Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. Prof. Norman Adamson Sigalla King

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. PROF. NORMAN A. SIGALLA KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata nafasi hii kuchangia kidogo kuhusu Mpango huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natanguliza kwanza shukrani kwa Rais wangu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kazi kubwa na nzuri anayoendelea kufanya mpaka sasa hivi. Mungu ambariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nikapata nafasi ya kushiriki ziara ya siku 21 ya mafunzo ya uendeshaji wa ndege, bandari pamoja na reli (SGR) pale China. Nilichojifunza ni nini? Nilichojifunza ni kwamba Bandari ya Bagamoyo ni mpango halisi wa Wachina wa kutaka kuisaidia Tanzania kujikwamua kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu kwamba Serikali ina macho/sura nyingi inavyoangalia jambo hili lakini jambo lenyewe hili usahihi kabisa ni kwamba niliongea na Wachina wakanionesha michoro ile, wakaonesha jinsi ambavyo Bandari ya Bagamoyo itakuwa inalenga kukwamua uchumi wa Tanzania. Pia wakaonesha kwamba tayari kuna makubaliano ya Mawaziri wetu wa Uchukuzi na nchi za Burundi na DRC Congo ya jinsi ya kuhakikisha kwamba wana-ferry chuma Msongati kwa kutumia Bandari ya Bagamoyo. Kwa hiyo, wao walipokuwa wanapeleka nguvu kuhakikisha kwamba wanajenga reli ya SGR wanafikiria zaidi kwenda Uvinza, Msongati, Burundi kwa sababu tayari kuna makubaliano ya kimkataba ya nchi ya Tanzania na Burundi. Pia kuna makubaliano ya mkataba kwenda Kalemi kwa sababu ya nchi ya Congo DRC na Tanzania pia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema kwamba suala la Bandari ya Bagamoyo ni ni muhimu sana kwa Tanzania. Sina hakika kama Serikali ina taarifa sahihi kuhusu jambo hili kwa sababu tumekaa pale siku 21, siku 21 za mafunzo ni nyingi sana kwa mtu mzima lakini tumekaa pale tukajadiliana na tukaoneshwa waziwazi jinsi ambavyo Bandari ya Dar es Salaam itazidiwa nguvu kama chuma cha Msongati kitachimbwa inabidi kipelekwe Bandari ya Bagamoyo ifanye ferrying ya chuma kile. Kwa hiyo, nafikiri ni vizuri sana ijulikane hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata Mradi wa Chuma wa Mchuchuma na Liganga na nimesema mara nyingi hapa, huu ndiyo mradi ambao sisi Watanzania ni wa kujivunia. Napata shida sana kuelewa kwa nini Serikali inapata shida kupeleka fedha na kutia saini mikataba ya Chuma cha Mchuchuma na Liganga kwa sababu mradi huu upo wazi. Ni kweli kabisa kama mchangiaji mwingine alivyosema kwamba miradi hii inasaidia sana kuongeza ajira za watu wetu kwa wingi sana. Bandari ya Bagamoyo, Mchuchuma na Liganga ni miradi ambayo itaongeza ajira kubwa sana kwa watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia ni kweli you cannot do anything now without China, ndio ukweli. Ukweli wa mambo kwa uchumi wa sasa hivi ukifanya skeleton ya uchumi wa dunia unavyokua huwezi ukajitenga na China, haiwezekani. China kwa sasa hivi is a leading country kwa uchumi. Nasikitika sana kusema hivyo kwa sababu China walinifikisha mahali ambapo waliona nafaa kuwa Mwenyekiti wa nchi 16 walioenda China lakini pia waliniona mimi kama ni unique person kwa sababu natoka Tanzania nchi ambayo wao wanaipenda. Kwa hiyo, wakaniambia kwamba wanakusudia kuifanya Tanzania kuwa ndio hub ya uchumi wa China Afrika kwa sababu reli inayojengwa Nigeria (Enugu) kuja Bujumbura inaunganishwa na reli inayokuja Msongati kwenda Bagamoyo, ndiyo master plan yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wao walikusudia kwamba Tanzania itakuwa ndio hub ya uchumi wa China Afrika. Walisikitika sana kuona kwamba Kenya wamekuja of late wamekubaliana kutengeneza reli ya kutoka Mombasa kwenda Nairobi kwa sababu mpango ulioanza ni wa kwao wa Dar es Salaam kwenda huko tunapopeleka lakini Kenya wakaja nyuma yake wakajenga reli ya kutoka Mombasa mpaka Nairobi na imeshakamilika na wanatengeneza fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana Serikali iangalie kwa makini sana juu ya China. China ni nchi ambayo inatupenda sana sisi na sisi tuna mahusiano ya damu na China, sio mahusiano ya kubahatisha. China kama akikosea tunaweza kuwaambia, tukiwaambia wanakubali na wanaelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Tanzania na China tuna mahusiano ya muda mrefu, mahusiano ya Mwalimu Nyerere na Mao Tse Tung ni ya muda mrefu. Kwa hiyo, ni hawa hawa waliojenga SGR hii ta TAZARA ya Dar es Salaam kwenda Zambia na wamejenga miaka hiyo wakati hatuna uwezo. Kwa hiyo, leo hii kwa nini tuone kwamba wao ni shida? Nafikiri lazima Serikali iangalie vizuri ili kufika mahali ambapo tunaweza tukafanya vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukifanya hivyo tutafanikiwa sana. Tanzania ni nchi bora sana lakini tutumie kwa usahihi nafasi na fursa ambazo tunazo. Tusipotumia kwa usahihi fursa tulizonazo tutapata shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni muhimu sana ku-resort into these plans ili tuweze kwenda nazo mbele, tusisikie maneno ya watu. Maneno ya watu wengi ni kutufanya sisi Tanzania tusifanikiwe. Wanasema China imefanya hivi, wanatoa mifano ya China kununua mgodi wa Zambia, tunaoujua vizuri uchumi wa China tunasema siyo kweli, kilichotokea Zambia ni kingine na Tanzania tunafanya vingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni muhimu sana Serikali yangu ya Tanzania ikubali ushauri huu iutekeleze mradi wa Bagamoyo na chuma Msongati. Mungu awabariki sana. Amina. (Makofi)