Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019

Hon. George Malima Lubeleje

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpwapwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019

MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hoja hizi za Kamati mbili kwanza niwapongeze wajumbe wa Kamati, wenyeviti wa Kamati hizi vilevile niwapongeze Waheshimiwa Mawaziri wanafanya kazi nzuri sana.

Mheshimiwa Spika, nianze kuzungumzia sekta ya maji, maji ni uhai, maji ni maendeleo, maji ni uchumi. Wilaya zetu za Mpwapwa na Kongwa pamoja na Jimbo la Kibakwe kuna matatizo makubwa sana ya maji na nashukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Maji ametembelea maeneo yale kulikuwa na miradi mitatu ua minne katika Jimbo la Mpwapwa. Mradi wa Mima bado unasuasua kidogo lakini mradi wa Mzase, Iyoma na Gumila Mheshimiwa Waziri wa Maji alipofika katika jimbo langu aliagiza Katibu Mkuu, makandarasi walipwe na kweli walilipwa na miradi hii inaendelea vizuri.

Mheshimiwa Spika, naomba niishauri sana Wizara ya Maji, Makandarasi ambao mnateua, mteue makandarasi ambao wana uwezo. Pili mteue wakandarasi ambao wanaweza kutekeleza miradi bila kusubiri fedha malipo ya kazi ile ndio watekeleze mradi. Wakandarasi wa Serikali iwalipe mapema kwa sababu kuna wakati fulani miradi inachelewa tunalaumu labda wakandarasi kumbe wakandarasi hawa hawalipwi mapema. Kwa hiyo, naishauri wizara iwalipe wakandarasi hela mapema ili waweze kutekeleza miradi hii mapema.

Mheshimiwa Spika, la pili ni sekta ya mifugo, sekta ya mifugo nchi yetu ina mifugo mingi sana lakini inachangia pato la Taifa kidogo sana, sijui kama inafika asilimia 5. Bahati nzuri niliwahi kutembelea nchi ya Namibia na Botswana tulikwenda kule na Mheshimiwa Pinda alipokuwa Waziri Mkuu. Botswana wana mifugo michache sana kama milioni mbili hivi lakini mifugo yao inachangia pato la Taifa kwa kiasi kikubwa sana, asilimia 40 lakini mifugo yetu sisi pato ni kidogo sana. Kwa hiyo, tuwaelimishe wafugaji wafuge ufugaji bora.

Mheshimiwa Spika, kwangu pale Mpwapwa kuna kituo cha utafiti wa Mpwapwa, mifugo ya Mpwapwa. Nilishauri kwamba wakulima wa Wilaya ya Mpwapwa watumie kituo cha utafiti wa mifugo cha Mpwapwa ili kuboresha maisha yao kwa sababu wafugaji wengi wanahitaji wawe na makundi mengi ya mifugo lakini hawataki kupunguza mifugo yao ili kuboresha hiyo mifugo iweze kuongeza pato la Taifa.

Mheshimiwa Spika, lingine ni kuhusu sekta ya kilimo, sekta ya kilimo ndio inaleta pato kubwa sana katika nchi yetu. Katika kilimo kuna kilimo cha umwagiliaji kuna kilimo cha kawaida lakini kuna kilimo cha umwagiliaji. Utakumbuka katika jimbo lako na jimbo langu kuna miradi mingi sana ya umwagiliaji, ukiangalia bonde la Chamkoroma, Bonde la Mseta, Bonde la Tubugwe unakuja Bonde la Matomondo kuanzia Mwenzere, Mlembule, Tambi unakwenda mpaka Bonde la Mbori, Wagodegode mpaka Mabonde ya Lumuma na Malolo. Haya mabonde yangekuwa yanatumika vizuri kwa kilimo cha umwagiliaji nina uhakika hata tatizo hili la njaa lisingetokea.

Mheshimiwa Spika, skimu nyingi zimechakaa, ukitembelea miradi kwa mfano miradi katika langu na jimbo lako hii miradi tangu skimu zimekarabatiwa sasa ni miaka 5 au miaka 8 hazijafanyiwa ukarabati kabisa. Kwa hiyo, naishauri Wizara ya kilimo mkarabati hii skimu za umwagiliaji ili hawa wakulima waweze kunufaika na kilimo hiki cha umwagiliaji. Nchi yetu ina mabonde mengi sana na yakitumika vizuri kwa kilimo cha umwagiliaji nina hakika tutaondoa tatizo hili la njaa katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa na haya machache tu nakushukuru sana na naunga mkono hoja zote hizi mbili na niongeze tena kwa kuwapongeza Kamati na vilevile kuwapongeza mawaziri wanaoshughulikia hizi Kamati. Ahsante sana.