Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. Saada Salum Mkuya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Welezo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. SAADA MKUYA SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Mpango wetu wa Maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, nitoe pongezi zangu za dhati kabisa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jinsi anavyoliendesha gurudumu hili la maendeleo hapa Tanzania. Ameonesha weledi mkubwa hususan katika kuweka usimamizi mzuri kabisa wa rasilimali zetu lakini kurejesha nidhamu ya kazi hususan kwa watumishi wa umma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Naibu Waziri pamoja na timu yote. Kwa kweli mpango hadi kufikia hapa tunaletewa sisi na tunasomewa na kuona kwamba kila kitu kimepangika basi siyo kazi nyepesi, ni kazi ngumu lakini tumeweza ku-manage na kufika leo kwa mujibu wa ratiba ilivyopangwa. Pongezi zenu sana na katika kipindi hiki kwanza nampa pole sana Mheshimiwa Waziri Dkt. Mpango kwa baridi lakini naamini ata-manage kuchukua maoni yetu haya, haitamuathiri of course. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wangu kwanza naomba nitoe maoni ya ujumla. Mpango wetu ni mzuri umepangika na unaeleweka vizuri lakini kidogo naomba katika yale maeneo ya usimamizi ama maeneo ya tathmini ni lazima sasa tuweke wajibu wa kila mdau katika mpango ule. Ukisoma sasa hivi utaona ni wadau wachache wamewekwa pale lakini naamini kwamba kila mmoja wetu kwa nafasi yake ana nafasi kwa ajili ya kutekeleza Mpango wetu wa Maendeleo lakini vilevile ana nafasi kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wenyewe wa Mpango wa Maendeleo. Kwa hiyo, naomba utakapokuja Mheshimiwa Waziri au hiyo version nyingine itakayokuja ambayo ndiyo itaweka frame ya bajeti yetu, wadau wanaohusika katika utekelezaji na tathmini waelezwe kwa kina. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe mfano, kwa mfano, Waheshimiwa Wabunge hatukutajwa katika Mpango kama as if sisi wajibu wetu tu ni kutoa recommendations hapa lakini actually sisi tuna wajibu wa kusimamia na kuchukua maelekezo haya na kuwapelekea wananchi tunaowawakilisha. Katika changamoto moja iliyoainishwa humu ni kwamba wananchi hawaelewi kwa kina kuhusiana na Mpango huu, sisi kama Wabunge, mbali ya kutoa recommendations hapa lakini tuna wajibu wa kuchukua haya maoni na kila kitu na kuwapelekea wananchi ambao ndiyo tunaowawakilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wananchi wenyewe wana wajibu wa kutekeleza Mpango huu. Kwa hiyo, nashauri wadau wanaohusika waelimishwe vizuri kuhusiana na mpango na sisi kama Wabunge tuna kazi hiyo lakini tuna kazi vilevile ya kupitisha bajeti hapa kwa ajili ya utekelezaji wa Mpango. Kwa hiyo, hili ni suala technical ambalo nadhani litakwenda kufanyiwa kazi wala halina shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine ni dogo tu, hizi projects zilizoainishwa humu kuna ujenzi wa campus ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kwa upande wa Zanzibar. Nadhani ili hili likae vizuri, campus ile ya Zanzibar sasa hivi inaitwa Kampasi ya Karume. Kwa hiyo, naomba tukiiandika tuwe tumeiandika vizuri kwamba sasa hii campus ya Zanzibar siyo campus ya Zanzibar ni ya Karume na imeekwa hivyo kwa umuhimu wake. Kwa hiyo, lazima tu-take note on that. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende katika maeneo specific. Pengine katika miaka miwili, mitatu iliyopita wakati tunachangia Mpango wengi wetu hususan sisi Wabunge ambao tunatoka Zanzibar tuli-take note kwamba Mpango haukuainisha kitu chochote ambacho kinahusiana na Zanzibar. Inawezekana majibu yalikuwa ni kwamba Zanzibar wana Mpango wao, that’s good lakini Mpango huu wa Maendeleo una areas of support kwa Zanzibar na nadhani ni muhimu tukazieleza ili sasa katika improvement ya Mpango iwe imeainishwa vizuri. Kuna maeneo ambayo hakuna namna lazima yaingie kwa sababu ndiyo wajibu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa upande wa Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye masuala ya uwekezaji (investment); inawekana kabisa siyo jambo la Muungano, lakini international cooperation ambayo ndiyo msingi wa kupatikana EFDI’s, ni suala la Muungano. Sasa ikiwa tutaangalia ku-enhance International Cooperation kwa maana ya mashirikiano ya kimataifa