Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. Masoud Abdalla Salim

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mtambile

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataala aliyetujalia uzima na afya njema ya kuweza kuchangia mapendekezo ya mpango huu tulionao leo mbele yetu. Nianze na mwenendo wa viashiria vya umaskini kama ambavyo wenyewe waliotuletea Madaktari wetu mabingwa kama hivi vifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, walituambia kwamba, mapato na matumizi ya Kaya binafsi yamepungua na umaskini umepungua kutoka asilimia 9.7 hadi asilimia 8.0 kutoka mwaka 2011 – 2017. Kwa hivyo umaskini unaelekea umepungua kwa kiasi kikubwa. Hata hivyo, najiuliza umaskini huu uliopungua ni kwa kiasi gani wameangalia Watanzania hawa wanakula milo mingapi, mwaka 2011 walikuwa wanakula milo mingapi, 2012, 2013, 2014, 2015, 2016 na 2017 kama wanatembea kweli vijijini na kama wataalam hawawadanganyi umaskini hata kipindi hicho haujapungua na haujapungua kwa sababu bei za bidhaa zimekuwa zikipanda. Mwaka 2011 debe la mahindi lilikuwa Sh.5,000 mpaka 6,000; debe la mahindi mwaka 2017 lilikuwa Sh.12,000, sasa debe la mahindi limefika Sh.18,000 na kuendelea, wanasema umaskini umepungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija kwenye unga wa sembe wenyewe, mwaka 2011 bei yake ilikuwa ni ndogo kwenye Sh.700, 800 hadi 1,000 leo 2019 bei ya unga wa sembe ni aibu imefika hivi sasa hadi Sh.1,500, umasikini umepungua! Jamani wataalam wetu madaktari hebu tuambieni ukweli, waliowaambia maneno haya, utaalam huu ni akina nani hata mtuambie hivi maana sisi wengine si Madaktari kama nyie, ni watu wa kawaida tu, ni Walimu tu wa shule za sekondari, lakini tunataka watuambie kupungua kwa umaskini huu na kupanda kwa bei; sukari, 2011 kama kweli kutoka asilimia 9.7 hadi asilimia 8.0 bei ya sukari mwaka 2011, 2012, 2013 na sasa waangalie 2017 sikuambii hivi sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, wanasema kwamba mfumuko wa bei kwanza kutoka Januari 2019 hadi Septemba 2019 umetoka kwenye asilimia 2.3 hadi asilimia 3.2, wao wenyewe wamekiri kama kuna mfumuko wa bei, sijui madaktari wetu wanatuambia nini ningeomba niwashauri; kwamba bado hali ya umaskini nchini kwetu unaongezeka, wanaokula milo mitatu sasa wamepungua, kunakuwa na pasi ndefu, sasa wanasema ni pasi ndefu, wanakunywa tu chai mchana wakitoka hapo usiku kidogo, basi wanalala. Hiyo ndiyo hali halisi ilivyo, tembeeni vijijini muone hiyo ndiyo hali ya umaskini ulivyo msidanganywe na wataalam wanaoleta kwenye makaratasi, twende kwenye uhalisia mtembee vijijini muone shughuli, ni kizaa zaa, mwaka huu!

