Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Kuridhia Itifaki ya Kinga na Maslahi ya Kidiplomasia ya Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (The East Africa Community Protocol on Information and Communication Technology)

Hon. Eng. Isack Aloyce Kamwelwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Katavi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Azimio la Kuridhia Itifaki ya Kinga na Maslahi ya Kidiplomasia ya Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (The East Africa Community Protocol on Information and Communication Technology)

WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kukushukuru wewe mwenyewe na Kamati ya Kudumu ya Miundombinu, ambayo ndiyo mshauri mkuu katika uendeshaji wa Wizara yangu ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamechangia katika itifaki hii pamoja na Kambi ya Upinzani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Kudumu ya Bunge, imeshauri maeneo saba wakati inawasilisha maelezo yake. Nikiri kwamba maeneo hayo nimeyapokea na kwamba yataendelea kufanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaje maneno machache ambayo Kamati ya Bunge imeshauri, kwamba ziko taasisi nyingine, kama akina Vodacom, akina Halotel ambao nao wameweka mkongo wa Taifa. Uzuri wa hii itifaki ni kwamba sasa inaweka misingi katika kujadiliana kuhusu masuala haya, kwa sababu iko imani kwamba hata nchi nyingine pia inawezekana kuna jambo kama hilo. Sasa baada ya itifaki hii, basi itifaki inaweka msingi, haya masuala yote yatajadiliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu udhibiti wa mkongo, kwa bahati nzuri nchi yetu tayari ina taasisi ya TCRA ambayo ndiyo mdhibiti wa masuala ya mawasiliano pamoja na hii miundombinu yote, zipo taasisi za Serikali ambazo zinadhibiti ili kuhakikisha kwamba shughuli yote inafanyika kwa usalama mkubwa na bila kupoteza mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati imehoji pia kwamba Tanzania sasa inaridhia, kwa hiyo, nchi nyingine zichukue hatua za kuridhia itifaki hii ili tuweze kwenda pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mheshimiwa Nsanzugwako, ametaja nchi tatu ambazo tayari zimesharidhia. Kwa hiyo, nasi tutakuwa wa nne, baada ya muda tutamalizia na hiyo nchi moja ambayo imebaki. Kwa taarifa tulizonazo, kila nchi inashughulikia suala hili kwa sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kambi Rasmi ya Upinzani, pia nayo ilitoa maoni mazuri tu, kwanza kuhusiana na gharama za maunganisho kuwa ni kubwa. Itifaki hii inakuja kujibu hilo, ikiwepo pamoja na gharama za roaming. Baada ya kuridhia itifaki, sasa tutakaa pamoja. Ni ukweli usiopingika kwamba taasisi za watoa huduma wa mawasiliano, kila taasisi ina tariffs zake. Kwa hiyo, kulikuwa na ugumu fulani, lakini baada ya itifaki hii, tutakutana nao na kujadiliana nao kwa sababu wanaotoa huduma Tanzania ndio wanaotoa huduma Kenya, ndio wanaotoa huduma Uganda, wawe na tariffs za pamoja ili gharama za roaming ziweze kuwekwa kwa pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia walizungumza suala la kuwa na sarafu ya pamoja. Kama nilivyozungumza kwamba itifaki hii, ndiyo msingi wa kujadiliana haya mambo yote ili kuhakikisha kwamba msingi wa itiofaki ni kwamba wananchi wapate gharama nafuu, basi unafikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru sana Wabunge wanne waliochangia, kuanzia na Mheshimiwa Ruth Mollel, akaja Mheshimiwa Nsanzugwako, Mheshimiwa Chumi na Mheshimiwa Maige. Kwa ujumla tu ni kwamba wote wamekubaliana na kuunga mkono itifaki hii iweze kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, itifaki inayopendekezwa kuridhiwa, inaweka misingi ya awali ya pamoja baina ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa nchi wanachama wanakubaliana kushirikiana katika masuala ya kujenga, kuendeleza na kutumia miundombinu ya TEHAMA, huo ndiyo msingi kwamba shughuli zote sasa, itakapofikia kwenye kuunganisha kwenye mipaka, tunakuwa tuko pamoja, kwenye masafa tunakuwa pia tuko pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno haya, kwa mujibu wa Ibara ya 63(3)(e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayolipa madaraka Bunge la Jamhuri ya Muungano kujadili na kuridhia mikataba yote inayohusu Jamhuri ya Muungano ambayo kwa masharti yake inahitaji kuridhiwa; na kama nilivyowasilisha, mapema leo hoja ya azimio, kwa kuzingatia Kanuni ya 54 ya Kanuni za Kudumu za Bunge, sasa naliomba Bunge lako Tukufu, kwa kuzingatia Kanuni ya 79 ya Kanuni za Kudumu za Bunge, kufanya maamuzi kuhusu Azimio la Kuridhia Itifaki hii ya Afrika Mashariki ya Mitandao ya Teknolojia, Habari na Mawasiliano na kwa lugha ya kigeni, East African Community Protocol on Information and Communication Technology Networks.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.