Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. Mbaraka Kitwana Dau

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa hii. Nami nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujaalia uzima na afya ili leo tuweze kujadiliana masuala yanayohusu nchi nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana mtoa hoja Mheshimiwa Dkt. Mpango na Mheshimiwa Dkt. Kijaji kwa namna walivyoutendea haki Mpango huu ulio mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi zangu pia ziende kwa Waziri mwenye dhamana ya ujenzi kabla sijaanza kuujadili Mpango wetu huu. Namshukuru sana Waziri mwenye dhamana ya ujenzi, kivuko chetu kile cha Nyamisati kimeshaanza kujengwa na tumeahidiwa mwezi wa pili kitakuwa tayari. Kwa hiyo, nina kila aina ya sababu ya kumshukuru Mheshimiwa Rais pamoja na watu wote pale Wizarani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo, sasa nianze kuchangia Mpango. Umekuwa ukisisitiza mara kwa mara hapa kuhusu suala la namna gani sisi Wabunge tunaweza tukaingiza input zetu ili huu Mpango uwe bora zaidi. Waheshimiwa Wabunge mara nyingi wamekuwa wakizungumza upande wa matumizi zaidi, kila mtu anakuja barabara sijui gati kuliko namna gani tunaweza kuboresha Mpango wetu ukawa na mapato zaidi ili kuweza kufidia hii miradi ambayo sote hapa kila mmoja anavuta mradi unaomhusu kwenye Jimbo lake. Mimi nitakuja na mapendekezo ya namna bora ambavyo tunaweza tukauboresha Mpango huu ili Serikali ipate mapato zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ni kwenye eneo la uvuvi wa bahari kuu. Amezungumza kwa muhtasari sana ndugu yangu Mheshimiwa Ally Keissy pale. Kwanza nianze kukushukuru wewe binafsi, ulinifanya mmoja wa wajumbe katika ile Kamati inayochunguza namna gani Serikali inaweza ikanufaika na uvuvi wa bahari kuu, tumekutana na mambo mengi sana na ningeomba sana ile taarifa kama itawezekana tuifanye public kwa sababu kuna mambo mazuri mengi sana mle. Hata mimi mwenyewe pamoja na kuwa ni mjumbe basi huwa naihitaji hata kuipitia na kuidurusu lakini inakuwa ni shida kidogo kwa sababu bado haijawa public.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imezungumzwa kwenye Mpango kwa nukta chache sana, nadhani nukta tatu ama nne kuhusu uvuvi wa bahari kuu. Jambo la kwanza Serikali inaangalia uwezekano wa kujenga bandari ya uvuvi. Jambo la pili kufufua shirika letu lile la meli la TAFICO. Jambo la tatu ni namna gani tunaweza tukapata vifaranga vya samaki na namna za kuvifuga kwenye vizimba. Haya yote ni mambo mazuri lakini naomba tuangalie namna gani tunaweza tuka-prioritize mambo haya. Tukiyachukua yote kwa ujumla wake inawezekana pengine gharama zikawa ni kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kwanza tu-focus kwenye bandari ya uvuvi peke yake, tupate bandari ya uvuvi. Watu wengine walisema kwa nini Bandari ya Dar es Salaam msiweke magati mawili au matatu na kule Zanzibar nako kuwe na gati maalum kwa ajili ya meli za uvuvi, haiendi hivyo. Typical bandari ya uvuvi ni fully fledge bandari, inakuwa na logistics center zake nyuma kule. Samaki huwezi ukawachanganya na bandari ya cargo, huku kuna mbolea, huku unashusha sijui chemical gani halafu kuna gati lingine tena unashusha bidhaa ya samaki, hatutopata accreditation ile ya European Union kupeleka vyakula nje kwa sababu kutakuwa na contamination kutokana na mazingira ya bandari ya mizigo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunapozungumzia bandari ya uvuvi tunazungumzia kitu kikubwa sana, very complex na tungeomba Waziri alijue hilo. Kwa bahati mbaya sana mpaka leo hii Serikali bado haijajua hata site bandari itajengwa wapi. Tumeshatenga fedha katika bajeti kama tatu zilizopita kwa ajili ya upembuzi yakinifu, walau kupata kujua bandari tunaenda kuijenga wapi, Kilwa, Dar es Salaam, Bagamoyo, Mafia au wapi? Mpaka leo hilo tu halijaamuliwa. Bajeti hii tunayoitekeleza tayari kuna fedha za upembuzi yakinifu nadhani shilingi milioni 300 au shilingi 500, I stand to be corrected, za namna ambavyo mshauri atapatikana ili aweze kutushauri bandari inajengwa wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa dakika chache sana tuiangalie overview ya ile biashara yenyewe ya uvuvi wa bahari kuu. Eneo letu linaloitwa EEZ (Exclusive Economic Zone) la Tanzania ni zaidi ya kilomita za mraba 300,000 yaani hiyo ni nchi ndogo 10/15, hilo eneo lote ni la kwetu sisi. Kwa masikitiko makubwa eneo hilo lime-lay idle, hakuna kinachoendelea kule kwenye EEZ yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, amelizungumza Mheshimiwa Ally Saleh pale kwa muhtasari kwamba Serikali na nashukuru Waziri mwenye dhamana yupo hapa, Serikali mwaka 2016 waliweka kitu kinaitwa royalty ya 0.4 kwa kila samaki. Samaki wanaovuliwa ni aina ya jodari (tuna) basi, soko la dunia halitaki samaki mwingine yoyote asiyekuwa jodari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa walipo-introduce royalty ya 0.4 wale wenye meli kubwa ambao ili aje kuvua kwenye pwani yetu (EEZ) walikuwa wanalipa leseni moja ni mpaka Dola za Kimarekani 36,000 na kwa wakati mmoja kwenye EEZ yetu zinaweza zikawepo kule meli zaidi ya 100, unaweza ukazidisha dola 36,000 mara meli 100, hiyo ni kwa ajili ya leseni tu na tulikuwa tunapata hizo. Hata hivyo, hapa katikati mwaka 2016 tukaweka 0.4 kwa maana katika kila kilo ya jodari 0.4 inabidi iende Serikalini pamoja na yale malipo ya leseni, wale mabwana wakakasirika wakaondoka. Kwa hiyo huu ni mwaka nadhani wa pili au wa tatu, hakuna kinachoendelea kule kwenye EEZ yetu na samaki kama wanavyosema watu wengine siyo bidhaa ambayo ni kama dhahabu, ukichimba itaisha, samaki ni wanapita (gyratory), usimpovua wewe atakwenda Somalia atavuliwa, kwa hiyo, sisi tunakosa kwenye hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niliuliza jambo hili kwenye Kamati na Mheshimiwa Mpango atakumbuka nikaambiwa 0.4 imeshafutwa bwana Dau hujui, toka mwezi wa Nne imefutwa, nikawaambia haiwezekani Bunge la Bajeti tumezungumza 0.4 hapa na Waziri mwenye dhamana akasema tunaangalia uwezekano wa kuifuta hapa katikati, nadhani jana, majuzi nikaambiwa kuna maendeleo yanaendelea huko 0.4 imefutwa. Sasa naomba jioni tutakapokuja, Mawaziri watakapoanza ku-react na hizi taarifa basi watuhakikishie 0.4 imefutwa au haijafutwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, watuhakikishie ili tujue kwa sababu tunachopoteza ni kingi na tusipotoza haina maana kwamba, maana yake afadhali ile kauli unayosema Mwalimu Nyerere alisema hii dhahabu kama hatuna ufundi wa kuichimba ikae tu watakuja kuichimba vizazi vijavyo, lakini kwenye samaki hakuko hivyo, usipomvuna wewe ataenda kuvunwa Namibia. Kwa hiyo naomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa basi atusaidie namna gani ya kuona 0.4 inaondolewa na bandari ya uvuvi mchakato wake unaanza mara moja. Hilo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, hizi tozo kwa ujumla wake naomba Waziri wa Fedha na Mipango aziangalie, hizi Sectoral Ministries kila mmoja anakuja na tozo yake, inakuwa ni vurugu! Kwenye utalii kule, sijui TANAPA Waziri wa Maliasili na Utalii naye anaweka tozo zake, huku Waziri Mifugo na Uvuvi anaweka tozo huku, sijui Waziri gani naye akiona kidogo tu mambo yanakwenda vibaya anaweka tozo. Kunakuwa na utitiri wa tozo, naiomba Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango, ndiyo waratibu hizi tozo, hizi tozo kadri zinavyozidi kuongezeka...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Dau naambiwa eti ni kengele ya pili, lakini malizia nakupa dakika mbili umalizie.

