Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. John Wegesa Heche

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Tarime Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii adimu ili nichangie na kwa sababu siku hizi maisha yangu yamekuwa mahakamani kwa muda mrefu, leo nimepata fursa ya kuchangia niseme machache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii nchi ni yetu sote na hata kama mtafanya kiburi na kudharau wenzenu na kufikiri mna mamlaka ambayo hayajawahi kutokea duniani hapa, hakuna jambo jipya hapa duniani. Mwaka 2016 tulijiwekea mipango kwenye kitabu hiki ambacho kina mpango wa 2016/2017 - 2020/2021 ambapo kwenye kitabu hiki ndiyo tunatohoa mpango wa mwaka mmoja mmoja ambao tunaujadili leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamezungumza sana wenzangu, nami ningependa miongoni mwa maeneo ambayo nataka nichangie ni kwenye hili eneo la ukurasa wa 11. Najua Mheshimiwa Dkt. Mpango tunakuonea sana huna mamlaka na haya mengine yanaagizwa.

Hata hivyo, kwenye mambo ambayo mliahidi kwenye malengo hapa ni kuhakikisha kuwepo kwa mgawanyo wa madaraka, kukuza demokrasia, uvumilivu wa kisiasa na kijamii. Kwa mara ya kwanza kwenye historia ya nchi hii tangu kuanza mfumo wa vyama vingi hata mwaka 1995 ambapo ndiyo introduction ya mfumo wa vyama vingi ilikuwa inaanza kwa mwanzo kabisa ambapo watu walipaswa kuwa na hofu, mambo yaliyofanyika kipindi kile hayakuwa mabaya kama yanayofanyika leo miaka 27 baada ya mfumo wa vyama vingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkuki kwa nguruwe kwa binadamu ni mchungu sana na what goes around comes around. Watu wa chini kabisa akinamama, vijana na wazee, wamekwenda kuchukua fomu za kugombea ujumbe wa Serikali ya Kijiji, Uenyekiti wa Kitongoji na Uenyekiti wa Kijiji ngazi ya chini kabisa ambapo migogoro mingi wakati mwingine inatokea huku kwenye levels za Ubunge na nini haiwagusi moja kwa moja kule chini, kule chini kuna watu wanachaguliwa siyo kwa sababu ya vyama vya kisiasa, uchaguzi wa kitongoji wakati mwingine hauangalii chama unaangalia ni nani aliyesimamishwa kwenye eneo husika na ana nguvu kiasi gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mathalani, tunaishi kitongoji kwenye kijiji chetu pale Kitagasembe kinaitwa Chelela, Kitongoji cha Chelela, baba yangu alikuwa Mtemi, alikuwa na wanawake wanane, sisi peke yetu kwenye familia ya mzee Heche tupo zaidi ya watu 90 pale; chukua vijana ambao wameoa, wameolewa pale. Kwa hiyo, ukichukua basically kile kitongoji ni watu wa ukoo mmoja tu. Leo kwa sababu mnajiona mna nguvu eti mnataka muende ku-impose mtu kuongoza watu ambao hawamtaki, anashirikiana nao vipi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na watu wazima na akili zetu tumekaa humu juzi Mkurugenzi ameita watu Chuo cha Ualimu Tarime pale wanapitia fomu, Mkurugenzi anafundisha mtendaji kufanya forgery. Maswa Wilaya nzima ya Maswa yenye Majimbo mawili watendaji wamekimbia kwa siku saba hawaingii ofisini eti watu wapiti bila kupingwa na nyie mpo humu mnaona ni kitu cha kawaida kinachofanyika kwenye nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka niwaambie, mmechukua chuki mmeipeleka mpaka kwenye level ya kitongoji na kwa sababu ya kiburi hamtaelewa haya ninayoyazungumza lakini mwanzo mzuri utaanza tu mwakani na nyie wenyewe ndani yenu na mtai-feel. Na hilo linatosha na niishie hapo lakini nataka niwaambie kwanza mmejitia aibu ambayo haijawahi kutokea…

DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. JOHN W. HECHE: Na kwa mara ya kwanza inathibitika kwamba CCM pamoja na kujifanya ni chama kikubwa…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Heche…

MHE. JOHN W. HECHE: Na ni chama chenye nguvu na ni chama ambacho…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Heche naomba usubiri taarifa, kuna taarifa.

