Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana ambaye ndio Mwenyekiti wetu wa kikao kwa siku ya leo, kunipa fursa kujadili mapendekezo ya mpango wa maendeleo ya Taifa kwa mwaka 2020/2021.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikiliza michango mingi na mingi ni mizuri. Kwa sababu mpango wetu huu ni wa mwisho, mimi nitajielekeza kwenye Kitabu cha Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano ambacho Bunge lako Tukufu lilipitisha na miradi ambayo mpaka sasa haijatekelezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka wa 2016 tulipokuwa tunajadili kitabu hiki kuna miradi ya kielelezo ambayo sisi kama Taifa tulipanga itekelezwe. Katika miradi ya kielelezo, ipo ambayo tumefanikiwa kwa kiwango fulani na ipo ambayo tumeiondoa kabisa na Serikali inashindwa kuleta majibu ya msingi kulieleza Bunge lako Tukufu kwa nini tumeshindwa kuitekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi Na.1, ukisoma ukurasa wa 83, miradi ya kielelezo inayohusiana na Kanda za Maendeleo, kuna ujenzi wa Bandari Mpya ya Bagamoyo, amezungumza Mheshimiwa Mtemi Chenge hapa. Ni kwamba bandari hii, lile eneo lote lilikuwa lina uwezo wa kuongeza ajira zile zisizo rasmi na kufikia 100,000. Sasa hebu fikiria leo katika nchi ambayo wananchi wanalalamika hakuna ajira, hii bandari ambayo ilipaswa iwe tayari imetekelezwa, tangu mpango wa pili tumeanza kuuandika, mpaka leo hakuna majibu ya kutosha, Serikali inashindwa kutueleza ni kwa nini jambo hili linashindwa kutekelezeka?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni uanzishaji wa Kituo cha Biashara na Huduma Kurasini. Hii ipo kwenye Mpango ukurasa huo huo wa 83(e). Jambo hili mpaka leo halipo popote na Serikali imelipa fidia lile eneo, limekaa pale halina kazi yoyote. Maana yake tulipitisha Mpango ambao tumeshindwa kuutekeleza na leo Serikali haijatoa majibu. Mradi huu vilevile ulikuwa unaongeza ajira ambazo zinafikia walau zile zisizo za moja kwa moja pale, zaidi ya 100,000 zingeweza kupatikana kwa mradi huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uanzishwaji wa Mji wa Kilimo Mkulazi. Tuliandika kwenye Mpango huu wa Miaka Mitano na mpaka leo tunakwenda kwenye mpango wetu wa mwisho, huwezi kuona Serikali inakuja kutoa maelezo, huo mradi wetu wa ujenzi wa Mji wa Kilimo wa Mkulazi mpaka sasa tumefikia wapi na matokeo yake ni nini kulingana na mpango tulivyoupitisha?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi mwingine tulioupitisha kwenye Mpango ambao mpaka sasa hivi haujatekelezwa ni uanzishaji wa viwanda vya vipuri na kuunda magari. Hii ipo kwenye kitabu hiki cha Mpango wetu ukurasa wa 84. Mpaka leo huo mradi haujatekelezwa, hakuna viwanda vya vipuri vya kutengeneza magari hapa ambavyo vimeanzishwa; wala viwanda vya kuunda magari ambayo tulikuwa tunahitaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ya uchimbaji wa makaa ya mawe ya Liganga na Mchuchuma, hii imekuwa story. Mimi tangu nasoma sekondari miaka ya 1990 mpaka nimeingia Bungeni, sasa nafanana na akina Mheshimiwa Mkuchika sasa hivi, bado story ni ile ile ya Liganga na Mchuchuma. Mheshimiwa Mtemi Chenge amezungumza, tunashindwa kuingia mikataba ambayo inaeleweka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliweka malengo sisi kama Taifa letu; malengo na viashiria kwa ajili ya utulivu wa kufanya biashara katika Taifa letu. Kwa mfano, mwaka 2015/2016 urahisi wa kufanya biashara Tanzania ilikuwa katika nafasi ya 139 kati ya nchi 189 na malengo tuliyoweka katika mpango tulisema inapofika mwaka 2020/2021 tuwe katika nafasi ya 100. Yapo kwenye vitabu hivi, lakini unapozungumzia leo, nchi yetu iko nafasi ya 144. Lengo lilikuwa nafasi ya 100, lakini mpaka sasa tuko wa 144 kati ya nchi 190. Ni malengo tuliyojiwekea ambayo mpaka leo katika huu Mpango hayajateklezwa. Sasa unaweza…

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (UWEKEZAJI): Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Silinde kuna Taarifa.

