Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. Richard Mganga Ndassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumve

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa nafasi hii ili nichanguie mpango ambao umeletwa kwetu kwa mujibu wa Ibara ya 94 kama ilivyo kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nauunga mkono sana mpango huu, kwa sababu ndiyo utaratibu wetu humu Bungeni, kwamba mara bajeti inayofuata, lazima kuwe na mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kitabu cha Mheshimiwa Dkt. Mpango, ameeleza vizuri sana naomba nisome kidogo tu. Katika mwaka 2021, Serikali itasimamia vipaumbele vifuatavyo; kuimarisha na kusimamia mfumo wa ukusanyaji wa mapato, lakini akaenda mbali zaidi, akasema, malengo ya mpango wa bajeti yanalenga kuimarisha makusanyo kwa kutekeleza hatua za kiutawala zikiwemo kuboresha mazingira ya kufanya biashara kwa wawekezaji kuimarisha uzimamizi wa ukusanyaji wa mapato ya kodi na yasiyo ya kodi, lakini akaendelea akasema, usimamizi wa sheria ya kodi, kupunguza upotevu wa mapato na kuyaanisha na kupunguza tozo ya ada mbalimbali zikiwemo za wakala wa Serikali ya matumizi ya fedha za umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la nidhamu ya matumizi ya umma ya fedha za Serikali, nianze kwanza kukupongeza sana sana Mheshimiwa Spika wetu ambaye ni Mwenyekiti wetu kwa kikao cha leo, kwa mambo matatu ambayo wewe umeonyesha kwa dhahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, jambo la kutuletea hizi tabulates hizi ndani ya Bunge, umepunguza sana sana matumizi ya karatasi ambayo yalikuwa yanatumia fedha nyingi sana za Serikali, ilielezwa kwamba matumizi yake kwa mwaka ni karibu bilioni 1.2. Sasa bilioni
1. 2 kama fedha hizi leo hatutumii tena, zitakwenda kwenye mipango mingine, kwa hiyo, nikushukuru sana pamoja na Ofisi yako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, hapo awali, Serikali tukiwa Bungeni, Wabunge wako, tulikuwa tunafanya vikao vyetu wakati wa kamati, tunafanya vikao vyetu nje ya maeneo ya Bunge, tulikuwa tunafanya UDOM, wengine wanakwenda Hazina, wengine sijui wanakwenda Mipango, wengine wapi, hiyo yote ilikuwa ni kutumia fedha visivyo, fedha za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa busara zako, ukaamua kwamba kuanzia sasa Kamati zote za Bunge, shughuli zake za kibunge zitafanyika katika majengo ya Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakushukuru sana, huwezi ukajua, kwa sababu huwezi kuiona moja kwa moja, fedha ambazo tulikuwa tunazitumia, hata sisi wenyewe Wabunge, tulikuwa tunatoka huko tuliko, tunakwenda UDOM, mara unapotea mara unarudi, unakuja tena hapa, mara unakwenda, matumizi yale tulikuwa tunatumia fedha lakini tunatumia na muda, kwa sasa, muda wetu ni mfupi sana unaotumika, tunatumia muda mwingi lakini tunatumia vizuri, kwa sababu shughuli za kamati za Bunge zinafanyika ndani ya eneo la Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, mtu mwingine anaweza akaona ni kitu cha kawaida, lakini siyo cha kawaida, ukiwa na miaka 10, miaka 20, umri unakwenda, kupanda zile ngazi za kwenda ghorofa ya nne, hasa mzee wangu Mheshimiwa Lubeleje, bahati nzuri sijui leo hayupo, kupanda zile ngazi kwenda ghorofa ya nne, iikuwa ni issue. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa busara zako na ofisi yako, hivi sasa leo kwenye jengo la utawala, lakini pia hata kwenye eneo ambalo kamati za Bunge zinafanyika, kote kuna lift, tunakushukuru sana sana kwa kuboresha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niishauri Serikali, kama tunataka tukusanye mapato yetu vizuri, yapo maeneo ambayo Serikali imeyaacha. Kwa mfano, ukipita hii njia ya kwenda Dar es Salaam, utakuna na malori ya mafuta, utakutana na malori ya mizigo, yenye namba, siyo za Tanzania, yenye namba za nchi za jirani, lakini ukienda kwenye ule mlango wa hicho kichwa cha gari, mmiliki wa hilo gari, tuna jina la mtanzania!