bila ya kuangalia upande mwingine katika context ya uwekezaji, hatuwezi kufanikiwa. Huu Mpango wa Taifa una wajibu vilevile wa kuangalia maeneo ambayo yanavuka yanakwenda Zanzibar. Hayo maeneo tunapenda angalau yawe yameainishwa katika Mpango huu, siyo lazima katika utekelezaji wa moja kwa moja, lakini katika mipango yetu ni lazima yaoneshwe kwenye uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingine tunaona kuna makongamano ya wawekezaji yanafanyika, lakini tukiuliza pengine labda ushiriki wa Zanzibar uko wapi, utaambiwa hili siyo jambo la Muungano, lakini international cooperation pale ni jambo la Muungano na ni jambo ambalo linabebwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo hatuwezi kukwepa kwa namna nyingine yoyote, ni lazima tushirikiane kwa pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kuhusiana na biashara, ni vizuri Mpango wetu huu wa mwaka 2020/2021, unaangalia hasa kuimarisha biashara kimataifa pamoja na biashara kikanda. Biashara (Inter Trade) kwa maana ya Tanzania Bara na Zanzibar bado imekabiliwa na changamoto kubwa sana hususan pale ambapo biashara ama pale ambapo bidhaa zinazozalishwa Zanzibar zikitaka kuja sasa Tanzania Bara angalau ku-access soko, zinakabiliwa na changamoto kubwa. Biashara ya kikanda, biashara ya kimataifa haitaweza kuimarika kama biashara ndani ya nchi, ndani ya pande mbili itakuwa inakabiliwa na changamoto. Hili lipo katika wajibu wa outline ya Mpango huu ambao tunauelezea na hili ni lazima liangaliwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi Mheshimiwa nadhani Jaku aliuliza swali kuhusiana na changamoto hizi za biashara lakini majibu mepesi, majibu ya moja kwa moja yanayotelewa ni kwamba haya mambo tunayapeleka katika Kamati ya SMT na SMZ. Unajua vitu vingine viko katika capacity yetu, ile Kamati inakutana siyo mara nyingi na kwa wakati mmoja hatuwezi kuainisha changamoto zote zinazoukabili Muungano wetu. Pengine mambo mengine sisi kama watendaji tunafaa sana tusaidie hawa viongozi wetu, siyo lazima twende katika Kamati ile, lakini sisi katika capacity yetu tumeteuliwa kwa sababu ya kuwa na capacity ya kusimamia maeneo yetu. Tunaweza kabisa kuyachanganua bila ya kupita katika kamati, katika cooperation zetu, katika Wizara zetu na taasisi zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo, hii inawezekana si moja kwa moja kwenye Mpango, lakini Mpango una wajibu wa kuhakikisha kwamba hata ule Mpango wa Maendeleo wa Zanzibar na wenyewe unaendelea na unafikiwa ili kuleta matumaini mazuri ya maendeleo kwa Watanzania wote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni utalii, tunashukuru sana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa bold vision hii ya kununua ndege zetu. Ndege pamoja na benefits nyingine, ndege hizi zinatumika katika kutangaza utalii, lakini hakuna ndege hata ambayo at least ina nembo ya utalii kwa upande wa Zanzibar. Hakuna! Shirika la Ndege la Tanzania ni Shirika la Muungano. Kwa hiyo ni wajibu hata basi tu kuwe na connotation labda Stone Town au karafuu. Yaani angalau tuwe tumebeba dhana ya utalii kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hilo halipo. Kwa hiyo tunaomba utalii siyo jambo la Muungano lakini tools za utalii zinabeba Muungano wetu. Tunaomba basi angalau consideration hiyo iwepo na iwe inatekelezwa. Presence ya Zanzibar katika Shirika letu tuwe tunajua kwamba this is ours, tuwe tuna ile sense of ownership. Tunapongeza sana hizi hatua lakini tunajua kwamba obligation hii ipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye masuala ya umeme tulipiga sana kelele kuhusiana na VAT. Nashangaa mambo madogo kama haya tunachukua muda mrefu sana kulumbana katika nyumba hii, lakini hatimaye hilo limekuwa tunaishukuru sana Serikali. Gharama za umeme bado na Mheshimiwa Waziri amekuwa akisema mara nyingi kwamba hilo jambo linafanyiwa kazi. Linaendelea kufanyiwa kazi, linaendelea kufanyiwa kazi kwa kipindi cha miaka mitatu, lakini wananchi wa upande mwingine wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanaumia na maisha. Mpango huu wa maendeleo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hautakuwa mpango successful kama kwenye sehemu nyingine katika Jamhuri…..

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante sana.

MHE. SAADA MKUYA SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)