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamezungumza kwenye umaskini ule mwingine wa kipato, kwamba nao umaskini wa kipato umepungua hapa ni sawa na utaalam wao, lakini hasa waangalie hasa na hali ya umaskini inavyoongezeka kwenye Jiji la biashara tuje Dar es Salaam ambapo ndiyo linaitwa Jiji la biashara, ukienda pale Kariakoo maduka yamefungwa, mpango huu hauna jibu, hauna jibu, hautoi tija yoyote kuonesha mkakati gani ambapo wataboresha maisha ya wafanyabiashara katika Jiji la biashara la Dar es Salam, maduka pale Kariakoo yamefungwa, mpango huu hauoneshi jambo lolote, hakuna mpango hakuna mpangilio. Watuambie wana mpango gani au wana mpangilio gani wa kufufua Jiji la kibiashara la Dar es Salam. Shughuli ipo kweli! Watuambie madaktari wetu sisi ni wadogo sana kwao, wao wamesoma zaidi sisi ndiyo hivyo tena, watuambie madaktari hawasomeki, hawaeleweki waliowandikia sijui ni akina nani, shauri yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, kwenye ukurasa huu wa 43 wamezungumza habari ya utawala bora. Hasa utawala bora umo kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuna Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Ibara ya 29 na 30 yaani majukumu yake. Sasa wamezungumzia moja kwenye utawala bora, mkakati wa Serikali kuhamia Dodoma, kwani utawala bora ni hilo tu? Katiba ya Jamhuri ya Muungano inasema ukienda kwenye Ibara ya 3(1) inazungumzia Tanzania ni nchi ya kidemokrasia yenye kufuata mfumo wa vyama vingi na ni nchi ya kijamaa. Ibara ya 5(1) inazungumzia haki ya kupiga kura yaani kuchagua na kuchaguliwa hawajagusa kitu hawa Madaktari, kule kwetu wanasema tawileni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hali ya kawaida, katika hili la kupiga kura kuchagua na kuchaguliwa, tunaelekea kwenye chaguzi za Serikali za Mitaa demokrasia imeminywa, demokrasia imepuuzwa, leo ni malalamiko kila kona, vyombo vya habari kila kona ndani na nje ya nchi kwamba hali ya demokrasia Tanzania imeminywa, wagombea wote wa Upinzani wameondolewa, matatizo yamekuwa ni makubwa na kwangu mimi kama mdau wa ulinzi na usalama ambaye napenda amani na utulivu wa kweli naona hicho ni kiashiria kibaya cha ulinzi na usalama lazima niseme kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani watu kufanya madudu yao waliyoyafanya ukaondoa wagombea wa Upinzani kwenye demokrasia ya mfumo wa vyama vingi, iko ndani ya Katiba, leo ukasema na sisi tunataka amani na utulivu. Jamani, Madaktari Serikali nzima inisikie, Mheshimiwa Jafo kasema kwamba watu waendelee kupeleka pingamizi hapa na pale, imeelezwa na Mheshimiwa Mbunge mmoja hapa, kwamba hao wanaopelekewa wamekimbia hawapo.

Huu ni mfumo wa vyama vingi, kama hamtaki mfumo wa vyama vingi, futeni vyama vingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu najiuliza mambo ambayo kila siku ninyi mko kwenye redio masaa 24, mmefanya hiki, mmefanya hiki, anakuja Polepole anasema, mko peke yenu siku saba tu ambazo ni kampeni, waacheni watu wachague na kuchaguliwa, raha ya kushinda ni kushindana, msiende peke yenu muone mambo mengi mliyokwishafanya mnatutangazia wananchi watapima, lakini tunakwenda kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa, ni aibu na fedheha kubwa ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Serikali Mheshimiwa Jafo katoa tamko lake lakini pamoja na hayo hebu jamani angalieni hili, warudisheni hawa wagombea nchi hii twende kwenye amani na utulivu wa kweli lakini kilio kila kona hawa ni binadamu. Kumbe viashiria hivi vinavyofanywa najiuliza je, Serikali ya kijiji ndio inataka amani itoweke? Ni Serikali za kwenye kata au za kwenye wilaya au kuna baraza gani najiuliza mimi mwenyewe binafsi kwa sababu unapowanyima fursa watu kuchagua na kuchaguliwa hili ni tatizo ni kiashiria kibaya kwenye amani na utulivu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri wanaohusika na vyombo vya ulinzi na usalama waliomo ndani na nje ya humu ndani niwaombe sana suala hili si la kulifumbia macho ni lazima wahakikishe kwamba watoe tamko la wagombea hawa wa