Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kwa Mwaka 2019

Hon. Naghenjwa Livingstone Kaboyoka

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kwa Mwaka 2019

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru tena kwa mara nyingine kwa kunipa nafasi ya kuhitimisha hoja hii muhimu ya Kamati. Naomba kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hoja ya Kamati na pia naomba kutoa ufafanuzi na maelezo ya
msisitizo kwa baadhi ya hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kuhusu utaratibu wa utekelezaji wa kazi za PAC, Kamati ya PAC inafanya kazi kwa mujibu wa Kanuni za Bunge. Hoja zilizowasilishwa na Kamati katika taarifa hii ni zile tu ambazo Maafisa Masuuli husika walihojiwa na Kamati na majibu ya hoja zao kufanyiwa uhakiki yaani verification na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo hoja ambazo hazikufanyiwa uhakiki na CAG na Maafisa Masuuli husika kutohojiwa hazikujumuishwa katika Taarifa hii. Kwa muhtasari hoja zote za Waheshimiwa Wabunge zimesisitiza utekelezaji wa mapendekezo ya Kamati katika maeneo mahsusi ili kuboresha usimamizi wa fedha za umma katika Serikali Kuu na Mashirika ya Umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, mapitio ya baadhi ya hoja hizo ni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Allan Kiula amechangia kuhusu hoja ya ukusanyaji wa mapato inayotekelezwa na TRA. Amesisitiza kuwa TRA ni roho ya Taifa, hivyo, lazima TRA ifanyie kazi changamoto kadhaa ili kodi zote ziweze kukusanywa kwa wakati. Ni vyema hoja na pendekezo la Kamati linalohusu weledi na ufanisi likazingatiwa. Aidha, kesi za kodi ni muhimu zikamalizika kwa wakati na zile kodi ambazo hazikusanyiki ni vema zifutwe ili vitabu vya hesabu za TRA ziwe sahihi. Aidha, Mheshimiwa Kiula amesisitiza pia kuhusu kukwama kwa Miradi ya TBA na NHC na hivyo mapendekezo ya Kamati kuhusu kukamilisha Miradi ya Taasisi hizi ni vyema yakazingatiwa ili kuokoa fedha za Serikali;

Mheshimiwa Ali Salim khamis ameongelea suala la kutokamilika kwa usimikaji wa mifumo ya usimamizi na udhibiti wa shughuli za Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA). Amebainisha namna ambayo Viongozi wetu Wakuu wa Nchi wamekuwa wakisisitiza kuhusu suala la mapato ya Bandari, hivyo anasisitiza TPA ikamilishe Usimikaji huo mapema ili kudhibiti mapato ya Serikali;