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, please!

MWENYEKITI: Kuna taarifa, Mheshimiwa Dkt. Mollel taarifa…

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, please!

T A A R I F A

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kumpa taarifa Mheshimiwa Heche kwamba yeye hafikiri kwamba kile kikao chetu tulichokaa kwa Mheshimiwa Komu tukijadili wizi wa rasilimali za chama na tukasema hilo litatuathiri kwenye uchaguzi na uwezo wa sisi kusimamia uchaguzi kwa sababu ukiangalia hata makatibu wa CHADEMA wilaya zote na kata walishindwa kuwezeshwa ili kufika chini kuweza kuwasaidia na kusimamia utaratibu mzima wa ujazaji fomu na vitu..

MWENYEKITI: Mheshimiwa Heche naomba uendelee

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: ndio sasa madhara yake haya ambayo tulitaka kumpindua Mbowe kwa ajili hiyo wewe ukatusaliti wakati ule huwezi kufikiri?

MWENYEKITI: Mheshimiwa Heche.

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri hata anaweza kuaminika kidogo baada ya kusema hayo, sio?

MWENYEKITI: Taarifa hiyo sema wewe kwamba umepokea au hujapokea.

MHE. JOHN W. HECHE: Anaweza kuaminika kidogo baada ya kusema hayo?

MWENYEKITI: Usiniulize mimi sema wewe umepokea au hujapokea?

MHE. JOHN W. HECHE: Ndio namuuliza sasa kupitia wewe. Kwa hiyo…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Heche hiyo taarifa umepokea, hujapokea?

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, please hiyo sio taarifa, haihusiani na tunachozungumza.

MWENYEKITI: Basi endelea.

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kuna mambo ya nchi ambayo tumejiwekea malengo ya kuyatekeleza na yapo kwenye vitabu vyetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimesema mambo haya ya kihuni, mambo ya forgery, aibu mnayoyaleta na mnafundisha watendaji wa Serikali wakianza kufanya forgery kwenye mambo ya kiserikali kule chini ikiwemo kuiba pesa za wananchi, sitegemei kuona mnalalamika kwa sababu nyie wenyewe ma-DC na RC wamekaa wanafundisha watu kufanya forgery, hilo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili…

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu.

MWENYEKITI: Kuhusu utaratibu, Mheshimiwa Chief Whip.

KUHUSU UTARATIBU

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kutumia kanuni ya utaratibu lakini inayoendana na kanuni ya 64 lakini vilevile itaambatana na kanuni ya 61, nitakwenda kwenye 61(a) na nitakwenda pia kwenye kanuni ya 61(f).

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashindwa kuendelea kumvumilia Mbunge anayechangia. Mbunge anayechangia anataka kulithibitishia Bunge hili kwamba Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi huko walipo wameitisha vikao na kuwafundisha watu kufanya forgery, tuhuma hizi ni nzito na kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi tukakaa hapa ndani ya Bunge tukatoa tuhuma kubwa kama hizi kwa viongozi wenye madaraka walioaminiwa ndani ya Serikali kuwahudumia wananchi na Mbunge mmoja tu humu ndani kwa interest zake…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, anayezungumza sasa ni Mbunge mmoja sio wote…

WABUNGE FULANI: Wote

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Akaamua kujenga
tuhuma hizo nzito na tukamuacha amalize mchango huu bila kutumia kanuni hiyo ya utaratibu ndani ya Bunge, tunachokijua wote utaratibu unaongozwa na sheria na kanuni. Na kwa mtu yeyote ambaye anaona utaratibu umevunjwa na Waziri wa TAMISEMI ameshatoa maelekezo mazuri na kila mtu ana haki…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: …ya kupeleka tuhuma hizo kwa msingi wa utaratibu wa kisheria, ninamuomba Mheshimiwa Heche ama atoe uthibitisho wa hao Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi waliokuwa wamewafungia watu na kuwafundisha kufanya forgery kwa kuzingatia kwamba kwa mujibu wa sheria hao wote anaowataja wanatambulika kisheria kwenye dhana nzima ya uchaguzi huu ama afute kauli yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile, ninaendelea kukiomba kiti chako Mheshimiwa Heche atumie lugha yenye heshima ambayo haitadhalilisha watu wengine ndani ya Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba mambo haya ya utaratibu niyalete mbele yako Heche afute hiyo kauli na kama hafuti atuletee uthibitisho. (Makofi)