Mheshimiwa Angella Kairuki.

T A A R I F A

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (UWEKEZAJI): Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo anapotosha. Ukiangalia kwenye nafasi ambayo Tanzania kwa sasa tumeishikilia kwa ripoti iliyotoka mwezi wa Kumi, tumetoka nafasi ya 144 kwenda nafasi ya 141. Nami nilitarajia angeweza kupongeza kwa sababu, ukiangalia siyo nchi nyingi ambazo zimeweza kupata mafanikio hayo; na hii ni hatua katika kuelekea katika maboresho makubwa kwa ajili ya kuweza kuboresha nafasi ya Tanzania katika tathmini hii ya Benki ya Dunia. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Silinde, unaipokea Taarifa hiyo?

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa hiyo Taarifa. Labda nimweleze tu. Ndiyo maana nimezungumzia Mpango. Mpango wetu tulisema tunavyozungumza leo, tuwe nafasi ya 100. Uko nafasi ya 141. Au unataka tukupongeze wakati Mpango huu tumeandika sisi wenyewe? Issue ni malengo. Tumesema mwisho wa mwaka utafanya mtihani utapata marks 90, umepata 54, unataka upongezwe. Wewe uko ume-under score. Sijui kama umenielewa! (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ndiyo upungufu wa kutokukubaliana na hali halisi. Mwaka 2010 Tanzania ndiyo ilikuwa katika nafasi bora kabisa ambayo yumewahi kufikia. Mwaka 2010 tulikuwa nafasi ya 125 ya urahisi wa kufanya biashara katika nchi 189. Kwa hiyo, tumerudi nyuma, hatuwezi kujipongeza katika vitu ambavyo hatujafanya vizuri sana. Kwa hiyo, nasi haya tumeyatoa ili Serikali iweze kuyafanyia kazi, sio ku-counter attack tu kila kitu, hamwezi kufanikiwa katika hicho kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye mapendekezo yangu ya Mpango, nini ambacho Serikali sasa inapaswa kukifanya ili kuhakikisha baadhi ya mambo wanaweza kuyafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo namba moja kama Taifa ambalo tunapaswa sana kuliwekea mkazo ni kutumia nafasi yetu ya kijiografia kuhakikisha tunatumia huu ukanda wetu, kwa maana sisi kama Tanzania tunazungukwa na nchi zaidi ya nane. Hizi nchi ndiyo tunapaswa kuzifanyia biashara kuliko hizi porojo ambazo tumekuwa tukifanya hivi sasa. Hiyo ndiyo namba moja. Nilitegemea kwenye Mpango, Serikali ingekuja na Mpango huu unaokuja watueleze ni namna gani tutafanya biashara na nchi zote zinazotuzunguka kwa kutumia Tanzania kama sehemu ambayo ndiyo itakuwa kituo kikuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nilikuwa nasoma ripoti ya wiki iliyopita, Kenya peke yake kwa kutumia bandari yao tu wamesema wamepunguza asilimia 50 ya ushuru kwa wafanyabiashara wote watakaotumia Bandari ya Mombasa. Hao Kenya, yaani wameshaweka incentives ya kuhakikisha wanatunyang’anya hata hizi biashara tunazofanya na nchi nyingine. Sasa Serikali na Mheshimiwa Dkt. Mpango hapa, nataka aieleze nchi kwamba nasi tunafanya nini kuvutia hizi nchi wanachama zinazotuzunguka kuhakikisha tunapata faida ya kuwa katika nafasi bora kabisa katika…

WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Silinde kuna Taarifa. Mheshimiwa Eng. Isack Kamwelwe.

T A A R I F A

WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa Taarifa mzungumzaji kuhusiana na uwongo ambao umetembea kwamba Bandari ya Mombasa imepunguza ushuru kwa asilimia 50. Jambo hilo halipo, ilikuwa ni uwongo, uchochezi tu wa wafanyabiashara. Bei iko pale pale kule Mombasa. Dar es Salaam ndiyo tunaendelea kupunguza bei ili tuwe na meli nyingi na ndiyo maana sasa hivi zinaanza kuingia meli kubwa za mita mpaka 300 zinazobeba ma-container mpaka 5,000. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Silinde unaipokea Taarifa hiyo?

