Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. Joram Ismael Hongoli

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kushukuru kwa kupewa nafasi ya kuchangia Mpango huu wa mwaka 2020/2021.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa namna anavyotekeleza majukumu yake. Tumeona mipango mizuri na miradi mikubwa inatekelezwa, kwa hiyo, nampongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimpongeze pia Waziri wa Fedha na Naibu Waziri wake kwa namna wanavyosimamia mapato na hata utekelezaji wa mipango mbalimbali, nawapongeza sana. Taarifa mliyoileta ni nzuri na inaeleweka, tunaiona mipango mnaisimamia vizuri na inatekelezwa vizuri naamini na hii itatekelezwa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nianze kuzungumzia upande wa kilimo hasa uwekezaji katika sekta ya kilimo. Kama taarifa inavyoeleza kwamba sekta ya kilimo ndiyo inayochangia asilimia 28.2 katika pato la Taifa lakini pia inaajiri zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania lakini ukiangalia ukuaji wake ni mdogo sana, bado uko asilimia 5.3. Sekta ambayo inaajiri watu wengi lakini bado ukuaji wake upo asilimia 3. Kwa hiyo, hapa bado tuna kazi kubwa ya kufanya. Niiombe Serikali tujitahidi kuwekeza kwenye kilimo ili tuweze kwanza kupanua ajira, lakini pia fedha za kigeni nyingi sisi kama Tanzania tunategemea sana kwenye mazao haya ya biashara lakini pia kwenye sekta ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mazao ya biashara kama chai, kahawa, korosho na mengineyo, yakisimamiwa vizuri toka mwanzoni, kwa maana ya toka kwenye uzalishaji hata kwenye uchakataji na mwisho yakatafutiwa soko zuri yana uwezo wa kuingiza fedha za kigeni nyingi sana. Kuna nchi nyingine uchumi wao unategemea tu mazao kama haya lakini wanafanya vizuri na wanapiga hatua kubwa. Kwa hiyo, niombe sana jambo hili liangaliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kenya ni nchi ya jirani tu haya mazao inayategemea sana, inauza kwa kiasi kikubwa lakini pia bei yake ipo juu ukilinganisha na Tanzania sisi bado tupo chini. Kwa mfano, kwenye zao la chai na kahawa, haya mazao yameyumba sana na ukiangalia hata usimamizi wake siyo mzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Njombe sisi tunalima chai, ukienda Lupembe hivi leo kuna chai inamwagwa yaani maana yake hakuna mnunuzi au wanakosa mnunuzi au mnunuzi hana uwezo wa kuchakata chai yote.

Kwa hiyo, unaweza ukaona namna gani tunavyopoteza fedha za kigeni kupitia hii sekta ya kilimo. Kwa hiyo, niiombe Serikali iweke usimamizi mzuri kuanzia kwenye uzalishaji, uchakataji na mwisho wa siku na soko lenyewe lisimamiwe vizuri ili tuweze kuongeza uchumi wa Taifa letu na pato kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine linalotatiza kwenye sekta ya kilimo ni miundombinu. Ukiangalia kwenye maeneo ambako uzalishaji ni mkubwa miundombinu ya barabara sio mizuri. Hivyo, usafirishaji wa mazao toka shambani kwenda viwandani na badaye kutoka viwandani kwenda masokoni unachukua muda mrefu na mwisho wa siku kuathiri ubora wa mazao haya na mwishoni unakuta kwamba hata pato lake linaathirika kwa sababu kwenye soko la dunia huwezi kushindana kwa sababu ubora wake unakuwa umepungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe kwenye upande wa miundombinu hasa barabara hizi zinazounganisha mkoa mmoja mpaka mkoa mwingine, kwa mfano Njombe pale katikati tunazalisha chai, miti, nguzo, parachichi na mazao mengine lakini shida ni kuunganisha mikoa. Kwa mfano, kwenye Jimbo langu la Lupembe barabara ile ya Kibena – Lupembe – Madeke, pale katikati kuna uzalishaji mkubwa sana, ile barabara ingekuwa ya lami tayari mazao yanayozalishwa maeneo ya Lupembe na maeneo mengine kama Mlimba kule ndani yangeweza kupelekwa sokoni na mwisho wa siku tukapata faida kubwa kupitia mazao haya yanayozalishwa pale lakini kupitia sekta ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali iongeze bajeti TARURA ili barabara zinazoenda vijijini ziweze kujengwa. TARURA wanashughulikia barabara zote zinazoenda kwenye mashamba na kwenye vijiji mbalimbali waongezewe bajeti. Hivi ilivyo sasa hivi bajeti yao ni ndogo, hawawezi kutengeneza barabara zote zinazoenda kwenye mashamba haya kwa sababu hawana fedha. Kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Dkt. Mpango katika mipango yako ile angalau kipindi hiki tujitahidi kuwaongezea TARURA fedha kwenye bajeti yao ili waweze kukamilisha jukumu zima la kutengeneza barabara kwenye maeneo ya vijijini ambako huko ndiko kuna uzalishaji mkubwa wa mazao haya ya chakula lakini pia mazao haya ya biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie pia juu ya Mradi wa Mchuchuma na Liganga. Mradi huu tumekuwa tukiusikia muda mrefu kwamba utatekelezwa. Nipongeze hatua za Serikali kwenye ukurasa wa sita wa taarifa ya Mheshimiwa Waziri lakini pia kwenye kifungu kidogo kile cha (6) inaeleza kwamba kazi ambazo zimeshatekelezwa ni pamoja na utafiti wa kina kuhusu wingi wa madini lakini pia thamani ya madini na aina ya miamba na uhakiki wa mali za wananchi watakaopisha eneo la mradi. Niipongeze sana Serikali kwa hatua ambayo mmefikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa twende mbali zaidi, twende kuhakikisha kwamba tunautengea fedha za kutosha mradi huu ili uweze kuanza kwa kuwa tukianza kuzalisha ule mkaa pale Mchuchuma utaweza kuzalisha umeme wa kutosha na umeme huu unahitajika sana. Pamoja na kwamba tunampongeza sana Rais tumeanza kukamilisha ule Mradi wa Rufiji, ni kweli ni mradi mkubwa, lakini huu mradi unategemea hali ya hewa, hali ya hewa ikibadilika tunaweza ukapata shida pia, uzalishaji wa umeme wa Rufiji unaweza ukapungua lakini kumbe tukiwa na mradi mwingine wa Mchuchuma ule unaozalisha umeme kwa kupitia makaa ya mawe haya maeneo mawili yanaweza yakasaidiana kuhakikisha kwamba viwanda vyetu na shughuli za kiuchumi katika nchi yetu zinaendelea vizuri bila kuathirika. Kwa hiyo, tusitegemee source moja, tuwe na source zote mbili. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mpango tuongeze fedha kwenye mradi huu ili uanze kutekelezwa na hatimaye umeme uanze kuzalishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia taarifa inaeleza kwamba kuna madini mengine pia yatazalishwa, kwa mfano kuna vanadium, titanium pamoja na chuma. Hizi vanadium na titanium zinatumika sana kwenye kujenga engine za magari lakini pia titanium inatumika kujenga engine za ndege, ni mradi muhimu sana. Kwa hiyo, kumbe badala ya kuagiza baadhi ya malighafi kutoka nje kwa ajili ya ujenzi wa engine tutaweza kupata malighafi hapahapa nchini. Kwa hiyo, tunaweza tukauza lakini pia tukazitumia sisi kama nchi kwa ajili ya kutengeneza engine hizi za ndege hapahapa za mwendokasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine ni juu ya elimu. Kuna shida kubwa sana kwenye upende wa walimu hasa wa shule za misingi. Shule nyingi zina uhaba wa walimu wa shule za misingi. Kwa hiyo, niombe katika Mpango wetu tujikite kuhakikisha kwamba tunaongeza idadi ya walimu watakaoajiriwa wa shule za msingi ili wasaidie kutoa elimu bora kwenye shule hizo. Pia walimu wa sekondari kwenye shule zetu bado ni wachache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri katika mipango yetu tujitahidi kuhakikisha kwamba tunaongeza idadi ya watakaokuwa wanaajiriwa kwenye shule za msingi ili watoto wetu waweze kupata elimu bora. Maana watoto kama wataenda bila walimu au walimu wanafundisha darasa kubwa la watu 100 au 80 watoto uelewa wao utakuwa ni mdogo, kuna wengine hawataelewa vizuri. Kwa hiyo, tujitahidi kuhakikisha kwamba tunaongeza idadi ya walimu hasa shule za msingi na sekondari ili watoto wetu waweze kupata elimu bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni juu ya ndege. Tumeshanunua ndege za kutosha na tunaendelea kununua, tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa jitihada zake za kununua ndege lakini bado sijaona sehemu ambayo inaelezea utaratibu wa kuongeza mafundi wa ndege. Ni kweli tumenunua ndege, je, hizi ndege tutakuwa tunaenda kutengeneza nje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali ianzishe utaratibu wa kuwa na kitengo na mafunzo maalum kwa ajili ya ma-engineer watengenezaji wa ndege ili ndege zetu baadaye tusitegemee kwenda kutengenezwa nje ya nchi, ziweze kutengenezwa hapahapa nchini. Kwa hiyo, tuanze utaratibu kama ni kuwapeleka nje kwa sababu tayari tumeshanunua Bombardier tuwapeleke huko kwenye viwanda hivyo vinavyozalisha hizo ndege na kwenye vyuo hivyo vya kutengenezea hizo ndege ili waweze kujifunza na tuwe na wataalam wetu ambao watakuwa ni mafundi wa ndege zetu. Itakuwa siyo vizuri ndege inaharibika inabidi ulete mtaalam kutoka nje au ulete fundi kutoka Marekani lakini tukiwa na mafundi wetu kwanza tutapunguza gharama za kukodi mafundi hawa lakini pia tutaongeza ujuzi na ajira kwa vijana wetu ambao wapo hapahapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nipongeze sana Serikali kwa juhudi zake za kuhakikisha kwamba inajitahidi kuboresha huduma ya usafirishaji kwa kupitia reli, hasa hii reli ya Standard Gauge. Nampongeza Waziri anaeleza kwenye taarifa yake kwamba reli ya TAZARA itaenda kuboreshwa lakini mmeanza kwanza kununua vichwa vipya saba vya treni na mitambo mbalimbali. Ni muhimu reli ile ikaboreshwa kwa sababu ukanda wa Kusini mizigo mizito yote inapita kwenye barabara lakini tukiwa na reli hizi Nyanda za Juu Kusini na nchi ya Zambia tutaweza kusafirisha mizigo mizito kwa kupitia reli hii na hatimaye barabara zetu zinazoenda Mbeya, Ruvuma na Zambia zitadumu muda mrefu kwa sababu mizigo mingi mizito sana itasafiri kupitia reli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nashukuru sana kwa nafasi. Naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)