Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii

Hon. Riziki Saidi Lulida

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru na nimshukuru Mwenyezi Mungu anayenijalia afya njema na mimi kuwepo hapa na kuchangia hoja iliyokuwepo mezani. Kwanza napenda nitoe pole kwa wananchi wa Mkoa wa Lindi ambao wamekutana na mafuriko makubwa ambayo hayajawahi kutokea katika kipindi cha zaidi ya miaka 50. Mafuriko haya yalitokea mwaka 1952; lakini mwaka huu wananchi wa Lindi wamekutana na mafuriko.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nilikwenda kuona eneo la tukio; lakini kuna watu ambao hawajaona hayo matukio. Lazima Mwenyezi Mungu tuwaombee wale wenzetu ambao wako katika mazingira magumu. Kitu ambacho hujakiona ni sawasawa na usingizi wa giza au usiku wa giza. Wenzetu wako katika mazingira magumu ambayo ukienda lazima utalia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kilwa peke yake ni zaidi ya watu 15,000, Lindi takriban watu 8000 wako nje hawana mahali pa kulala, hawana kitanda, hawana godoro, hawana maji, hawana nguo, hawana chandarua. Sisi Wabunge Mungu ametupenda tumekaa humu ndani, tuko vyumbani tumelala, tumepumzika, tunashiba ndiyo maana kuna wengine wanabeza wakati mwenzangu kaka yangu Mheshimiwa Bungara anazungumza watu walibeza, msibeze, na ukibeza Mungu hataleta furaha katika nafsi yako.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna methali inasema kitu kimoja ukimkuta mtu masikini akikuomba pesa kama hauna pesa nyamaza, lakini kama unayo mpe kwa kuwa yeye naye anahangaika anataka kunusuru maisha ili apate rizki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimetoka hapa kwenda Lindi na Nanjime nimekwenda Nanjilinji nimeshindwa kufika. Ina maana leo hivi kwenda Liwale huwezi watu wako katika kisiwa, kwenda Luwangwa watu wako katika kisiwa, kwenda Kilwa ndani vijijini watu wako katika visiwa, watu wanaokolewa na helkopta. Nimesikitika kuna mtoto anaitwa Derick Masanja huyo mtoto ana miezi 11; maana haya mafuriko hayakutokea wakati wa mvua yametokea wakati jua linawaka; maporomoko yametoka huko yamewakuta watu wakiwa mashambani, wakiwa na mifugo. Leo ninavyozungumza jamaa zangu Wasukuma ambao wametoka Ihefu hawana ng‟ombe, hawana mifugo yao, maisha yao ni magumu, hivyo tusibeze wakati wenzetu wakikuona kwanza wanaanza kulia.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninalimba Bunge langu Tukufu kwa umoja tulio nao na huruma tuliyo nayo watakaokuwa tayari tuanze kuchangia tuwasaidie wenzetu. Huu ndio umoja ninauona mimi utatusaidia angalau kunusuru tuonekana na sisi Bunge tunaonekana tuna umoja na tunafarijika kwa kuwafariji wenzetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo ninaingia katika hoja iliyokuwa mezani, nitazungumzia suala la maralia. Ukiachilia mbali UKIMWI malaria gonjwa ambalo linamaliza watu Tanzania, na bahati nzuri mwaka jana mwezi wa 12 nilihudhuria mkutano wa mabadiliko ya tabianchi (climate change meeting) ambao ilifanyika Madrid. Haya tunayoyaona walishayazungumza wenzetu mwezi wa 12. Walisema hivi; Afrika Mashariki kutatokea na maangamizi matatu; la kwanza mafuriko ambayo hayajawahi kutokea katika miaka mingi ndio haya tunayaona sasa hivi; lakini la pili kutokana na mafuriko haya na mvua za holelaholela mazalia ya mbu yatakuwa maradufu. Hivyo tutegemee ugonjwa wa Maralia ambao tulisema tunataka kuutokomeza bado tuna mkakati rasmi wa kuhakikisha maralia yamnatokomezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mheshimiwa Waziri Ummy Mwalimu tuko naye beneti katika suala la maralia, mimi ni Mwenyekiti wa Maralia; tuko nae kila siku yeye yuko kwenye kipaumbele kuhakikisha Tanzania yenye zero maralia inaanza na yeye na mimi nikifuatia na nyinyi vilevile mfuatie.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kimoja nataka nimuambie ndugu yangu Mheshimiwa Ummy Mwalimu, Mheshimiwa Waziri, mikoa mitano mikubwa ambayo ina maralia ambayo ni high burden maralia ni Lindi, Mtwara, Geita, Kigoma na Kagera; lakini baadhi ya watendaji wanataka kuvuruga. Wametoa ajira ya kwenda kusaidia hiyo mikoa basi wameandika mikoa 10 ambayo imepewa kipaumbele, nataka nitaje kwa majina, Dodoma ambayo ina only one percent, Singida, Geita, Shinyanga, Kigoma, Katavi, Kagera na Mara; lakini Lindi na Mtwara hamna ilhali Lindi ina 24 percent. Sasa tujisikieje? Tujisikie sisi tuendelee kufa kwa ajili ya watendaji wachache wanaotuharibia program zetu za maendeleo ya kutokomeza maralia wanaiacha Lindi na Mtwara hamna? Kwa bahati nzuri mimi gazeti ninalo na nitakupa ulifanyie kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ninaomba kitu kimoja, tu sitaki kubishana, naomba uiingize Lindi na Mtwara iwepo katika kundi la watu ambao ajira ipelekwe kwa watu kwenda kusaidia maralia hasa sasa hivi. Kutokana na mafuriko haya mimi nimekwenda site watoto wanatapika wanatisha. Ina maana wamekaa wanaumwa na mbu, hali ya maralia Lindi na Mtwara ni kubwa; na mafuriko yale kwa Lindi ina maana maralia kwao itakuwa ni maangamizo na vifo vitakuwa vingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaizungumzia suala la walemavu; Wizara hii ndio Wizara ya Walemavu. Tumepitisha sheria ya haki za walemavu lakini hakuna ajira ya walamavu. Walemavu wanaonekana ni kama kundi ambalo halistahili kupata ajira katika nchi hii. Tuna asilimia tatu ya walemavu tujiulize, Bunge lenyewe limeajiri walemavu kwa asilimia hiyo? Hapa ndani je, asilimia hizo zimetimia ina maana kwanza tujinyooshee sisi wenyewe ndani ya Bunge tunalitekelezaje suala la walemavu na ajira? Tunahitaji alama za sign language, hakuna Bunge. Watu wanakaa wanataka kuangalia Bunge linazungumzia nini, hakuna. Ina maana bado Bunge hawajajipanga kuhusu suala la walemavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Bunge kama Bunge tunaporidhia tuwe namba one kuhakikisha haki za walemavu zinaanza ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hapo tutasema kweli Bunge tumejisafisha ndipo tutake kusafisha maeneo mengine ya walemavu. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa kengele imegonga ya pili.

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumzia tena kuhusu hao walemavu kwanza nishukuru Serikali….

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili imegonga Mheshimiwa

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Naibu Spika, haaa haijatimia!

NAIBU SPIKA: Ahsante sana, shukrani.