshimiwa Rais aliyepita alisema jambo lililoumiza nchi watu wanaumia halafu likaachwa hivyo hewani. Kwa hiyo kwanza unaipokea taarifa hiyo ya Mheshimiwa Peter Serukamba?

MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea.

NAIBU SPIKA: Haya.

MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Naibu Spika…

NAIBU SPIKA: Hilo la pili sasa refusha pale kwenye ule mjadala wako.

MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mkapa ameongea kuhusu Mauaji ya Zanzibar ambapo leo kuna wajane, watoto na ame-confess mwenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ndiyo, ndiyo kwenye kitabu chake.

NAIBU SPIKA: Aahha. Mheshimiwa Lema kuna mambo mawili umeyazungumza. Hoja ya ku-confess maana yake ameandika na kama kitu kinachoaitwa confession ndio maana huwa tunapenda maneno yatumike ya lugha moja, kinachoitwa confession ni kitu ambacho unakubali kwamba kuna jambo fulani hivi ulishafanya. Confession ni lugha ya Kisheria sasa wewe ukisema ame-confess ni kana kwamba wewe unavyoyaeleza hayo mauaji ame-confess nini kwa sababu mimi mwenyewe kitabu nimesoma? Sasa ili tutunze muda wetu vizuri aidha, uyaondoe hayo uendelee na jambo lingine au kama unataka kuyaweka eleza ame-confess nini kwa sababu kitabu na mimi nimekisoma na ameelezea mauaji ya Zanzibar kwa kawaida tu kama alivyoeleza sehemu nyingine. Ameeleza kwamba yalitokea, kwa hiyo akisema yalitokea ni kwamba ni kweli watu walikufa, hakuna mtu anayekataa kwamba kuna watu hawakufa.

MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Naibu Spika, kile kitabu cha Mheshimiwa Rais Mkapa siyo fiction, ni kitabu ambacho ameelezea maisha yake ya Uongozi na Utawala wake na akasema vitu ambavyo anavikumbuka ambavyo vimetia doa maisha yake ya utawala ni pamoja na hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hata hili la Mkapa ambalo ameandika mwenyewe mnataka kuli-defend? (Kicheko)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Lema…

MHE. GODBLESS J. LEMA: Ndio …

NAIBU SPIKA: Lazima uwe tayari kuelewa unachoelekezwa, usitake kupindua unachoelekezwa, hapana. Nimekueleza hivi ukitumia neno confession ni kwamba anakubali jambo Fulani, sasa alichokifanya ameeleza uhalisia kwamba kifo kilitokea na yeye hafurahii, sasa unavyosema ame-confess, ame-confess nini? Kwamba yeye ndiye aliyeua ama alituma mtu kuua. Kwa hiyo uwe unaeleza vizuri jambo namna alivyosema Mheshimiwa Rais kwenye kitabu chake, usiongezee wewe ya kwako kwa sababu kile ni kitabu chake yeye.

MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimekuelewa, naomba niazime maneno yako halafu ndiyo yaingie kuwa mchango wangu kwamba Mheshimiwa Mkapa amesema kama ulivyosema, halafu tuendelee. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni hayo hayo tu, nimeazima lugha yako kwa sababu imekaa kistaarabu, nafikiri unataka niwepo kwenye hili Bunge mpaka mwisho, kwa hiyo nimeazima lugha yako nisiingie hatiani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mashaka yetu kuhusu hizi pesa najiuliza tu Mheshimiwa Waziri Mpango toka mwaka 2016…..

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

WABUNGE FULANI: Hapana jamani. Eeh.

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

WABUNGE FULANI: Hapana.

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa, huku kushoto kwako.

WABUNGE FULANI: Hapana.

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, Dkt. Mollel huku.

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge leo tuna mambo mengi kidogo hii itakuwa ni taarifa ya mwisho.

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, namwelewa Mheshimiwa Lema anapokuwa na wasiwasi na vilevile yeye kama Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA alaaniwe, kwa sababu wakati nina bajeti hapa ya kama trilioni tatu ambayo baada ya ile taarifa yao waliyotoa CHADEMA au Mheshimiwa Mbowe pale Dar es Salaam, walijipanga kwenda kutafuta nje trilioni tatu kuja kufadhili mkakati wao ambao ni mchafu kwenye nchi yetu na ninyi mlaaniwe ambao mnatengeneza mazingira ya fujo kwenye Taifa hili kwa kutumia hela za Mabeberu halafu mnakuja…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa…

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, halafu mnakuja kusema mwisho wa siku mnataka laana halafu…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Lema malizia mchango wako …

MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niwashukuru Chama cha Mapinduzi kutuchukulia Mheshimiwa Dkt. Mollel, Mungu awabariki sana. Hebu imagine huyu alikuwa kwetu, halafu ukatokea muujuza yuko kwenu kwa hiyo, niwashukuru sana kwa kweli Mungu awabariki sana na kama kuna wengine mmewaona huku wako kama hivyo tafadhali fanyeni kazi kwa bidii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hebu imagine alikuwa ni Mbunge wetu wa Siha. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Endelea …

MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Naibu Spika, halafu ninyi mkatumia mikakati yote akawa wa kwenu, mimi nikushukuru, nishukuru Chama cha Mapinduzi, nimshukuru Katibu Mkuu, nimshukuru na Mwenyekiti wa Chama Taifa na kama mkiwaona wengine kama hawa kwa kweli tusaidieni ili tuweze kujenga chama kizuri. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachosema ni nini? Namheshimu sana mimi binafsi Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mpango, ninachosema kwamba 2016/2017, ndiyo tulipitisha hii Sheria sasa 2016, 2017, 2018, 2019 na 2020 miaka minne baadaye ndiyo mnaleta Azimio la kufuta deni la almost half a trillion? Sasa tunasema hapa kuna dili na tukasema hii tabia mmeanza lini?

Mheshimiwa Naibu Spika, ninyi huwa mnapeleka, mlianza kujenga Chato bila Azimio mlihamishia Dodoma hapa bila Azimio, mkaenda huko Stigler‟s Gorge bila Azimio, mkaenda kwenye ndege bila Azimio, sasa hii tabia nzuri mmeanza lini?(Makofi/Kicheko)

NAIBU SPIKA: Muda wako umeisha, Mheshimiwa kengele imeshagonga, ahsante sana.