Mheshimiwa Felister Bura amebainisha kuhusu gharama zinazoongezeka kwa Miradi ya NHC iliyosimama kwa muda mrefu kutokana na Wakandarasi kuendelea kuwepo eneo la Mradi. Kama Waheshimiwa Wabunge walivyochangia mawazo, naye pia anasisitiza kutekelezwa kwa mapendekezo ya Kamati ya kuangalia namna bora ya kukamilisha Miradi hiyo ili kuokoa fedha za Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimimiwa Anatropia Theonest, mchangiaji wa nne pamoja na mambo mengine amesisitiza kuhusu umuhimu wa TRA kuendelea kuongeza ufanisi ili kufikia lengo la ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Kamati inaamini mapendekezo ya Bunge yatazingatiwa na mwaka ujao wa fedha TRA itavuka malengo ya ukusanyaji kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Joyce Sokombi amechangia kuhusu ucheleweshaji wa Miradi ya TBA kwa sababu mbalimbali kama usimamizi mbovu wa Miradi na uhamishaji wa vifaa katika miradi. Ametoa mfano wa Jengo la Tume ya Uchaguzi Dodoma, hivyo ni muhimu mapendekezo ya Kamati kuhua TBA yakafanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Kigua amelifahamisha Bunge kuhusu kupungua kwa hoja za Ukaguzi ikilinganishwa na miaka ya nyuma. Namshukuru pia Mheshimiwa Kigua kwa kutoa ufafanuzi kuhusu namna Kamati inavyoshughulikia hoja za Ukaguzi baada ya uhakiki wa CAG. Aidha, amesisitiza kuhusu umuhimu wa ukadiriaji sahihi wa kodi na kumalizika kwa kesi zaidi ya mia nane za kodi, amesisitiza kuhusu pia NHIF na NHC. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mambo mawili ambayo yamejitokeza ambayo nafikiri Kamati ni vyema tukayazungumzia, pamoja na kwamba tunasema kwamba mambo haya hayako kwenye, maeneo haya hayako kwenye Kamati yetu katika Taarifa hii, ni vyema mimi nikiwa Mwenyekiti wa PAC kwa vile yametajwa na kwa vile Rais wetu wa Nchi, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ametajwa kuhusiana na kumwajibisha Mheshimiwa Kangi Lugola ni vizuri pia nikataja mambo ambayo nafikiri kwamba yataweza kumfanya Rais Dkt. John Pombe Magufuli asionekane ni mtu wa double standard (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Anatropia alisema kwamba kama Mheshimiwa Kangi Lugola alitolewa katika nafasi yake kutokana na kutoleta Mikataba ya Zimamoto hapa Bungeni, yeye alitoa wasiwasi kwamba kuna Mikataba ambayo imeonekana haikuletwa hapa na ikafanya Kamati ishindwe kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ninachosema kama Mwenyekiti wa PAC ni kwamba, kwanza kuna Mkataba huu wa E-Migration, huu Mkataba Kamati ilikaa na ikaomba Serikali ilete ule Mkataba ili uweze kuufanyia kazi. Badala ya Afisa Masuuli kujibu au kuleta tukapata maelezo ambayo barua ninayo sina haja ya kusema details kwamba Kamati tulimalize tu maana lina mambo nyeti, kitu kilichonishangaza uandishi wa maelekezo haya hauonyeshi kwamba una weledi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza mwandishi huyu hakuweza kuelewa kwamba Kamati ya PAC inafanya kazi kutokana na taratibu zilizowekwa na Bunge hili Tukufu, Kamati haina Mamlaka kufuta hoja yoyote ya CAG kama hoja ile haikuletewa vielelezo au kama CAG hakuelewa au hakukubaliana na yale maelezo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo nilichukua hatua ya kuongea na Spika na kumwambia Mheshimiwa Spika, kazi uliyotupa PAC ni kufuata taratibu za Bunge, taratibu zilizowekwa na Bunge kwamba hela yoyote ya Serikali ambayo imetolewa lazima itolewe maelezo kwamba imetumikaje. Kutokana na huu mfumo wa E-Migration, kilichotakiwa siyo kuangalia kama kuna coding au kuna nini nyeti za ule mfumo, kilichotakiwa ni jinsi manunuzi yalivyofanyika kama Sheria ya Manunuzi imefuatwa, pesa zimelipwa ilivyotakiwa na ni kiasi gani ili kusudi hata mapato yanayotokana na hizi passports ionyeshe kwamba inawiana na investment iliyofanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikasema kama Mwenyekiti kwamba, inaelekea Rais hakushauriwa vizuri maana Rais angeshauriwa vizuri ingekuwa ifuatwe taratibu iliyowekwa na Bunge na ndiyo maana Rais alivyogundua yaliyotokea kwa Mheshimiwa Kangi Lugola alimsimamisha akamwajibisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama hivyo ndivyo tunategemea hata hili la E-Migration halijakwisha, bado tutalifanyia kazi pamoja na CAG na kuona kwamba utaratibu unafuatwa na kama kuna jambo lolote tunategemea Rais akae na Spika, ili amweleze tatizo ni nini, Spika aweze kumshauri kutokana na Sheria za Kibunge ili kuanzia hapo sisi na CAG Kamati ya PAC ndiyo tunaweza kukaa na kusema hili jambo limefungwa au bado. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala lingine ambalo mimi nilihusishwa na Kamati yangu, wachache wetu kuhusu uniform za Polisi, kuhusu uniform za Polisi maana tunataka kumtoa Rais wetu asionekane ana double standard, mimi nilikuwa nimesafiri, nilikuwa South Africa nikapata barua kwamba wenzangu wameteuliwa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na wachache wa Kamati yangu kwenda kuangalia zile uniform za Polisi, wakati huo alikuwa Mheshimiwa Zungu ndiyo Mwenyekiti wa Kamati hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikamwambia Mheshimiwa Zungu naenda kama nani kwa vile, mimi kama naenda kukagua na Kamati yangu, ina maana tumekaa na CAG tumepitia zile nyaraka zote zilizotakiwa maana suala la CAG halikuwa kwamba uniform tukazione kwa macho. Suala la CAG ilikuwa tuangalie namna uniform zile zilivyonunuliwa; je, huyo aliyepewa tender alipatikanaje? Uniform zililetwa kutoka wapi? Ziliingia bills of laiding ziliingia vipi, zikoje, kiasi cha fedha iliyotumika ni ngapi, from there ndiyo CAG aweze kwenda store kuangalia kuna nini? Kutokana na zile ripoti aone kwamba hizi uniform ziliagizwa 100, zimekuja 100, viatu viliagizwa 10 vimekuja 10? Kinyume cha hapo CAG hawezi kutoka akaenda kwenye store akaangalia kitu ambacho hana documentation kwamba anaangalia nini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kulikuwa na mis-conception ambayo Mheshimiwa Kangi Lugola ali miss-lead Bunge kwa kuapa na kusema atavua nguo kama uniform hazipo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ina maana hasomi hata taratibu za kwamba...

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ngoja tuongozane vizuri.

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, sawa.

NAIBU SPIKA: Wewe hapo sasa hivi unavyozungumza ni kana kwamba nawe ni mchangiaji wewe ni mtu ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ambaye umekasimiwa madaraka ili uje ujibu hoja za Wabunge na humpi mtu mwingine hoja na baada ya kuzungumza wewe, maazimio uliyotuletea Bunge litahojiwa.

