Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

Hon. Njalu Daudi Silanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Itilima

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hotuba hii ya Waziri wa Kilimo, hotuba nzuri. Nimpongeze Katibu Mkuu pamoja na timu yake ya Wakurugenzi, Wenyeviti wa Bodi zinazoshughulikia mazao yetu. Nitaanza na kutoa pongezi zangu kwa Mheshimiwa Rais kwa jinsi anavyoingilia masuala ya mazao ya biashara, Kahawa, Pamba, Tumbaku nakadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nataka kutoa ushauri kwa Mheshimiwa Waziri mwaka huu tulikutana na wewe ukasema mambo ya pembejeo ulikuwa na mashaka lakini nafurahi sana katika kitabu chako ukurasa wa 37 jinsi viuatilifu vilivyopatikana katika maeneo yetu, nasema ahsante sana. Naiomba Serikali; mwaka jana tuliazimia katika Bunge kuwa ifikapo tarehe moja Mei kila mwaka lazima msimu wa zao la pamba uwe umefunguliwa ili wananchi waweze kupata fedha katika kipindi hicho. Tulileta hiyo hoja binafsi kwa makusudi kwa kutambua maeneo tunayotoka na wananchi wetu adha wanayoipata; kuanzia mwezi wanne kunakuwa na changamoto ya uhitaji wa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri anisaidie, kuna baadhi ya maeneo hadi sasa makampuni hayajapata vibali kwa ajili ya kuingia kununua. Lakini ieleweke kwamba sisi kama nchi na kama taifa tunategemea wakubwa wetu walioko nje Duniani kule kwa ajili ya mazao yetu haya. Bila kuwa na mipango na mikakati na utaratibu litakuwa Bunge na itakuwa nchi ya kulalamika kila kukicha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninaamini tukisimama vizuri tukashirikiana kwa pamoja Waheshimiwa Wabunge, wenyeviti wa Bodi zile husika, wafanyabiashara, tutatatua changamoto tuliyonayo hii. Haya mengine Mheshimiwa Waziri mnapita katika kipindi kigumu lakini mimi ninaamini tukiweka mazingira ambayo yatakuwa rafiki tutaondokana na zana nzima ya kila mwaka lazima zao la pamba wakae wakutane kupiga kelele, tumbaku wapige kelele, kahawa wapige kelele ilhali waamuzi tuko ndani ya Bunge hili. Kwa hiyo naamini tukisimama kwa pamoja na kuweka utaratibu na tukatumia taaluma za wataalam naamini tutafanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshuhudia miaka mitatu katika Bunge lako Tukufu lakini nimeshuhudia katika mikutano ya wadau hakuna jambo lolote la maana tunaloondoka kwa kuzungumza isipokuwa ni kutimiza wajibu tu. Naiomba Serikali kupitia Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana, hebu lisimamie hili jambo ukae nalo kwa makini tuondokane na mambo ambayo hayana maana. Kinachotuletea matatizo ni kuchelewesha utekelezaji lakini dhana ni nzuri. Leo ukisoma kuhusu zao la pamba zao linaendelea kuteremka lakini hatujui hatima yake ni nini, tutaanza tena kulalamika lakini majibu tunayo sisi wenyewe Waheshimiwa Wabunge pamoja na wanaojua dhamana ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi ningeomba sana suala hili hasa kwenye pamba; nazungumzia sana kwenye pamba kwa sababu natoka kwenye pamba na nita- declare interest kwamba mimi ni mnunuzi wa pamba, najua changamoto wanazozipata wananchi. Siku mbili hizi pale Kishaku kuna watu wamekamatwa wananunua pamba shilingi 500 kwa kilo. Kwa hiyo utaona ni adha gani wananchi walivyo na shida. Ana mali yake anahitaji hela, hiyo ulichukue na ulifanyie kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Waziri, nilimsikiliza kwenye hotuba yake kwenye kipindi akielezea habari ya ushirika. Ushirika umeleta tija katika maeneo yetu kuwa na ubora wa pamba ambao ni mzuri na tunahangaika sasa, navyoona kadri tunavyokwenda tunaweza tukaanza kupata premium ambayo ilikuwa imepotea kama senti tatu na kuendelea kwa ubora tunaoendelea nao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini changamoto iliyopo lazima ushirika muendelee kuuimarisha si maneno ya kukutana kusema tumekubaliana, hapana; na Mheshimiwa Waziri nikushauri, mwaka jana tuliingia kwenye ushirika na wengine tulikuwa tuna wasiwasi nao lakini tunaanza kuona inakokwenda. Ta hivyo bado kuna vitu vinakuwa vinaongezeka kila mwaka. Ningeshauri Serikali tuwe na mfumo tunaoanza nao wa kwanza tunapata na majibu yake, si leo tukianza mwaka huu baada ya miezi mitatu unasema wakulima wote wafungue account, baada ya miezi miwili tena unakuja na ajenda nyingine; ningeomba kwa jambo hili tuwape muda watu tusiwe tukijiaribia hili tunakuja na jingine inatutia mashakani na tunaleta wasiwasi kwa watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ieleweke kwamba benki tulizonazo zina uwezo mdogo kuwafikia wananchi vijijini. Tulikuwa na benki NBC ikabadilishwa kuwa NMB kwa maana ya Rabobank ndio watakuwa washughulikiaji wakati wa kusaidia wakulima wetu; lakini maeneo mbalimbali na wilaya nyingine zilizoko humu ndani hazina benki za hizo NMB. Kwa hiyo utawezaje kupeleka fedha kijijini zaidi ya makampuni labda 10 halafu waingize kwenye account halafu yule mwananchi atoke kilomita 150 kwenda benki; mtaona hata walimu wanapoitapa ile adha ya hela zao kwenye mabenki. Kwa hiyo kutakuwa na changamoto nyingine ambayo sio rafiki kwa wakulima na kutuletea maswali yasiyokuwa na maana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali mifumo hii iendelee kusimamiwa vizuri. Pia tusimamie kupata viongozi wa ushirika wenye weledi na wenye uchungu na watu. Yako malalamiko, baadhi ya wahasibu waliochaguliwa fedha wanazolipwa hazitoshi, mtu hawezi kulipwa shilingi 80,000 na huku anasimamia mamilioni ya watu. Maana yake ni kwamba unakaribisha wizi mwingine kwenye ushirika huo husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ningeomba hao watu wanaosimamia fedha wapewe angalau posho kubwa ainayoweza kulingana na hadhi yao kama wasimamizi wa fedha za umma au za wafanyabiashara itatusaidia kuliko mtu anashinda njaa analipwa 80,000 mshahara na huku anapokea mamilioni ya fedha; unatengeneza ushawishi moja kwa moja kuibiwa fedha hizo na matokeo yake tunaanza kusema ushirika haufai; kwa hiyo niombe sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la mwisho nimpongeze Mwenyekiti wa Tume ya Ushirika kaka yangu Titus Mlengea Kamani kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya sasa aendelee zaidi kule chini kuhakikisha anasimamia vizuri.

Mheshimiwa Mwneyekiti, niwapongeza sana Bodi ya Pamba nimpongeze Dkt. Kabisa alistaafu lakini amerudi na pamba sasa imeanza kuongezeka muendelee…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)