upinzani kurejesha kugombea, nchi hii twenda vizuri tuko katika mfumo wa vyama vingi. Ama kama sikio la kufa halisikii dawa shauri yenu mimi nishasema na kwa sababu lugha yangu hii naizungumza mnaifahamu vizuri ni Kiswahili cha kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema haya nirudie tena kwa sababu mimi binafsi ni mdau mkubwa wa ulinzi na usalama, ukataka usitake huwezi kuzungumza masuala ya ulinzi na usalama humu ndani Bungeni usimtaje Masoud. Kwa hiyo, lazima niseme kwamba dawa mfumo wa vyama vingi tuangalie viashiria ambavyo vinaweza kuleta tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie mzungumzaji huku niko peke yangu dakika zangu mlizonipa hizo nimeongea na wenzangu kwamba niendelee na shughuli, nashukuru haya sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie mpango huu pia hautojibu hamna chochote mtazungumzia habari ya jibu la milioni 50 kila kijiji umaskini utapungua wapi. Serikali iliahidi kwamba mtatoa bilioni 50 kwa kila kijiji hamna kitu, mpango hauna jibu lolote kama kweli mnataka kukuza uchumi na kupunguza umaskini mpango hauna jibu lolote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mnaposema milioni 50 kwa kila kijiji mwaka wanne huu si mngetuacha tu tukaenda kwenye vijiji tukawaambia wananchi hiyo ndio hali kumbe mnaogopa kweli mfumo wa vyama vingi, shughuli ipo mwaka huu, hakuna jibu milioni 50 kila kijiji imekufa hivi hivi waziwazi. Madaktari mngekuja mtuambie milioni 50 kila kijiji uko wapi mpango bado mnao? Mpango huu hauonyeshi mkakati wa kuboresha maendeleo ya wafanyakazi, mishahara ya wafanyakazi annual increment nyongeza hata ya kila mwaka nayo ni tatizo shaghalabagala mwaka! Mtuambie madaktari nini mmekusudia mnataka kuipeleka wapi Tanzania? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uzuri bahari kuu humu hakuna mpangilio maalum deep sea fishing ambao duniani kote tuna bahari ya kutosha, deep sea fishing humu mtueleze ukubwa wake mna maelezo kidogo tu. Uvuvi wa bahari kuu uko wapi watu wanakuja hapa na meli zao wanachukua samaki wanakwenda kuuza, sisi katika hali kama hiyo tuangalie mkakati wa kuboresha uvuvi wa bahari kuu, lakini Mheshimiwa Mpango huu haoneshi madaktari mtuambie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie na suala zima la kilimo mmegusia sehemu ndogo ya uhitaji wa masoko lakini katika mwaka uliopita wakulima wa mbaazi waliathirika sana hadi leo wakulima wa mbaazi wana wasiwasi kupata soko la uhakika kwa sababu walikuwa wanalalamika wakauza kilo ya mbaazi shilingi 200 mpaka 300 mtuambie mkakati wa Serikali wa kuboresha soko la uhakika la wakulima wa mbaazi uko wapi, mpango unaonesha mtuambie na hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri anaangalia kwelikweli kumekucha kweli katika mkakati huu mimi nafikiri mtupe majibu mazuri. Kwa sisi wengine mwezi huu unaitwa mwezi wa mfungo sita mwezi ambao Mtume Muhammad Sallallahu alayhi wa sallam tupo wataratibu wapole tukimaliza hii tena uko mbele lakini tunataka Serikali itoe majibu sahihi ituambie mkakati madhubuti na endelevu wa kuboresha masoko ya uhakika ya mazao ya kulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo machache kwa sababu nilibamizwa na mambo mengine hapa niseme hayo yanatosha lakini nisisitize suala zima la utawala bora lifanyiwe kazi isiwe bora utawala. Kama tunataka utawala bora twende kwenye utawala bora kama unataka bora utawala endeleeni kwa sababu mna nguvu. Narudia tena kusema kama kuna utawala bora kama mlivyoandika ukurasa 43 twendeni kwenye utawala bora tuwe na chaguzi ya mfumo wa vyama vingi watu wachague wachaguliwe, kama mnataka bora utawala endeleeni kwa sababu mna nguvu. Lakini hii ina athari kubwa utawala bora nyie mnataka bora utawala, tatizo ni nini kuna hofu ya nini nyie ni watu wazima humu ndani katika Bunge hili upande huu wa upinzani huu mimi ndio mtu mzima wao na ukiona mtu mzima analia kuna jambo. Kama mnataka kusikia sikieni kama hamsikii shauri yenu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, asanteni sana nashukuru. (Makofi)