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri huwa tukizungumza tunapowapa data huwa wanaelewa na wanafuatilia na huwa hawayatolei majibu mpaka tuwakumbushe humu ndani ya Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu hapa ni kuhakikisha tunatumia nafasi, geographical position advantage tuliyonayo kuhakikisha tunafanya kuwa incentives ya ku-promote biashara kushirikiana na nchi nyingine. Hiyo ndiyo hoja yangu kubwa. Hata kama Mheshimiwa Waziri hapa anasema ni speculation, lakini hiyo haiondoi mantiki ya kwa nini watu wamepeleka hizo speculations Kenya badala ya kuzileta hapa Tanzania, kwamba kwa kufanya biashara hapa Tanzania, maana yake unaweza ukapata hizo benefits na kuondoa hiyo migogoro inayoendelea? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, tuwe wa kweli. Nchi yetu kwa sasa bado tunashindwa kuwekeza katika mifumo ya PPP. Hii tumeieleza muda mrefu sana, nami nitaieleza kwa kifupi sana. Mheshimiwa Mtemi hapa amejaribu kuzungumzia, lakini sisi nchi yetu tukiruhusu PPP ninaamini mambo mengi makubwa yanaweza kufanikiwa kuliko tunavyofanya sasa hivi. Nami ninachokitaka hapa, PPP ielekezwe kwenye miundombinu na wala siyo kitu kingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi unapoleta sekta binafsi ikashirikiana na Serikali, ikajenga barabara kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro, Dar Express Way, muundombinu ukakaa pale, ile sifa inakwenda kwa Serikali, haiendi kwenye sekta binafsi kwa kujenga ile barabara. Ukichukua hela hizo hizo, kwa mfano reli tumeigawanya maeneo mengi, fedha hizi hizi ukachukua PPP ukajenga reli, faida ya ile reli inakwenda kwa wananchi na wala siyo kwa ile sekta binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kifupi sana, ukiangalia wenzetu wa Malaysia walipokuwa wanaanza huu mfumo wa PPP, katika phase ya kwanza waliingia mikataba ya hovyo ambavyo na wao wenyewe wanakiri, lakini pamoja na kwamba walifanya mikataba ya hovyo wakasema phase ya pili walirekebisha phase ya kwanza. Sasa sisi hapa kama uling’atwa na nyoka zamani, unasema sasa hiyo njia sisi hatutaki kuelekea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hoja yangu kwa Serikali katika huu Mpango, tujikite kuwekeza kwenye PPP katika miradi ya miundombinu. Ukijenga reli hapa hakuna mwekezaji ataondokanayo, mtu akijenga barabara hapa hata akiingia hasara hakuna mtu ataondokanayo, lakini kitu pekee ambacho nisingekubaliananacho, PPP isifanyike kwenye masuala ya service only. Yaani kwenye upande wa huduma, nchi ijitegemee yenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwa sababu sasa hivi tuna ndege, tunataka tuone sasa katika Mpango wetu hapa, service industry tunaiwekeza kwa kiwango gani katika nchi yetu? Tufanye kama wanavyofanya wenzetu wa Rwanda pale, yaani wana Conference Tourism, wana Business Tourism. Sasa hivi dunia nzima iwe ni vikao vya FIFA, iwe ni vikao vya Mabunge ya Afrika, iwe ni vikao vya Mabunge ya Dunia, wote wanakwenda Rwanda kuwekeza kwa sababu wanaona ka- nchi kao ni kadogo, hawana rasilimali za kutosha kwa hiyo, wana-promote watu kwenda Rwanda kufanya mikutano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, shirika lao la ndege linapata faida, lakini na nchi vilevile inapata mapato kwa sababu, watu wengi wanakwenda pale. Sasa hayo ndiyo mambo ambayo tulitegemea Mpango wetu uwekeze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kidogo tu cha mwisho, tumenunua Dreamliner mbili ambazo nafikiri ninyi wenyewe mmeziona. Tusingependa kuziona zinakaa pale, tunataka tuone kwenye Mpango hapa route za Kimataifa. Route kubwa ziwe zinaainisha kama ambavyo wale wote wanaopanda ndege kwenda Kimataifa ukisoma vile vitabu vyao vinakuonesha destination ambazo wanatarajia kwenda, destination za sasa. Sasa na haya tuyaone hapa ili walau hizi ndege zisiwe hasara kwa Taifa, badala yake zilete faida. Ahsante sana. (Makofi)