Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia mapendekezo ya mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikupongeze sana Mheshimiwa Waziri Dkt. Mpango kwa kazi nzuri unayoifanya, wenye macho tunaona. Na usitegemee kusifiwa na kila mtu Mzee Dkt. Mpango, nikuombe usikate tamaa, tufanyie kazi. Sisi wenye uhitaji na msaada wako na akili yako bado tunayo imani na tunaendelea kukushauri uendelee kupiga kazi, Watanzania tunakuamini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikiliza wasomi wetu hawa, amesema Waziri aliulizwa faida ya ndege akasema dola milioni 14, nilikuwepo kwenye kupokea ile ndege, ni sawa milioni 14 lakini kama msomi alitakiwa kuelimisha umma faida ya ndege haiji kwenye ndege peke yake, vipo vitu vingi ambavyo kwa kupitia ndege tulizozileta tumeshapata faida. Ingetokea muda wakataja faida zote ambazo baada ya kuleta ndege. Sasa tatizo ndio hili Mheshimiwa Heche unazungumza halafu unakimbia, ungekaa humu ukasikiliza.

Angeweza kupata fursa ya kuambiwa faida ambazo tumeshapata kwenye hizi ndege, haya maneno hayatakiwi kuzungumzwa na mtu msomi kama hawa. Ndio maana tukisema vilaza watu mnaanza kutuzomea humu ndani. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Taarifa.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Musukuma naomba muendelee tu.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba tumshauri ndugu yetu Mheshimiwa Dkt. Mpango. Tunaona kazi ambazo mnazozifanya za kuweza kubuni vitu ambavyo kiukweli kila mtu anafurahia Serikali ya Awamu ya Tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwana ushauri mchache; Serikali imeamua kurudi Dodoma, ni lazima tubuni vitu ambavyo baada ya miaka mitano tunaona sasa hivi Dodoma inaenda vizuri kwenye makusanyo labda kwenye kuuza viwanja na kodi za majengo lakini tungebuni vitu ambavyo baada sasa ya hivi vitu kuisha tuwe na kitu cha kudumu hapa Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Mheshimiwa Waziri tungeweza kutengeneza bandari kavu Dodoma, kukawa na ICD Dodoma ambapo makontena yanayoenda Rwanda na Burundi yawe yanachukuliwa Dodoma hapa hapa. Tutakuwa tumetengeneza chanzo kikubwa kwanza kwenye treni yetu itakuwa inatoa makontena kuleta hapa lakini tutapata ajira ya malori kusafirisha makontena kuleta hapa na malori ya Burundi na Rwanda hayataenda tena Dar es Salaam, yataishia Dodoma na kurudi. Tutakuwa tumefungua chanzo kikubwa sana kwa wananchi wa Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, naishukuru pia Serikali, katika watu waliofaidi kwenye Awamu ya Tano na mimi naweza nikajisifu nimefaidi. Ile kauli ya Mheshimiwa Rais ya juzi kwamba halmashauri zote zirudi kwenye maeneo ya wananchi, Halmashauri mojawapo ni ya Geita DC ambayo imerudi Nzela naipongeza sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba kukueleza tu Mheshimiwa Mpango kwamba kwenye mpango sasa uweke, tumekubali tumerudi kwenye nyumba hizohizo tunabanana. Kuna halmashauri ambazo tayari walikuwa wana pesa wameshaanza kujenga lakini kuna Halmashauri ambazo hatukukuwa na bajeti kabisa kwenye kipindi hiki, tumerudi sasa tumeamua kuanza lakini kwenye mpango ujao tunaiomba Serikali ifikirie namna yoyote ya kuweza kutuma pesa kwenye hizi halmashauri ambazo hazikuwa kwenye huu mpango wa kujenga majengo ya halmashauri na nyumba za watumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nilikuwa napenda kushauri pia kwenye suala la viwanda. Tunaipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuhamasisha viwanda na kuja na Sera ya Viwanda, lakini nilikuwa na ushauri mdogo. Mawazo ya Mheshimiwa Rais ya kusema tuwanyang’anye viwanda watu ambao wameshindwa. Ni mawazo mazuri, lakini ninyi Wasaidizi wake, mngeenda mbali zaidi mkafikiria. Kabla ya kuwanyang’anya viwanda, mngewanyang’anya mawazo yao kwanza; mkawaita mkawasikiliza, mkawauliza ni kwa nini walikwama kuendeleza viwanda? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna mtu anayeweza kuingia pressure ya kukopa fedha kwenye Taasisi za Benki ukafungua kiwanda halafu ukakitelekeza. Haiwezekani! Lazima kuna sababu zilizopelekea watu wakashindwa kuendesha viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakupa mfano. Twende wazi tu, awamu iliyoisha haikuwa na mfumo wa kuendeleza viwanda vya Tanzania. Huwezi ukafungua kiwanda ukazalisha kitu ukakiuza shilingi 1,000/= halafu kinaletwa kutoka China kinauzwa shilingi 200/=, kwa vyovyote vile lazima utakimbia tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, hawa watu ambao walikuwa na viwanda ambavyo Serikali mmevichukua, ni vizuri mkawaita mkawapa nafasi. Mfano ni mzuri tu, tulimshauri vizuri kipindi kile kuhusu dhahabu; na walipowaita watu wa dhahabu wakawaeleza matatizo yao, leo unaona pesa wanazokusanya kwenye dhahabu. Vivyo hivyo Mheshimiwa Rais aliwaita watu kule Ikulu akawasikiliza, wakamweleza matatizo yaliyoko TRA. Leo unaona kila mtu hapa anasimama anasema bandari imejaa makontena. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri, hebu awaite hao watu walionyang’anywa viwanda; hata Serikali tunachukua tu viwanda, lakini hatuna alternative. Mmechukua viwanda, leo ni miaka miwili tumevifunga tu; hamwashi mashine, hamna ulinzi, watu wanajiibia tu vitu vya watu. Namwomba Mheshimiwa Waziri awaite, awasikilize, wakwambie wamekwama wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nataka nikuhakikishie, Wafanyabiashara mliowanyang’anya viwanda wako tayari kuandika commitment ya kuvifungua viwanda hivyo kwa sababu Serikali yetu inalinda viwanda vya ndani. Kwa hiyo, nina uhakika hata nikiingia madeni nitazalisha kitu nitauza. Haiwezekani ukasema mimi ninazalisha chini ya target. Utazalishaje kitu hakinunuliwi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri hebu wachukue hawa watu tuliowanyang’anya viwanda, awaite azungumze nao, waandike commitment, wafungue viwanda na ndiyo msimamo wa Serikali ya Awamu ya Tano, Serikali ya Viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nilikuwa najaribu kumshauri Mheshimiwa Waziri, kwenye Mpango ujao, nilikuwa namsikiliza mtu mmoja jana aliulizwa swali, Naibu Waziri wa TAMISEMI akajibu. Mimi natoka kwenye Halmashauri, kumekuwa na purukushani huko, kila Halmashauri inaandika andiko la kujenga masoko, stendi na minada. Mheshimiwa Waziri kama ni chenga mnayotaka kupigwa sasa ni hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania wa hali ya chini hakuna aliye na uhitaji wa soko la kisasa la ghorofa. Tuna shida za maji na barabara. Hakuna aliye na shida ya stendi ya ghorofa. Nikuulize Mheshimiwa Waziri, nanyi wasomi hebu fanyeni research tu ndogo, ni lini mliwahi kuboresha soko halafu mkafaulu? Nakupa mfano, Soko la Machinga Complex mliboresha, leo limekuwa kichaka tu cha kulala wezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkaboresha Soko la Makumbusho, likachakaa na lenyewe mpaka mkalazimisha kuingiza daladala. Haya, tukaenda Mwanza Rock City Mall, tulifukuza watu, leo limechakaa liko vilevile. Namwomba Mheshimiwa Waziri, tubadilike. Hili suala la kutengeneza stendi za kisasa lifanyike na wafanyabiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa mfano mwingine kwa Mheshimiwa Waziri. Mimi nakaa Mwanza, kuna zaidi ya shilingi bilioni 70 tunajenga Stendi ya Nyegezi iliyokuwa inazalisha, gari zilikuwa hazijabanana tunajenga soko la mjini katikati…

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti taarifa!.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, soko la mjini katikati wanaoteseka ni wananchi.

