Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

Hon. Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru japo kwa dakika chache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia kilimo tunazungumzia kiungo kikubwa sana ndani ya taifa. Nitapenda kuchangia vyuo vya utafiti. Hakuna maendeleo ya kilimo kama hatujapeleka fedha na vyuo vya utafiti kuwekwa kipaumbele. Naomba nishauri tu Wizara ya Kilimo, kwamba, kama hamna kipaumbele kipaumbele cha kwanza kwenye Wizara yenu iwe ni vyuo vya utafiti. Huwezi kufanya chochote kwenye kilimo bila kuweka kipaumbele kwenye utafiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vyuo vichache vya utafiti, lakini hata vilivyopo havipelekewi fedha, na hata fedha zikitengwa hazipelekwi kwa wakati. Kilimo kinachoendelea Tanzania ni kilimo cha mazoea, ukiangalia mbolea inayotumika kwenye mazao mengi wanatumia vile vidude vya visoda au vikopo vya maji. ni lini walifanya utafiti kwenye udongo kwamba kile ndicho kipimo sahihi? Ni kwa sababu ya mazoea. Hivyo, hatuwezi kuendelea bila kufanya utafiti, ni bora leo tukatenga fedha nyingi kwenye utafiti ili tuweze kuinua kilimo chetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la vituo vya rasilimali za kilimo. Lengo la kuweka vituo hivi lilikuwa ni kupeleka huduma kwa wakulima; na hivi vituo vilipaswa viwekwe kama vituo vya afya vya kila kata; lakini leo nitolee mfano mdogo tu, Mkoa wa Rukwa una kata 97 hivi vituo vipo 9, kuna kilimo hapo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la masoko; suala la masoko tumezungumza sana. Wajibu wa mkulima ni kuhakikisha analima au anzalisha kwa tija. Wakulima wetu wamejitoa lakini Serikali imeshindwa kutimiza wajibu wake kuwatafutia masoko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali, uamuzi mlioufanya kwenye korosho ni uamuzi wa dharura sana lakini kama ni uamuzi endelevu wa kutumia Benki ya Maendeleo ya Kilimo mtuambie kwamba itakuja kutumika na kwenye zao la mahindi, kwa sababu ilianza kwenye korosho na ile siyo benki ya korosho peke yake. Kwa hiyo, nashauri Serikali busara iliyotumika itumike tena, kama ilikuwa ni dharura tafuteni soko kabla ya msimu wa mavuno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la miradi ya umwagiliaji; hatuwezi kuwa na kilimo ambacho kinategemea mvua peke yake, lazima wajielekeze kwenye mabwawa ya umwagiliaji. Mengi yaliyopo mengine yamekufa, mengine yamesimama, kosa ni la nani? Serikali wana wajibu wa kupeleka fedha na mambo haya yanafanyika hivi ni kwa sababu Serikali inakosa kipaumbele; inashika pale, inashika hapa, matokeo yake kilimo chetu sijui wanakwenda kukipeleka wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Maafisa Ugani; nimefuatilia kidogo – akija Waziri atanisahisha, yaani mpaka sasa tuna upungufu wa Maafisa Ugani 20,100, hali ya kilimo itakuwaje kama Maafisa Ugani kuna upungufu huo. Nawaomba Wizara ya Kilimo kipindi wanapeleka mapendekezo yao kwa Serikali cha kwanza waombe idadi halisi ya Maafisa Ugani ambao watakwenda kutoa ushauri kwa wakulima wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kumekuwa na shida sana kwenye Wizara ya Kilimo; bei ya pembejeo haiendani na hali halisi ya bei ya mazao. Naomba nishauri kwa kuwa slogan ya Awamu ya Tano ni Serikali ya viwanda, viwanda wajenge hapa ili bei ya pembejeo ipungue, sasa hivyo viwanda watajenga viwanda gani, hivyo viwanda vitahifadhi nini kama upande wa materials wenyewe tumefeli, upande wa umwagiliaji tumeshindwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Wizara ya Kilimo iwe na vipaumbele, kipaumbele cha kwanza kabisa kiwe kuimarisha miradi ya umwagiliaji na hii itasaidia wakulima wetu. Suala pia la danadana la kutokuwalipa mawakala kwa suala la kwamba eti wanafanya utafiti; wanafanya utafiti kwa miaka mingapi? Wale wenye makosa basi wasipewe, wale ambao wanabainika hawana makosa walipwe fedha zao. Uhakiki huu pia ni kama njia mojawapo ya kutegeategea hivi, Serikali kushindwa kutimiza wajibu wake, kama fedha hakuna waseme kwamba fedha hakuna. Kuna watu wameuziwa nyumba zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala la bima za wakulima lifanyike haraka ili Serikali wajue maumivu ambayo wanayapata wakulima ili makosa wanayofanya Serikali wawe wanawajibika kwa wakulima hawa. Hili jambo liende sambamba na matamko ambayo yanatolewa. Nazungumza hivi kwa sababu, narudia tena leo kwamba tamko la Serikali lililotoka… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)