MWENYEKITI: Asante Mheshimiwa Chief Whip, Mheshimiwa Heche nilitegemea baada ya kuzungumza hivyo utakuwa na ushahidi hapo mkononi wa kutuonesha hayo uliyasema. Kwa vile huna ushahidi kwa hiyo naomba ufute hiyo kauli yako na usiendelee tena kutoa tuhuma nzito ambazo huna ushahidi hapo ulipo na vinginevyo nitakuzuia kuzungumza.

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, sitashangaa kama utanizuia kuzungumza na sitashangaa kama utavunja kanuni, kanuni inasema mnipe muda nithibitishe. Nimesema hapa Wilaya nzima ya Maswa watendaji siku saba, Majimbo mawili hawakuingia ofisini. Nimesema Tarime Mkurugenzi ameita watendaji baada ya kupokea fomu wamekaa nao chuo cha ualimu, naweza kuwathibitishia, give me time? Sasa ndio kanuni inavyotaka sasa unaniambia sina ushahidi una uhakika gani kwamba sina ushahidi? (Makofi)

MWENYEKITI: Hukusema kama unao, endelea haya.

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, tafadhali sana. Kwa hiyo, jambo la pili…

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa sasa umeanza usumbufu.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Heche naomba usubiri.

MHE. JOHN W. HECHE: Ndio kanuni ilivyo

MWENYEKITI: Naomba usubiri, Mheshimiwa Chief Whip taarifa.

T A A R I F A

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimetoa jambo la utaratibu, ninarudi jambo la taarifa kwa mujibu wa kanuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kumpa taarifa Mheshimiwa Heche na Wabunge wengine wote katika dhana hii ya kusimamia uchaguzi, vyama vyote vilishirikishwa, vikapewa maelekezo…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: …na vikapewa maelekezo lakini licha ya kupewa maelekezo…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Waheshimiwa naomba mtulie amalize taarifa.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: …na wewe mlokole?

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge naomba tusikilizane kila mtu atasikilizwa, Mheshimiwa Jenista naomba uendelee.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, sauti za mlango huwa hazimzuii mwenye nyumba kulala kwa hiyo hazinisumbui sauti zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninarudia kusema wapo wajumbe na wagombea, naomba nieleweke, wapo wagombea kupitia hata kwenye vyama vingine ambao walikutana na kupewa maelekezo ya kujaza fomu lakini ni hivyohivyo utaratibu wa kutoa maelekezo kwenye chaguzi zozote ni lazima msimamizi atoe semina na maelekezo kwa wasimamizi wake.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa
Mwenyekiti, ninataka hawa wanithibitishie katika vikao hivyo vya maelekezo Mheshimiwa Heche ana uhakika vikao vya maelekezo vilikuwa ni vya kufundisha forgery?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba mwongozo wangu wa utaratibu uzingatiwe na ninaomba kumpa taarifa Heche, vikao ni mahali popote katika kutoa maelekezo na sio kufundisha forgery.

MWENYEKITI: Waheshimiwa tusikilizane…

MHE. JOHN W. HECHE: Dakika saba za Mheshimiwa Heche zipo!

MWENYEKITI: Zipo dakika zako lakini urudi kwenye mpango kwa sababu huko unapokwenda Serikali za Mitaa na mambo mengineyo sio ishu muhimu kama hivyo unasema, Serikali inafanya kazi yake na hizo tuhuma ulizonazo hazina uthibitisho kwa sasa hivi huna wewe hapo ulipo. Kwa hiyo, kama unazo utaleta kwa wakati wako lakini wakati unatayarisha hizo tuhuma endelea na mpango mwingine.

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, now that’s leadership, nakushukuru sana kwa sababu wanakupa pressure anyway.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo ukurasa wa 111 kwenye hiki kitabu, kujenga demokrasia, kuimarisha uvumilivu, kujenga mihimili ya Serikali kuheshimiana sasa ndio maana Serikali wao wanafikiri wana nguvu kuliko Bunge humu, ndio kiburi wanachopata. Ukiona hayo yote ni kwa sababu wanajiamini wao labda wapo…

MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu.