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, basi la mwisho kwa dakika moja tu, nilishaongea na Mheshimiwa Waziri Mpango, hii leo naongea mara ya nne na nilimwambia kwenye Kamati sitaongea tena kuhusu suala hili. Kuna chanzo cha mapato kipo Mafia pale ambacho watalii wanatozwa kuingia katika maeneo ya hifadhi ya bahari, kila mtalii analipa dola 24. Tunamwomba achukue yeye kile chanzo, tunampa sisi chanzo kile aongeze mapato ya Serikali, awaambie TRA waende wakakusanye wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti,, nakushukuru sana kwa nafasi. (Makofi)

MWENYEKITI: Hebu hilo la mwisho yaani wakusanye badala ya TANAPA au?

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, hapana badala kuna Taasisi inaitwa Hifadhi ya Bahari (MPRU) ambao kimsingi wao kazi yao ni kuhifadhi maeneo na mazalia ya samaki, sasa tunapowapa kaziā€¦

MWENYEKITI: Badala ya kule kwa Luhaga Mpina enhe?

MHE. MBARAKA K. DAU: Ndiyo, sawasawa.

MWENYEKITI: Aaa, sawasawa. (Kicheko)

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa badala ya wao kuendelea kukusanya mapato, tunaona ile kazi ya mapato ni kazi ya TRA, wafanye TRA, halafu sisi tushughulike na uhifadhi.

MWENYEKITI: Nimekusikia Mheshimiwa. (Kicheko)

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.