Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. Selemani Said Bungara

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Kilwa Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nashukuru sana kupata nafasi hii, leo kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu ambaye anajua la mtu ambalo liko ndani ya moyo wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza natoa shukrani kwa Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuniletea miradi, kuhusu afya nimepata vituo vya afya vitatu, na katika jimbo langu kuna vituo vitatu na vyote vimepata fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ile barabara ya Kwa Mkocho-Kivinje, ambayo nilipiga kelele kwa muda mrefu sana tangu awamu ile ya nne, alhambulilah barabara imeisha, tunashukuru sana. Jambo lingine ambalo nashukuru sana kuna VETA Chuo cha Maendeleo, kimejengwa, kinaendelea vizuri sana, tunashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kuna mahakama ni nzuri kwelikweli, mahakama imekwisha, Alhamdulilah. Kwa hiyo, kwa kweli nashukuru, mengi ambayo nimeomba na niliyasemea katika Bunge hili, yametekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na waswahili wanasema mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni. Sisi ni wanasiasa, kuna wakati jambo likiwa zuri lazima tusifie, lakini kuna jambo likiwa siyo sawasawa, lazima tukosoe, na hiyo ndiyo siasa, hakuna aliyekamilika katika dunia hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachokiomba sana, sisi tuna Bandari Kilwa Masoko pale, sijaona katika mpango wako Mheshimiwa Mpango, kama bandari ile ambayo ina kina kirefu tena cha asili, sijaona katika mpango wako kama ipo na itekelezwe. Pia kuhusu habari ya maji, kuna mradi mkubwa sana, Mheshimiwa Mpango naona siku moja tuliyokaa, nakushukuru sana Mheshimiwa Mpango, mradi wa maji ule umeingizwa katika mpango wa Mradi wa India, katika ile miji midogo 29 na ule upo, ni mradi mkubwa sana. Naomba utekelezwe na Inshallah utatekelezwa kwa sababu nimeona katika mpango wako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja hayo, yote tunayopanga haya, kama hakuna utawala bora, kama hakuna utawala bora, sawasawa na kutwanga maji katika kinu. Tunakusifieni sana, kwa huduma za jamii mmejitahidi, lakini utawala bora, tatizo na ninamuomba Mheshimiwa Magufuli, aangalie katika hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania imefika katika hali mbaya, mlianza kwa kutisha, nchi ikawa kuna utekaji mwingi, kuna mauaji mengi, mkazuia mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, hakika Watanzania tumetishika! Hapo mmefaulu sana katika utawala bora! Tumetishika! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo, katika Wilaya yangu ya Kilwa, Jimbo la Kilwa Kusini, tumesimamisha wagombea katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa, katika vijiji 15 tulivyosimamisha hata kijiji kimoja hakuna aliye…

MBUNGE FULANI: Kwa chama gani?

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: CUF wewe hujui? (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wameondolewa katika uchaguzi, kuna mtu mmoja kaondolewa, kuna Kijiji kimoja cha Nanjilinji wameondolewa, walisema wao hawajui kuandika kingereza na hawajui kusoma kiingereza! Sasa katika fomu pale unaulizwa, chama chako gani? The Civic United Front, Chama cha Wananchi, ndiyo ameambiwa mmesema uongo! Ninyi mlisema kwamba hamjui kuandika kiingereza mbona mmeandika civic, wameondolewa sababu hiyohiyo tu! (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuseme, wametolewa wajumbe wangu 25 wa Kijiji cha Nanjilinji A kwa kuandika The Civic United Front, ninyi mnasema uwongo! Aa, jamani, sisi tumenukuu tu kadi yetu imeandikwa, sisi tukaangalia tukafuatosha tu, aaa! Mmesema uongo! Wangeliandika CUF, wangelitolewa, kwa sababu hakuna chama kinaitwa CUF, wakiandika The Civic United Front, wanakwambia wewe ulikuwa hujui kuandika kingereza, hujui kuandika kingereza, inakuwaje kuwaje? Imefikia hivyo Tanzania kweli! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mwingine ametolewa katika kinyang’anyiro, kwa kuandika Waziri, binti jina lake Fatuma Waziri Juma, basi katolewa kaambiwa hatujui jina linaloitwa waziri, jina… walah wabilah nayo! Hakuna jina linaloitwa Waziri, waziri ni cheo! Katolewa, walah wabilah watalah. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakwenda wapi? Tunaweka pingamizi, tunaambiwa, pingamizi lako umeandika mwenyekiti, badala ya kuandika uenyekiti, huna sifa! Huna sifa, unaomba nafasi ya uenyekiti! Wengi, hata CCM inawajua, wameandika hivyo hivyo, wengine wameandika uenyekiti, wengine mwenyekiti, basi unaondolewa, kugombea kwa sababu umeandika mwenyekiti, aaa! Lengo si lilelile unayegombea cheo cha uenyekiti, sasa mtu unasemaje! Tuseme nchi hii imefikia hatua hii, kweli jamani! Kukosea neno moja, ndiyo unaondolewa katika uchaguzi!

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini, cha ajabu sasa, twende leo wewe nani huyu, Mhagama wewe, twende mimi na wewe katika Kituo cha Msaidizi, tukachukue fomu za CCM, walah wabilah, wameandika vibaya kushinda sisi, lakini ninachojua, kanuni inasema, mteuzi atakuwa msaidi, na msimamizi masaidizi, aliitwa Ikulu! Sasa mtu kaitwa Ikulu, huyu anataka kusimama, hebu simama wewe. (Kicheko)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa, Mheshimiwa.

T A A R I F A

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge na hasa kwa kusifia kazi nzuri iliyofanywa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kwenye jimbo lake, na vilevile vazi lake zuri sana na linaakisi Shirika letu la Ndege Tanzania, kwa hiyo, anapongeza pia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba, hayo yote anayoyasema, Serikali imeshatoa taarifa, hao wote waliokuwa wanaitwa akina Waziri, wametoka Najilinji, walioandika kina Fatuma, waliondika uenyekiti, mwenyekiti, kama wanaona wameonewa, wakate tu hizo rufaa zitasikilizwa na mwisho wa kuzisikiliza ni kesho!

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile, ninaomba tu nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge, awe tu na subira, kesho, itampa matokeo yoyote yale ambayo yanaweza kuashiria hicho ambacho kimeonekana na ninamshukuru tu anakili kwamba kwamba, mtu amekosea kosa moja, kujaza fomu ya uchaguzi ni kama mtihani, ukikosea umekosea! Kwa hiyo, asubiri tu matokeo ya rufaa yatampa ukweli na uhakika wa kila kitu. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Bungara unasemaje kuhusu taarifa?

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza siyo taarifa, yeye kaniweka sawa tu. Nimekuelewa, nimekuelewa sana, lakini na hili la kusema, The Civic United Front, maana yake hilo la kukosea ndiyo umekosea, ndiyo umeandika sawasawa, lakini kosa lako unaambiwa wewe hujui kingereza, kwa kuwa umeandika kingereza toka, wewe unasemaje hilo, wewe unasemaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, huu ni mpango maalum, ni mpango maalum! Naomba sana, naomba sana, sisi watu wazima! Mnakoipeleka nchi siyo sawasawa, mnatutisha, mtu pengine kafumaniwa tu, kaenda kukata shamba la mahindi, kafyeka fyeka siyo sababu ya uchaguzi mnasema, kakata sababu ya uchaguzi, pengine alimfumania.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Bungara ahsante sana