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa!

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi hawahitaji soko, wanahitaji kukusanya hela, wamekopa mabenki, unakuja kuwahamisha unawapeleka mjini.

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa!

MWENYEKITI: Mheshimiwa Musukuma.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, acha kunipiga taarifa bwana, ngoja nizungumze.

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, aarifa!

MWENYEKITI: Mheshimiwa mwache aendelee. (Kicheko)

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mzuri uko Mwanza. Kataa haya maandiko ya kuboresha masoko. Masoko ni mapambo ya miji, watu tunataka kutengeneza miradi mikakati. Tunamwomba Mheshimiwa Waziri kama kuna kitu ambacho Serikali hii inafanya na watu wataikumbuka…

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tujengeeni reli, tujengeeni majengo mazuri, hata ukinipa taarifa…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Musukuma, subiri akupe taarifa tumsikilize. Haya, Mheshimiwa Stanslaus.

T A A R I F A

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kidogo tu napenda kumpa taarifa mzungumzaji, Mwenyekiti Mstaafu, Mheshimiwa Musukuma, Stendi ya Nyegezi gharama yake na design ni shilingi bilioni 14 peke yake na siyo shilingi bilioni 70. Nashukuru.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa taarifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema kuna miradi mitatu. Shilingi bilioni 14 Stendi ya Nyegezi, shilingi bilioni 21 soko, shilingi bilioni 20 na kitu Ilemela. Sasa hiyo ni shilingi ngapi? Nauliza hii stendi ya shilingi bilioni ya 14 ina miaka saba tu toka imefunguliwa. Wakati inafunguliwa tuliambiwa stendi mpya. Sasa hivi imekuwa kuukuu, tunajenga mpya pale pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, naomba sana tujikite kwenye matatizo ya wananchi. Hatuwezi kuwa na maandiko ya kuboresha stendi. Nami nataka niwaambie tu wale Wabunge wanaotoka kwenye maeneo ya kawaida, twende Nzega pale kwenye Stendi ya Bashe pale alipojenga, wale mnaopita pale, hizo ndizo stendi za kukusanyia hela. Hakuna mtu aliye na urafiki na stendi. Stendi ni sehemu ya kufika mtu unasafiri. Huwezi kuzunguka ghorofani, utaachwa na basi. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri tu, haya maandiko na yanakuja haraka haraka, wakati sisi tunataka kwenda kwenye uchaguzi. Kama kweli ndiyo, basi mlete pesa tujenge kwa force account, lakini haya mambo ya kuruhusu maandiko, yanatosha hayo; waliobahatisha basi, walioliwa waliwe, hakuna kuongeza tena hela. Tuchimbie maji, tutengenezee miundombinu ambayo kiukweli Watanzania wengi tunahitaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, Mheshimiwa Waziri hataachwa kusemwa, acha usemwe lakini watu tunajua kazi unayoifanya. Suala la uchaguzi, mimi natoka Kijijini na kwangu sikupitishi Jimbo zima. Nawapa mfano hawa Wapinzani, kosa kubwa mlilolifanya ni kushindwa kwenda kuelewesha watu wenu jinsi ya kujaza fomu.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mnakula bata kwenye mitandao huku, watu hawajui kujaza kule! Wanaandika CHADEMA, wala hawajui kujaza Chama chao full. Mimi nina watu kwenye Jimbo langu, ameulizwa kirefu cha ACT, hajui kuandika. Ungekuwa ni wewe na Kanuni unazo, ungefanyaje? Mmekalia ku-tweet, mitandao, nendeni kwenye Majimbo yenu mkafundishe watu wenu. Mkiendelea hivyo, hata kwenye Ubunge tunagonga mageni kama hayo. Nakushukuru. (Makofi)