Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati Kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019

Hon. Dr. Hussein Ali Mwinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwahani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati Kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika hoja hii iliyokuwa mbele yetu. Naomba niishukuru Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kwa maoni waliyotoa juu ya Wizara yangu ya Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa.

Mheshimiwa Spika, Kamati ilitoa maoni kwamba kukosekana kwa Sera ya Ulinzi wa Taifa kunaathiri ufanisi. Napenda niwaeleze tu kwamba sasa hivi tuko pazuri sana. Sera hii ilichelewa kwa muda kwa sababu tulikosa maoni ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kipindi kirefu, lakini nafurahi kulijulisha Bunge lako kwamba maoni yameshapatikana kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na kwamba kwa sasa wadau wanashirikishwa kwa maana ya vyombo vyote vya ulinzi na usalama kupitia maoni hayo; na rasimu ya sera yenyewe ili hatimaye ikamilishe mchakato ambao ni kupita katika Baraza la Makatibu Wakuu na hatimaye Baraza la Mawaziri. Nina imani kwamba suala hili litakamilika ili tuweze kupata sera na kazi zetu ziendelee vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, kukosekana kwa beacons za mipakani kunaathiri ulinzi. Ni kweli kwamba katika mipaka yetu kuna wananchi wamekuwa wakitoa beacons zile na kufanya shughuli za kibinadamu katika maeneo ya mipaka. Hili suala limeshughulikiwa kwa maana kwamba Wizara zote zinazohusika na suala hili; Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Wizara ya Ardhi, pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje, tulishakaa tukaamua kwamba sasa wakati muafaka umefika wa kurudisha beacons katika maeneo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vikao vilifanyika na wenzetu wa Kenya, Uganda na nchi nyingine na zoezi limeanza. Kwa upande wa Kenya tumesharudisha baadhi ya beacon na vilevile tunaendelea katika mpaka wa Tanzana na Uganda kurudisha beacon hizi. Kwa hiyo, suala hili linashughulikiwa na kiwango kikubwa kazi imeanza kufanyika.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa kuna suala la madeni ya Suma JKT kwa upande wa matekta. Ni kweli kwamba fedha bado hazijalipwa takribani shilingi bilioni 34, lakini juhudi kubwa zimefanyika na hivi karibuni tumeweza kukusanya zaidi ya shilingi bilioni tatu katika hatua hizo mpya. Tumeingia mikataba mipya na wale wote waliokuwa wamekopa ili sasa tuweze kuwafuatilia kwa karibu. Vilevile tumeweka Kampuni ya Udalali ya Suma JKT ambayo itakuwa inawapitia wote wanaodaiwa kwa madhumuni ya kuwadai na kuweza kurudisha fedha hizo. Kwa hiyo, hatuna shaka kwamba baada ya muda siyo mrefu tutaweza kuwa tunazirudisha fedha hizi ili ziweze kutumika kwa makusudio yaliyotakiwa.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa kuna hoja ya kutotolewa kwa fedha kwa Shirika la Nyumbu kunaathiri shughuli za utafiti wa shirika hilo. Ni kweli kwamba kwa muda mrefu fedha zinazotolewa kwa nyumba zimekuwa haba, mwaka huu wa fedha tuna shilingi bilioni 2.5 katika bajeti yao ambayo haikidhi kwa kweli. Nyumbu wamekuja na utaratibu mpya wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Kumi wa Shirika ambao wameutengeneza vizuri na wameweka bajeti ambayo kwa kweli itapita Serikalini. Tukiweza kupata fedha hizo shirika litarudi katika utaratibu wake wa awali wa kufanya tafiti za mazao ya kijeshi ili hatimaye tuweze kulirudisha katika ile dhamira ya kuwepo kwa shirika hili la Nyumbu.

Mheshimiwa Spika, ukiacha Kamati ambayo hoja zake zilikuwa ni hizo ambazo nimeshazitolea ufafanuzi, Mheshimiwa Maige alizungumzia kurudisha beacons ambayo na yenyewe nimeshaizungumza na Mheshimiwa Masele alisema Serikali iendelee kuipatia bajeti mashirika ya Nyumbu na Mzinga ili yaendelee kuzalisha mazao ya kijeshi na kudhibiti ulinzi katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza, mashirika yote mawili la Nyumbu na lile la Mzinga wameshatengeneza Mipango ya Maendeleo ya Miaka Mitano kwa Nyumbu na Miaka Kumi kwa Mzinga. Kwa maana hiyo, ni kwamba katika mipango ile ya muda mrefu wameweka bajeti zao pia, ni matarajio yetu kwamba bajeti hizo zitapatikana mwaka hadi mwaka katika kipindi hicho ili waweze kutekeleza majukumu yao kama inavyotakiwa.

Mheshimiwa Spika, pia kulikuwa kuna pongezi kwa Suma JKT kwa kazi nzuri ya ujenzi wanayoifanya katika maeneo mbalimbali kama Mererani, Ofisi za Serikali hapa Dodoma na kutoa mafunzo kwa vijana wetu. Tunapokea pongezi hizi na tunaahidi Bunge lako kwamba Suma JKT wataendelea na kazi zao za msingi za kulea vijana na vilevile kuzalisha mali.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)