Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019

Hon. Mbaraka Kitwana Dau

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa fursa hii. Nami nianze kwa kuwapongeza Wenyeviti wote wawili kwa mawasilisho mazuri. Nitakwenda kwa haraka kutokana na tatizo la muda.

Mheshimiwa Spika, nianze pale alipoishia Mheshimiwa Rehani, kuipongeza sana Serikali, Mawaziri wote wawili wa uvuvi upande wa Zanzibar na upande wa Tanzania Bara kwa kuondoa 0.4. Tumeanza kuyaona matunda. Pia nawe binafsi tunakushukuru kwa sababu mara ya mwisho tulipolizungumza hili jambo ulitia maneno yako na ninaamini Mawaziri wameyafanyia kazi na sasa tayari meli zimeshaanza kuja na tunapata mapato kama alivyosema Mheshimiwa Rehani.

Mheshimiwa Spika, nataka niendelee mbele kidogo kwamba Mawaziri wanasema wamesitisha kwa muda. Sasa ni muda muafaka sasa wakakaa wakaamua kama wanaifuta kabisa ama wanapunguza kiwango ama wanafanyaje ili hili jambo tulimaliza once and for all.

Mheshimiwa Spika, la pili, nilitaka nizungumze kidogo kuhusu suala la mkanganyiko wa matundu yale ya nyavu. Kuna sheria mbili hususan kule Mafia. Tuna sheria ya Hifadhi ya Bahari na tuna Sheria ya Uvuvi. Sheria hizi mbili zina mkanganyiko. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana, alikuja Mafia ametusaidia kwenye eneo la dagaa. Tayari mgogoro kule umekwisha, lakini kwa sasa bado tuna mgogoro kwenye eneo la samaki. Sheria hizi mbili bado zinaendelea kugongana. Naomba sana Mheshimiwa Waziri alifanyie kazi ili tumalize na hili tuweze kusonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, Mheshimiwa Waziri wa Uvuvi atakubaliana nami, maeneo ya kuvua samaki wengi unatakiwa uende kidogo maeneo yenye kina kirefu. Sasa kwa bahati mbaya Wizara inazuia matumizi ya cylinder gas ya kuweza kuzamia chini kwa ajili ya ma- divers kwa sababu wanasema kwamba wanaenda kuchukua majongoo bahari. Sasa watu wanapokwenda kuvua kwenye kina kirefu cha maji bila kutumia msaada wa gas cylinder tunawa-condemn to death. Tunaomba sana mliangalie hili, mlifanyie kazi ili kuruhusu wananchi hawa waweze kuvua kwa kutumia gas cylinder. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni suala la viboko. Mheshimiwa Waziri wa Utalii naomba anisikilize. Mwaka 2019 alituambia viboko wa Mafia watakwenda kupigwa mnada. Sasa hivi wameshafika 40 na wameshaanza kuingia mjini.

Mheshimiwa Spika, tunaomba sana Mheshimiwa Waziri wa Utalii mje muwaondoe wale viboko Mafia kabla madhara makubwa hayajaendelea kufanyika. Mpaka sasa mtu mmoja ameshafariki, ng‟ombe kadhaa wameshauawa na mazao yamekuwa yakiliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka kulizungumzia ni Channel ya Utalii. Mheshimiwa Kanyasu mwaka jana hapa ulijibu swali langu kuhusiana na Channel ya Utalii kuja kutangaza vivutio vya utalii kule Mafia vya samaki aina ya Potwe na vitu vingine ambavyo vinavutia kule Mafia lakini mpaka leo hili jambo halijatekelezeka.

Mheshimiwa Spika, Mafia ni sehemu ambayo ni ya kimkakati kabisa kiutalii, tungeomba sana Channel yetu ya utalii, ile ambayo inaoneshwa kwenye TBC waje kule wafanye shooting vivutio vile viweze kuonekana. Huyu samaki aina ya potwe tunamzungumza sisi tu humu ndani, watu wengi hawamjui, pengine hata Watanzania wengi nao pia hawamjui. Kupitia Channel yetu ile tunaamini kabisa mkitangaza tunaweza samaki yule akajulikana na vivutio vingine vinavyopatikana pale Mafia vikajulikana, ikatusaidia sana katika kuongeza mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kuhusu Kilimo cha Mwani; Mheshimiwa Waziri wa Uvuvi mwani Mafia unalimwa na kina mama kule baharini. Tunaomba sana, wakulima wa mwami hawana vifaa, utaalam, hajawahi kuja mtaalam yoyote kutoka Wizara ya Uvuvi kuja kuwapa semina au maelezo yoyote kuhusiana na kilimo cha mwani kule Mafia.

Mheshimiwa Spika, amezungumza hapa Bobali kuhusu zao la nazi na kwamba zao la nazi linapendezesha sana chakula kwa watu wa Pwani…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Dau dakika tano zimeisha…

MHE. MBARAKA K. DAU: …lakini…

SPIKA: Dakika 5 zimeisha Mheshimiwa Dau.

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja ya kamati, nashukuru sana. (Makofi)