Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. Deo Kasenyenda Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makambako

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kunipa nafasi ili niweze kuchangia. Kwanza nianze sana kwa kuishukuru serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. Magufuli kwa kazi nzuri inayofanya juu ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nimshukuru Waziri Mpango na Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Wizara kwa ujumla kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya. Nichukulie tu kwa mfano; kazi ambayo Mpango unafanya nichukulie tu kwenye Jimbo moja tu la Makambako acha nchi nzima ambako kazi inafanyika kubwa; mmeweza kutupa fedha nyingi ambazo hivi sasa wakandarasi wako site wanafanya shughuli za kusogeza huduma ya maji kwa Wananchi Ikelu, Ibatu, Nyamande, Mtulingala shughuli hizo zinaendelea vizuri, nakupongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile mmetupa fedha ambazo tunajenga hospitali pale ya Halmashauri ya Mji wa Makambako. Mmetupa fedha, shilingi bilioni 1,500, juzi mmetuongezea tena shilingi milioni 500. Kwa hiyo, hospitali ile inakwenda vizuri. Pia mmetupa fedha tumejenga Kituo cha Afya pale Lyamkena. Kwa hiyo, napongeza sana na kazi mbalimbali ambazo zinaendelea kufanyika katika Halmashauri yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana ukienda kwenye suala hili la uchaguzi, kwanini watu wamejitoa, wanasema Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Serikali za Mitaa amezungumzia kwamba watu wasijitokeze kwenye ofisi. Siyo kweli. Nizungumzie tu kwenye Jimbo langu; kuna Kata 12. Kata saba hakuna mtu aliyejitokeza hata mmoja. Kwa hiyo, hata kabla hawajasema hili, tulishinda tayari Kata saba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sasa wameona mwelekeo wa nchi nzima. Hilo ni Jimbo moja. Muelekeo wa nchi nzima, wameshaona tayari ushindi haupo. Kwa hiyo, wakaona ni vizuri watangaze kwamba wanajitoa, hakuna jambo kama hiyo.

MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Ehe, Mheshimiwa Sanga, hebu subiri.

T A A R I F A

MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nataka kumpatia taarifa mzungumzaji kwamba kwenye Kata zake 12 hawakujitokeza wagombea. Siyo kweli. Katika Kata zote walijitokeza Wagombea wa Chama cha CHADEMA. (Makofi)


MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Sanga, unaikubali Taarifa au unaikataa?

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua huyu ni dada yangu sasa…

MWENYEKITI: Unaikubali au unaikataa?

MHE. DEO K. SANGA: Naikataa, siyo kweli. Siyo kweli! Nitampa tu mfano. Pale Ngamanga ambako palikuwa panaongozwa na CHADEMA hawakujitokeza kwa sababu tumejenga zahanati na wao wamekiri na Mwenyekiti yule ameacha. Kwa hiyo, napongeza sana kwa kazi ambazo zinafanywa na Serikali ya Awamu ya Tano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kazi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano na ndiyo maana nilisema wakati ule, kwa nini Rais huyu asiwe wa maisha? Narudia tena, sasa ili mipango ikamilike kwa shughuli ambazo zimeanza za reli, ndege na kadhalika, ni vizuri muda utakapofika 2025 aongezewe hata miaka mitano ili miradi iweze kukamilika vizuri.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa, Mheshimiwa Bungara.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Eeeh!

MWENYEKITI: Haya.

T A A R I F A

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampa Taarifa kwamba naunga mkono kwamba Katiba ibadilishwe azidishiwe muda, pia na vyama vya upinzani navyo vifutwe…

MWENYEKITI: Mheshimiwa hebu kaa chini. Kaa chini! Mheshimiwa nitakutoa nje sasa hivi, kaa chini. Mheshimiwa Sanga, endelea.

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Vyama hivyo vitajifuta vyenyewe kwa sababu hawaelewi wanakwenda mbele au wanarudi nyuma. Vitajifuta vyenyewe. (Makofi/Kigelegele/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa Mheshimiwa Dkt. Mpango, kwa sababu sasa tumenunua ndege zaidi ya saba na tunataka angalau sasa viwanja vyote katika mikoa yetu viweze kuruhusu ndege kutua; kiwanja chetu cha Njombe ambacho hivi sasa mlituambia kwamba kiko kwenye mpango wa kutengeneza ili ndege zetu hizi ziweze kutua. Naomba tukamilishe kiwanja kile cha Njombe ili Wana-Njombe nao waweze kusafiri kwa ndege zao ambazo zimenunuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo liko kwenye mpango ni juu ya Liganga na Mchuchuma. Liganga na Mchuchuma ikianzishwa na ikakamilika, uchumi wa Mkoa wa Njombe na uchumi wa Taifa utaongezeka kwa asilimia kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kilimo, sisi tunaotoka Kusini tunategemea sana pembejeo aina ya mbolea ya DAPO na Urea, ndizo tunazozitumia sana katika mazao yetu; na mbolea hizi ziko katika bei ya juu. Pamoja na kwamba kuna bei elekezi, tunaomba tuwe na mpango shawishi kwa wawekezaji waweze kujenga viwanda vya mbolea katika nchi yetu, angalau vitapunguza bei za mbolea na kuwa chini hasa mbolea ya DAPO na Urea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu wamezungumzia juu ya kukamilishwa kwa maboma, nami naunga mkono. Tuna maboma ambayo yamejengwa na wananchi, Waheshimiwa Madiwani na Waheshimiwa Wabunge, likiwepo Jimbo la Makambako. Tumejenga maboma mengi; tuone namna ya kutenga fedha kukamilisha maboma haya, mengine yameshaezekwa, yanasubiri tu kupigwa ripu na kukamilisha na kadhalika ili maboma haya yaweze kukamilika kwa muda muafaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tuna miradi mikubwa, mmojawapo ukiwa wa maji, ule wa mkopo nafuu wa fedha kutoka Serikali ya India ambao utakamilisha miji karibu 28. Katika miji hiyo 28 na Njombe, Wanging’ombe, pamoja na Makambako ipo; tunaomba miradi hii, wananchi wanaisubiri kwa hamu sana ili kuweza kutatua tatizo la maji katika Mji wetu wa Makambako na mahali pengine ambako miradi hii itapitiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la ujumla ambalo nilitaka niseme, hili nalirudia tena; Mheshimiwa Dkt. Mpango, katika mipango ambayo umekuwa ukiipanga; ya miaka mitano na huu ambao tunaujadili hapa sasa, endelea, songa mbele. Kazi yako ni nzuri, unakwenda vizuri, Watanzania wanakutegemea. Wanategemea sana kwa mipango hii ambayo tunaijadili hapa. Mungu akubariki na akuongoze na amlinde Rais wetu ili kusudi tuweze kukamilisha miradi hii. Mawaziri wote ambao wanafanya kazi yako, wanafanya kazi nzuri na ndiyo maana shughuli zinakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)