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali inapoteza mapato mengi kweli kweli na hili eneo hili, ukienda kwa wale wenywe wanakwambia kwamba malori haya yanaposajiliwa nje, Serikali inakosa mapato ya ndani, Serikali inakosa fedha ambazo malori hayo yangeweza kununua mafuta hapa Tanzania, tunakosa ajira na vitu vingine vingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe Serikali, tunajiuliza tu, hivi kwanini haya malori, kama lori hili lilikuwa la Mheshimiwa Ndassa, au lori hili lilikuwa la Mheshimiwa Ndugai la mafuta, badala ya kulisajili Tanzania nakwenda kulisajili nchi za nje, lazima kutakuwa na tatizo tu, lakini nyumbani kwangu ni Dar es Salaam, lakini lori lakwangu, ambalo nikilisajili kwa Tanzania, Tanzania itapata mapato. Mafuta yale, maana yake sasa hivi utaratibu wanaofanya, yale mafuta, hawachukui tena hapa, wanachukua hokohuko, wanakuja wamejaza, kama lita 400, wanakuja kuchukua mizigo na kurudi, mafuta hayo lita 400, ambayo sisi tunatumia kama kwenye road tall, sasa mapato hayo yanapotea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali, hebu turudi nyuma, ili tushauriane vizuri zaidi, ili malori haya ya mafuta na malori ya mizigo, yaweze kusajiliwa hapa, kama kuna tatizo sehemu fulani, basi turekebishe, kwa sababu hicho ni moja ya chanzo cha mapato ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, ili twende vizuri zaidi, katika kusimamia nidhamu na matumizi ya Serikali na haya mapato ili lazima yapatikane, lazima kuna mambo ya kufanya, ya kusimamia. Suala zima la rushwa, rushwa bado ipo, kuna mianya mingi ya rushwa ambayo inasababisha mapato yetu kupotea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe Serikali, suala zima la ruswa, lakini pia uaminifu kwa wafanyanyazi, uzalendo kwa wafanyakazi wa Serikali, kwa sababu tunataka mapato yetu yaende mbele zaidi, lakini tukitazama kwa miradi ambayo tumeiainisha miradi mikubwa hii, reli, bwawa, ndege na mengine, bila kuwa na vyanzo imara vya mapato, hatuwezi kufikia ile target ambayo tunataka ifikie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe sana Serikali, wale watu wote ambao wanasimamia maeneo hayo, lazima nidhamu ya matumizi iwepo, wizi, rushwa usipatikane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la mwisho, kwa sababu kengele imelia, nikuombe sana na Bunge letu Tukufu, TRA huwa tunawapa malengo, kwamba lengo lenu kwa mwezi huu ni kiasi fulani, halamshauri zetu lengo lenu ni kiasi fulani, sijui, sina uhakika, kama maeneo mengine yana utaratibu wa kuwekewa malengo. Sasa ombi langu, kwa sababu tunazo taasisi za Serikali, kama TANAPA, Ngorongoro na mengine, hebu, lazima tuwe na kautaratibu kazuri ka kuweka, siyo kuweka wao, kwa sababu taasisi hizi tunategemea ili ziongeze pato letu, tunategemea zitoe gawio, sasa kama watakuwa wanajipangia wao bajeti yao, target yao kwamba wakati wanaweza wakaenda mbele zaidi, kama walivyofanya TCRA Septemba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, walikuwa wamejipangia chini lakini wakakusanya trioni 1.8, au 1.7. Kwa hiyo, hata mashirika haya ya umma, ambayo tunategemea tupate gawio kutoka kwa hizi taasisi, bado malengo yao yanaweza Serikali ikayapitia kupita kwa TR, akapitia akasema, hapa wewe hapana umedanganya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lazima pia, hilo gawio, siyo wao ndiyo waseme kwamba sisi tutatoa gawio hili, hapana, Serikali iseme! Kwa kufanya hivyo, mtakuwa mmewasaidia kupunguza matumizi yasiyokuwa na utaratibu tukiaacha wakajiendea tu yale matarajio yetu hatuwezi kuyafikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vinginevyo, naipongeza sana Serikali ya Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri sana anayofanya. Nje na ndani sisi sote tunakubali kwamba hili ni jembe la Tanzania, siyo vinginevyo. Nawaomba hata ndugu zetu, hata kama hutaki kukubali, Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli ni Rais wa nchi hii, anafanya kazi nzuri, kla mtu anaona na kusikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama watu wa nje wanasifia, wewe uliyeko ndani utashindwa kusifia? Basi hata kama hutaki kusema, hata ukiwa nje sema basi kwamba Mheshimiwa Dkt. John Magufuli Pombe hoyee! Hata ukiwa nje!

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii, naunga mkono hoja. (Makofi)