Sasa kama unatupeleka kwenye hoja tena nyingine na wewe ndiye uliyeleta taarifa hapa ndani Mwenyekiti utakuwa unaliongoza Bunge sehemu siyo. Kwa sababu wewe unapaswa kuzijibu hoja za Wabunge na siyo kuuliza kwa sababu hakuna mtu wa kukujibu, Serikali kwenye hoja hii wao ni wachangiaji kama mchangiaji mwingine, sasa ukija na wewe unauliza maswali, sasa nani atakayekujibu hayo maswali na wewe hii ndiyo hoja yako wewe. Hii ni hoja Mwenyekiti, kwa hiyo hoja zote zilizoletwa na Wabunge wewe ndiyo unazijibu hapo siyo mtu mwingine.

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, sawa. Nakushukuru.

NAIBU SPIKA: Ngoja tuongozane vizuri, kama kuna hoja ambazo kwenye Kamati hamkuzimaliza hilo ni la kwako Mwenyekiti, Serikali haiwezi kujibu hapa.

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, sawasawa.

NAIBU SPIKA: Wewe ndiyo unayejibu hoja zote zilizotolewa na hata hayo maswali unayouliza nilikuwa nataka tu nione unaelekea wapi.

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, sawa.

NAIBU SPIKA: Hata maswali unayouliza yote ni ya kwako wewe utujibu hapa kama Bunge ili tuweze kuamua kwenye Maazimio uliyoyaleta wewe na Kamati yako.

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa muongozo wako na hapo ndiyo nilikuwa nafikia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ili nitalitaja huko kwamba bado hili tutalifanyia kazi, kwa hiyo, umenieleza vizuri sana na nimekuelewa. Nataka nisahihishe kwamba…

NAIBU SPIKA: Mwenyekiti samahani, nisikilize kidogo.

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo naendelea na hoja.

NAIBU SPIKA: Kwenye maazimio ya kwenye kitabu chako hiki hayo unayotaka kuyaleta, sina hapa mezani mabadiliko yoyote kwenye taarifa hii.

(Hapa baadhi Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge tufuate Kanuni zetu, kama unataka kuleta mabadiliko kwenye Maazimio lazima mimi niwe nayo hapa mezani ni wapi unabadilisha na hayo mimi sina, kwa hivyo Mwenyekiti huwezi kutoa ahadi hapo ukataraji tutalihoji Bunge kwenye hizo ahadi, hapana, siyo utaratibu kikanuni.

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimekuelewa. Ni kwa vile…

NAIBU SPIKA: Kwa hiyo wewe jibu hoja za Wabunge walizokuletea, huwezi kuanzisha hoja mpya ili Bunge lihojiwe, Bunge litahojiwa kwenye taarifa uliyoleta na Maazimio uliyoyaleta.

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, sawa nakuelewa sana na nakushukuru, nilitaka nitoe tu ile kwamba Rais asionekane ana double standard.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mwongozo wako…

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, maana kuna mambo ambayo inawezekana hakupelekewa ndiyo nilitaka tu kueleza hivyo.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, Mwongozo tu kidogo.

MBUNGE FULANI: …asituletee mambo yenu hapa…

NAIBU SPIKA: Hamna Mwongozo akiwa mtu anazungumza, wewe unajua Kanuni na nitakuruhusu uisome hapo umesema mwongozo hakuna mwongozo mtu akiwa anazungumza, naomba ukae.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu utaratibu…

NAIBU SPIKA: Naomba ukae, naomba ukae…

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu utaratibu…

NAIBU SPIKA: Naomba ukae Mheshimiwa Halima. Naomba ukae. Mheshimiwa Kaboyoka.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, Kuhusu Utaratibu…

MBUNGE FULANI: Nyamaza…

(Hapa baadhi Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nipende kumpongeza Mheshimiwa Waziri Biteko kwa jinsi alivyoeleza kuhusu STAMICO na hatua ambazo amezichukua pamoja na Waziri wa Fedha. Kwa hiyo, nasema kwamba pamoja na maelezo yao ambayo ni mazuri na nawashukuru kwamba wameonyesha picha halisi hasa Mheshimiwa Biteko ambaye ameonesha jinsi ambavyo STAMICO imeshughulikiwa bado tutahitaji kupata verification kutoka kwa CAG. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nahitimisha kwa kumshukuru Mheshimiwa Spika kwa uongozi wake thabiti, nakushukuru pia wewe binafsi kwa uongozi wa Bunge letu, nawashukuru Wajumbe wenzangu wa Kamati kwa ushirikiano wao mkubwa hadi kukamilika kwa taarifa hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni matumaini yetu kuwa Serikali itazingatia kwa ukamilifu uchambuzi wa Kamati na kutekeleza mapendekezo ya Kamati.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na nawashukuru pia Wabunge wote kwa kunisikiliza.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo, naomba kutoka hoja kwamba Bunge lako sasa lipokee na kukubali taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali PAC kuhusu shughuli za Kamati hiyo kwa mwaka 2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.