Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa FAO wa Kuzuia Uvuvi Haramu kupitia Bandari za Nchi Wanachama pamoja na Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Kuanzishwa kwa Ushirikiano wa Kimataifa wa Nishati ya Jua (The Framework Agreement on the Establishment of International Solar Alliance)

Hon. Mussa Bakari Mbarouk

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa FAO wa Kuzuia Uvuvi Haramu kupitia Bandari za Nchi Wanachama pamoja na Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Kuanzishwa kwa Ushirikiano wa Kimataifa wa Nishati ya Jua (The Framework Agreement on the Establishment of International Solar Alliance)

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Spika, ahsante; na mimi niungane na wenzangu kwanza kuunga mkono kuridhia nchi yetu kujiunga na itifaki hizi ambazo zilizotajwa hapa ambazo ni FAO na masuala ya umeme wa jua yaani solar power. Mimi nianze kuzungumzia kwenye suala hili la mkataba wa FAO.

Mheshimiwa Spika, wazungumzaji waliopita wamezungumza lakini ni ukweli usiofichika; ni kweli kwamba meli nyingi za nje zinavua katika bahari yetu bila sisi wenyewe kufaidika, na hili tuliligundua tulipokuwa kwenye ile Kamati Maaluma. Tukaona kwamba kuna meli zinakuja zinatumia bendera yetu lakini wanavua halafu mapato sisi hatupati kodi wala hatupati hao bycatch wanaotajwa.

Mheshimiwa Spika, labda Mheshimiwa Mwenyekiti wangu wa Kamati hakuifafanua vizuri hiyo bycatch. Ni samaki wale ambao wanaovuliwa hasa kuna Kanuni za kiuvuvi kwamba lazima katika ile nchi ambayo mmevua mpeleke samaki kwa ajili ya lishe kwa matumizi mbalimbali, labda kwa mfano kama kwenye watoto au shule au magereza ni Kanuni inatakiwa samaki wale washushwe hapo, na wasiuzwe.

Mheshimiwa Spika, lakini sasa kama alivyose aliyekuwa Mwenyekiti wetu; wamekuwa wakishushwa hapa; kwanza hatuna bandari ya uvuvi, kwa hiyo wanaposhushwa wajanja wachache wananufaika wanawachukua wale samaki halafu wanawuza; sasa hili Wizara nalo iliangalie. Mimi, si kwa kujipendelea, lakini niseme hii bandari ya uvuvi ni vizuri ikajengwa haraka na nilikuwa napendekeza basi kama kuna sehemu ya kujengwa basi ingejengwa Tanga kwa sababu hakuna msongamano mwingi kwa masuala ya uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo mimi niseme tu kwamba tu kwamba tumeona kwamba katika masuala mazima ya uvuviā€¦

SPIKA: Mheshimiwa Mbarouk ijengwe Tanga sio Kongwa? (Kicheko)

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Spika, Kongwa hakuna bandari, kwa hiyo hili jambo ni vyema tukalifanya.

Mheshimiwa Spika, pia tumeona faida zinazopatikana kutokana na kuridhia hii mikataba tumeona kumbwa tunapata fedha za mafunzo za kujenga uwezo lakini tunapata pia misaada ya vifaa vya doria. Kwenye nchi zetu tumejifunza kwamba nchi kama Seychelles, Mauritius na kwingineko wanazo meli za doria, sisi hapa hatuna. Sasa Serikali nao baada ya kuridhia hili jambo la uvuvi lakini iangalie namna ya kupata hizi meli za doria ambazo tukijiunga tutapata misaada lakini na sisi wenyewe pia tujipange kuwa nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine hata meli za uvuvi zitatusaidia tutapata ajira kwa vijana wetu lakini na Serikali itapata fedha za mapato mengi kutokana na uvuvi wa bahari kuu. Kama alivyosema msemaji mmoja, kwamba kama tukisimamia uvuvi wa bahari Kuu vizuri tunaweza tukapata fedha nyingi kuliko kwenye dhahabu na almasi; hili sasa tulifanyie bidii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo napenda kulishauri Bunge letu na Serikali kwa ujumla; kwa wale wenzetu ambao wamefanikiwa katika masuala haya, Serikali isione tabu katika kutumia fedha, kwa mfano ama kupeleka Waheshimiwa Wabunge kwenda kujifunza ama kupeleka wataalam wetu wakajifunze. Wanafarsafa wanasema, ukitaka kula lazima uliwe, kwa hiyo na sisi tuhakikishe kwamba tunapeleka watu wetu kwa kutumia fedha zetu ili tuweze kukusanya mapato vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini nikija kwenye suala hili la umeme, nimeona hapa kwenye huu mkataba wa Solar kuna mambo mengi ambayo sisi Tanzania tunaweza kusema sio kisiwa. Wenzetu wengi wamefanikiwa kutokana na umeme wa solar kwa sababu kwanza ni umeme wa bei rahisi, lakini hata bidhaa za viwandani zinashuka bei kwasababu gharama za uzalishaji zinakuwa ni ndogo na umeme wa solar ndio umeme wa bei rahisi zaidi duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine, niseme tu kwamba Serikali isisite kutoa elimu hii ya manufaa ya umeme wa solar kwa sababu wengine wanatia dosari, wanasema umeme wa solar kama ni fridge la futi tano haligandishi vizuri, umeme wa solar kwenye nyumba hauna nguvu vizuri, sijui kwenye welding haufanyi vizuri; kumbe tumeona baadhi ya nchi wanautumia huu umeme katika kila jambo.

Mheshimiwa Spika, nilibahatika kwenda Denmark, tukakuta wenzetu wanautumia umeme wa solar, wametega kila maeneo wameweka panel zinachukua umeme unakwenda magerezani, viwandani, shule, na kwenye vyuo. Wenzetu wananufaika, sasa sisi sasa kwa hili naomba na sisi tusibaki nyuma, tutumie umeme wa solar kuendeleza maslahi ya wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine, kuna mwekezaji mmoja kule Kigoma, yeye huyu anazalisha umeme wa megawatt tano; kuna sehemu inaitwa Kisenzi. Sasa TANESCO watu kama hawa iwasogeze karibu, iwe inasaidia, kwa sababu TANESCO haiwezi ikasambaza umeme nchi nzima bila kuwa na washirika. Sasa watu kama hawa nao watumike kuwasaidia maeneo ya vijijini kuwasambazia wananchi wetu umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho niseme tu, napo hata hapa katika masuala ya umeme wa solar tujitahidi sasa katika vyuo vyetu kama VETA, katika mafundi wetu hawa wanaotumia umeme huu wa TANESCO, nao wapewe elimu kwa ajili ya kujifunza kutumia umeme wa solar ili kuepusha gharama za umeme, na ili kuyafanya maisha ya wananchi wetu yawe rahisi zaidi. Ahsante. (Makofi)