Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati Kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati Kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia. Mimi ni mjumbe wa Kamati ya hii, na nilikuwa namsikiliza mjumbe mwenzangu na najaribu kukuangalia hata wewe ulivyokuwa unahangaika kutupa maelekezo sisi wajumbe wa Kamati.

Mheshimiwa Spika, wala usishangae. Labda tu nikukumbushe ni vizuri wajumbe unapotuteua kutupeleka kwenye kamati ukafuatilia na michango yetu kwenye kamati na mahudhurio.

Mheshimiwa Spika, kuna baadhi ya wajumbe umewateua wakishasaini wanaondoka haya ndio matatizo tunayopata. Haya tunayosema, tuna mahudhurio lakini pia tuna maoni kwenye maoni kwenye Kamati hakuna mahala ambapo Heche ameshawahi kuchangia, akisaini anasepa. Kwa hiyo ni vizuri pia ukatufuatilia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimemsikiliza vizuri mchangiaji mimi nilidhani mawazo alikuwa anayachangia kuhusiana na uchimbaji…

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Spika, kuhusu utaratibu, amenitaja jina.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA:… Mheshimiwa Spika, Heche sikutegemea kama atatoa haya mawazo…

KUHUSU UTARATIBU

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, nadhani umeona, haya ndiyo yanayotokea kwenye Kamati. Nimemsikia rafiki yangu, mdogo wangu amesema yeye ni chuma, chuma kinaanzia kwenye kuokosea kanuni kama hivyo. Lakini la pili nimekusikia vizuri ukimtafuta Waitara usingehangaika hata Ester yupo hapa kiboko yake; na chuma chepesi huwa kinaanziwa kuyeyushwa na moto mdogo ule wa wahunzi, sasa moto mkubwa unakuja mzee nadhani ungejipanga. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia. Maneno aliyoyazungumza mchangiaji kama mjumbe wa Kamati ambaye kwa asilimia 90 naye ni kama Musukuma anategemea maisha ya wachimbaji nilitegemea angekuwa mtu wa kwanza kumpongeza waziri kwa kazi nzuri aliyofanya. Haya maeneo yangezumzwa na Msigwa rafiki yangu anayefuga mbwa kule wala tusingepiga kelele. Lakini kusema ukweli Heche hujatenda haki. Leo haya maneno kama wachimbaji wanakusikia unailaumu Wizara ya Madini ninakushangaa; na nina imani una muda mrefu hujaenda kutembelea wachimbaji.

Mheshimiwa Spika, mimi natoka Geita aje Heche tumuonyeshe refinery inaojegwa na hatua zilizofikiwa. Haya mambo hatubabaishi, yamefanyika na yako yanaendelea…

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Spika, kuhusu utararibu.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA:… Mheshimiwa Spika, nilikuwa nashauri tu mambo mazuri yanapokuja kiukweli lazima kuwe na taratibu. Tunakuona vizuri sana Mheshimiwa Waziri unatusikia kwenye madini changamoto ndogo ndogo. Kwa mfano anayejenga (smelter) refinery kule Geita jaribu kuongea na Wizara ya Viwanda wampe vibali, amekwama kupata vibali vya EPZ, ili aweze kuendelea na uwekezaji wake kwa kuwa kuna vitu anakwamba kwenye kodi. Kwa hiyo ni vizuri ukazungumza na watu wa viwanda wajaribu kuwahisha michakato ili aweze kuendelea.

Mheshimimiwa Spika, kwa sisi watu tunaokaa vijiji, leo ukizungumza umeme, wapiga kura wakakusikia unamlaumu Kalemani Waziri wa umeme, yaani sijui. Mimi nadhani wakati mwingine ni wivu tu na lile neno ulilolisema, upinzani. Mimi jimbo langu tulikuwa hatujawahi kuona umeme awamu zote; hata huko kwao Heche; leo kwenye awamu ya tano mzee kijiji changu kila mahali ni mjini, kuna umeme. Leo unasisimama humu kweli Mheshimiwa Heche hata kwa hicho ulichonacho? Mimi nadhani Waitara hakukosea kuchukua maamuzi ya kwenda hilo jimbo, nimeanza kuamini. Kwa design hii watu wako watachelewa kufika, kwa hiyo ni vizuri wakakupiga chini akaja mtu mwingine.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumezunguka hii nchi sisi wajumbe, kila mahala tumeenda kukagua utekelezaji miradi ya meme na nishati na madini Heche tulikuwa wote, leo unakuja huku unaanza kupiga kelele kupinga mafanikio makubwa yaliyofanyika? Mimi naomba nikukushukuru sana kunipeleka kwenye Nishati na Madini. Kwa kuwa mimi natoka kwenye madini nikisimama hapa nakwambia mzee ingekuwa Spika unatutembelea Wabunge wako njoo utembelee mkoa wa Geita sidhani kama kuna mbunge hata rudi humu ndani. Kwa sababu watu wetu wana maisha safi, kila mahala ambapo tulikuwa tunafukuzwa leo tunachimba; kila mahali tulipokuwa tunavumbua dhahabu tunaletewa mabomu leo mambo ni safi, halafu anasimama mtu anakuja anaongea anaponda Wizara! Kwa kweli mmefanya kazi nzuri na hii serikali iendelee kuwa na moyo huo.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri yapo ambayo ningependa kushauri. Kwamba ni lazima tujaribu kuangalia hata kwenye uongozi wa huko kwenye mikoa. Tunafanya vizuri, mimi naamini wawekezaji wengi wazuri wa kati tunawatafuta sisi wachimbaji wadogo wadogo kwa kutumia akili zetu bila kusaidiwa na serikali. Lakini tunapowaleta wawekezaji wetu masharti ni mengi mno Mheshimiwa Waziri. Mimi nina mfano nina mwwekezaji yupo Geita, yupo Nyamauna wewe unamfahamu. Kila siku anapigwa faini mpaka amefunga mgodi. Mara OSHA mara idara ya kazi mara huyu migration faini milioni mia nane na kitu mchimbaji wa kati ataendeala kusaivaive namna gani?

Mheshimiwa Spika, nikiuombe Mheshimiwa Waziri, pamoja na kwamba utakuja kueleza vizuri una vyombo vyako, hao wawekezaji wachimbaji tunavyowatafuta mtu wa kuwalinda ni, wewe usikwepe mzigo. Kama wataondoka wanaopata kazi ya kwenda kuwatafuta ni sisi wachimbaji wadogo, hakuna mahala ambapo tunafurahia; tunaona, unamleta mtu mwenye mtaji wa bilioni tano anazopigwa faini, mara idara ya kazi, mara sijui hana kibali, mara sijui nini; milioni mia tisa na kitu. Nakuomba Mheshimiwa Waziri; na kitabu ninacho hapa naweza nikakukabidhi; ukajionea adhabu mwekezaji huyu wa Nyamauna alivyopigwa; idara ya kazi, sijui osha, sijui nini hadi amefunga mgodi na ni mwekezaji ameajiri watu zaidi 500, hii haiwezekani.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nikuombe wewe Waziri na Waziri wa Kazi na wanao husika muwa-guide wale watu mikoani wasione wale wawekezaji kama chanzo kukamilisha ujenzi wa madarasa; hii haiwezeikani nikuomba sana Mheshimiwa waziri uyazingatie haya.

Mheshimiwa Spika, nakushuru sana kwa kazi nzuri kamati hii ilivyozifanya nakupongeza Mwenyekiti kwa umetu-guide vizuri na wajumbe wengine wa CHADEMA wenye akili timamu nadhani wanaelewa. Ninakushuru sana.