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine…

MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mbatia subiri.

MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu.

KUHUSU UTARATIBU

MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ninaamini heshima ya kusikilizana ni jambo la heri sana na maandiko yanasema kujibu kabla ya kusikiliza inaweza ikawa sio nzuri kwako, nisingependa kuendelea zaidi hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo anayozungumza Mheshimiwa Heche nilitaka nimpe tu taarifa kwamba ushahidi wa hao Wakurugenzi wanayoyafanya upo hapa kwa halmashauri nzima ya Wilaya ya Moshi nina vielelezo na Waziri ana vielelezo vyote hivi tangu jana mambo gani yanayofanyika. Kwa hiyo, haya mambo ni kweli yanafanyika na sio Tarime tu kwa hivyo nimempa Heche anayechangia taarifa hiyo ili aweze kujua kwamba ni sahihi kwa ajili ya ustawi, amani na utulivu wa nchi yetu ili tuweze tukaisimamia Serikali vizuri na kuishauri Serikali vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimempa taarifa hiyo. (Makofi)

MHE. JOHN W. HECHE: Asante sana.

MWENYEKITI: Sawa kabla hujaendelea Mheshimiwa Heche, Mheshimiwa Mbatia unasema kwamba vielelezo hivyo Mheshimiwa Waziri anavyo tayari, kwa hiyo kama anavyo tayari ina maana Serikali tayari imeshajua na kuna ruling yake ambayo imeshatolewa kwa hiyo sioni kwa nini mnazungumza tena hilo tena. Kwa hiyo, Mheshimiwa Heche naomba uendelee na mengine.

MBUNGE FULANI: Serikali imekataa, mbona imekataa mbele ya…

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante napokea taarifa, nashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, kuhusu Mchuchuma na Liganga; kwenye hiki kitabu Mheshimiwa Dkt. Mpango ulituambia kwamba Serikali yenu imekusudia kuendeleza mradi wa Mchuchuma na Liganga. Huu mradi mwaka 2009 Serikali iliingia mkataba na Kampuni ya Sichuan Hong Gold ya China na tukaunda kampuni moja kati ya kampuni ya China ya kwetu ya Watanzania na Serikali. Serikali ikiwa na 20% na kampuni ya Sichuan Hong Gold ikiwa na asilimia 80, mwaka 2009.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mwaka 2010 ndio mradi huu ilikuwa uanze, tuna mashapo ya makaa ya mawe pale tani milioni 428, tuna chuma pale tani milioni 125. Ule mradi ulikuwa una investment ya dola bilioni 3, zaidi ya trilioni 6.8, in fact ndio ungekuwa mradi mkubwa kuliko miradi mingi yote ambayo imeingiwa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ule mradi ulikuwa unaleta ajira kwa Watanzania direct zaidi ya 5000 na ulikuwa unaleta indirect ajira zaidi ya 30,000. Tangu mwaka 2009, leo tunazungumza miaka 10 baadaye mradi ume-delay, hakuna kinachoendelea, tunaandikiana kila mwaka Mchuchuma na Liganga lakini Watanzania ambao mliwaahidi kwenye uchaguzi kwamba mtawapa ajira hakuna ajira mnazotoa, watoto wa watu wamemaliza shule wamerudi vijijini hawana kazi ya kufanya na nyie mnakalia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnataka Watanzania waliopo kule kwetu waliomaliza ualimu na wao waanze kuimba flyover, ndege ambayo ndege nyie wenyewe mmethibitisha kwamba mmenunua ndege kwa zaidi ya trilioni 1 na bilioni zaidi ya 500 halafu kwa miaka 3 eti imewaingizia bilioni 30.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani mmenunua ndege trilioni 1 na bilioni zaidi ya 500 miaka 3 juzi Waziri anaulizwa na Rais anasema tumeingiza dola milioni 14, bilioni 30 wa miaka 3 kwa investment ya trilioni 1. Kwa hiyo, mtachukua miaka zaidi ya 80 kupata trilioni 1 na bilioni 500 ambazo mme-invest pale. Na mnataka Watanzania wote tukae tunaimba ndege ndege. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Heche.