Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. Wilfred Muganyizi Lwakatare

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Bukoba Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mchango wangu utajielekeza kwenye mambo mawili, kwa haraka haraka. Jambo la kwanza Mheshimiwa muwasilisha hoja na msaidizi wake na hasa msaidizi wake (Naibu) wanatambua kabisa kwamba takwimu ambazo zimekuwa zinatolewa zimekuwa zinaonesha Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mikoa maskini. Binafsi naamini Kagera haina sababu ya kuwa maskini au kutambulikana kuwa maskini. Nachoamini ni kwamba Mkoa wa Kagera haujatengenezewa mipango ambayo ingeweza kutumia fursa za geographical position ya mkoa pamoja na fursa nyingine kuwa mkoa ambao unachangia pato la Taifa na watu wake kwa matajiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kupitia Mpango huu naomba upelekee kuwepo mipango ambayo inaweza ikachochea uwekezaji wa kibiashara pamoja na uwekezaji utakaoshindana au utakaokuwa kwenye nafasi ya kushindana na biashara zilizoko katika nchi jirani. Mkoa wa Kagera ni mkoa ambao una advantage kuliko mikoa karibu yote ya Tanzania kwa kupakana na nchi nne ambayo ni mipaka ya moja kwa moja lakini pia inapakana na nchi mbili japo siyo moja kwa moja lakini nchi hizo mbili una uwezo wa kuendesha gari kwenda mpaka kwenye makao makuu ya nchi hizo na ukarejea katika mji wa Bukoba, nchi za South Sudan pamoja na DRC Congo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sasa kwamba uwepo mpango maalum wa upendeleo, taratibu za kikanuni, za kisheria zisaidie mpango huo wa kuifanya Kagera kuwa na mipango maalum ya kiuwekezaji na hata ikibidi mpango huo uwe wa upendeleo wa kipindi maalum, kama ambavyo imewahi kufanyika kwenye baadhi ya mikoa ikiwemo Dodoma wakati tunajenga Makao Makuu ili Kagera isiendelee kuhesabika kama mkoa maskini kwa sababu tu ya mipango ambayo ni mibovu. Mheshimiwa Mpango na hasa Naibu wake ambaye naamini amefika Mtukura, Lulongo, Rusumo, Kabanga anaweza akawa shahidi yeye mwenyewe jinsi upande wa pili biashara zinavyochanganya lakini ukiangalia upande wa Tanzania ni wakiwa. Mimi nafikiri ni suala la mpango ili kwa kweli Kagera iwe ni gate la nchi za Afrika Mashariki pamoja na nchi za Maziwa Makuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na suala hili, tunakumbuka katika kampeni za mwaka 2015, Mheshimiwa Rais wakati akijinadi miongoni mwa ahadi alizozitoa katika Mkoa wa Kagera ni kuifanya Kagera kuwa sehemu maalum ya kiuwekezaji. Sasa naona kipindi kinayoyoma sijui huu mpango tunaoujadili sasa nafikiri unaweza ukanusuru na ahadi ya Mheshimiwa Rais ikatekelezeka. Pia katika kuweka kiki kubwa zaidi katika kikao cha RCC cha juzi ambacho kimefanyika pale mjini Bukoba na nafikiri Mheshimiwa Mwijage ni shahidi alihudhuria hicho kikao ni kwamba mkoa umepitisha suala hili kama azimio na naamini tayari limeshafikishwa katika ofisi husika ili Mheshimiwa Mpango hili suala aliweke katika mpango wake kwa sababu ni jambo ambalo limeridhiwa na limepitishwa katika vikao vyetu vya RCC. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya pili, naamini mpango huu na ndivyo ilivyo kwamba ndiyo utakaozaa bajeti ya mwaka 2020/2021 na hiyo bajeti itasheheni mabilioni ya kuingia kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2020. Experience ya chaguzi ndogo za Madiwani, chaguzi ndogo za Majimbo na hata uchaguzi unaoendelea hivi sasa wa mchakato wa Serikali za Mitaa, hautoi picha nzuri kwa taifa letu kama kweli tuko serious na mfumo wa vyama vingi. Mbaya zaidi tumekuwa tunaonekana tunapoteapotea, mipango ya kiuchaguzi tunaonekana hatujawa wazoefu badala ya kuwa uchaguzi inaonekana unakuwa uchafuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri hatupaswi kuwa na mipango na kupanga bajeti kubwa kwa chaguzi ambazo zinaacha watu wamepigwa, vilema, watu wamefungana na zaidi watu wameongezeana chuki, hawasalimiani na wanafungana. Kwa kweli huo hautakuwa ni uchaguzi wa kuweza kuleta tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka wakati Mwalimu akiwa mojawapo ya watu walioshadidia na kupitisha mfumo wa vyama vingi japo watu waliopiga kura asilimia ilikuwa ndogo, Mwalimu alikuwa na matumaini makubwa na mfumo wa vyama vingi kwamba itakuwa kitovu cha watu kuchakata mawazo ya watu tofauti na kujenga mipango ya kuweza kujenga uchumi endelevu kwa faida ya watanzania, ndiyo ilikuwa vision ya Mwalimu. Pia, mtakumbuka kwamba Mwalimu wakati alipoona kwamba hatujawa tayari katika suala la kuchimba madini, alifanya maamuzi ya makusudi kuweza kuahirisha kwamba tusihusike katika suala la madini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitamke kabisa, nilikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha CUF kwa muda mrefu sana tu. Nilishuhudia mambo yaliyotokea baada ya uchaguzi wa Zanzibar mwaka 2001 ambayo ilisababishwa na dalili ninazoziona hata hivi sasa kwa Tanzania Bara. Tukifanya mchezo tunakwenda kuchafua nchi yetu kwa sababu za kiuchaguzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mambo yako hivi, mimi ningeshauri, kuliko kuendelea chaguzi kuwa sehemu ya kutesa watu wetu, basi tuunde mfumo tofauti na huu tulionao, iletwe sheria, ifanyike research tuwe na mfumo tofauti wa kupambana hivi na hivi na hivi ili uchukue nafasi ya mfumo tulionao sasa hivi ambao kwa kweli siyo endelevu. Kwa kweli wananchi wao walikuwa na utashi, wameonesha kuupenda mfumo wa vyama vingi lakini watu wenye ubinafsi mimi naona hawaupendi mfumo huu kwa sababu zao binafsi. Kipimo pekee cha kuonesha watu kwamba wana utashi, huu uchaguzi wa Mitaa umefanyika baada ya miaka minne yote hakuna mikutano ya vyama vingi, hakuna mikutano ya kisiasa lakini…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Lwakatare naona bado dakika mbili.

MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Sawa.

MWENYEKITI: Unaweza ukachangia Mpango sasa.

MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo mpango wenyewe, mimi nataka kupinga huu Mpango utakaotuletea fedha ya bajeti ya uchaguzi utakaoharibika na kutochagua viongozi bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi, kitendo cha wananchi kujitokeza kwa wingi baada ya kuzuiwa kufanya mikutano, zaidi ya 92% na ndiyo takwimu sahihi, nafasi 92 ziligombewa, halafu unakuja kuwaondoa inabaki 12% kwa takwimu tulizonazo, haitupi matumaini mema huko mbele. Mimi naamini CCM walipaswa kutumia fursa hii kuzipima project ambazo CCM wanazitaja kwamba zimefanyika kuwaachia watu ambao wanagombea waende kuzinadi ili wachaguliwe kwa sababu ya project nzuri zilizofanyika wapate kura lakini hiki kitengo cha kutumia mlango wa nyumba…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Lwakatare, ni kengele ya pili.

MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Naam.

MWENYEKITI: Ni kengele ya pili.

MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru lakini Mheshimiwa Mpango ningeomba bajeti na mpango wa ku-provide fedha kwa uchaguzi ambao ni uchafuzi bora hiyo fedha isitolewe na tuwe na mfumo mwingine, kama CCM wabaki wenyewe basi waendelee wenyewe kuliko kuwa na uchaguzi wa kuwaumiza watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)