Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

Hon. Deogratias Francis Ngalawa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ludewa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kuwa mchangiaji wa kwanza katika Wizara hi ya Kilimo. Kwanza napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Hasunga na Manaibu Mawaziri wake, Mheshimiwa Bashungwa pamoja na Mheshimiwa Mgumba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi sasa ime-target kwenda kwenye uchumi wa viwanda na uchumi wa viwanda hautaweza kuja kama kilimo chetu hakijawa ni kilimo cha ufanisi kwa sababu naamini kwamba viwanda hivi malighafi zake zitatoka kwenye kilimo. Sasa nipende tu kujua mpango mkakati wa Wizara wa ku-boost up hivi viwanda ili viweze kuimarika ukoje, kwa sababu naamini asilimia zaidi ya 75 ya wananchi wa Tanzania ni wakulima, sasa mpango upoje wa kuwainua hawa wakulima ili waweze kuhakikisha wkamba wanatengeneza malighafi za kutosha kwa ajili ya ku-boost up hivi viwanda, kwa ajili ya kuhakikisha kwamba viwanda vyetu vinasimama na kujitegemea bila kutegemea kwa kiasi kikubwa malighafi kutoka nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wetu wana uwezo wa kuhakikisha kwamba kilimo kinakuwa endelevu, lakini kitu kikubwa ambacho kinazuia hiyo, ni miundombinu ya maeneo ya uzalishaji. Maeneo ya uzalishaji miundombinu yake kufikika ni migumu sana na hii ndiyo inayopelekea wakulima wetu kupata faida kidogo. Sasa ifike mahali maeneo ya uzalishaji miundombinu yake iwe ya uhakika. Mfano, kule kwetu Ludewa; Ludewa ina uwezo wa kuilisha hii nchi kupitia mahindi lakini miundombinu yake siyo mizuri sana, barabara zetu siyo nzuri sana. Kwa hiyo niiombe sasa Serikali iboreshe miundombinu ya barabara ili iweze kuwafikia wale wakulima na tuweze kuilisha hii nchi na tuweze kutoa malighafi ya kutosha ku-support hivi viwanda ambavyo sasa tunategemea viwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kilimo kupewa kipaumbele kwa kiasi kikubwa, hivi viwanda ambavyo tunavitegemea kwamba ndiyo iwe engine ya uchumi wa hii nchi tutakuwa tunapoteza muda. Kwa hiyo, napende kusema kwamba hii miundombinu ambayo ipo lazima iboreshwe hususan barabara wakulima wetu wanapata shida sana. Mfano, katika kipindi hiki cha masika, kuna mazao ambayo yanavunwa kipindi cha masika lakini yanashindwa kutoka kwenye eneo la uzalishaji kuja sokoni. Kwa hiyo tukiweza kuhakikisha kwamba tunatengeneza miundombinu vizuri hasa ya barabara, naamini kwamba kilimo kina uwezo mkubwa wa ku-support viwanda ambavyo sisi tumejielekeza kama nchi kwenye uchumi wa hivyo viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumza kilimo, tunazungumza mbegu. Mbegu zetu nyingi siyo bora, lakini nauona mpango wa Serikali sasa wa kuhakikisha kwamba tunawaletea wakulima wetu mbegu bora ili tuweze kufanya uzalishaji mkubwa na ambao ni wenye tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kitu kingine ambacho wakulima wetu wanapata nacho shida ni suala la mbolea. Mbolea kwa kweli haziendi kwa target, hazi-meet target za wakulima. Kipindi cha ukulima mbolea hazipo, lakini wakati unaelekea kwenye maeneo ya mavuno ndiyo zinakuja mbolea za kupandia. Kwa hiyo kuna haja sasa Serikali ikajipanga mbolea ziende katika kipindi husika. Kama ni mbolea ya kupandia basi iende katika kipindi cha kupandia, kama ni mbolea ya kukuzia iende kwenye kipindi cha kukuzia. Hilo litaleta tija kwa wakulima na pia Serikali itapata faida kwa kupitia kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wetu wana tatizo kubwa la soko. Tumeona mwaka jana wakulima wetu walikuwa na mazao mengi, walizalisha kwa kilimo kikubwa hususani mahindi. Mahindi kwetu kule Ludewa ni zao la biashara si zao la kilimo, kwa hiyo tunapozungumza mahindi kama zao la biashara kulikuwa na kuna haja sasa ya Serikali kuja na mpango mkakati wa kuhakikisha kwamba tunapata soko la kutosha ili kuwahamasisha wakulima wetu kulima kwa bidii na kwa tija, la sivyo tukitegemea tu soko moja la NFRA halitoshi. Kwa hiyo nchi ijipange sasa kutafuta masoko ya mazao ya mahindi na mazao mengine yote ya chakula ili wakulima wetu walime kwa tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukizungumzia kama nchi tunalo gap kubwa, tunalo gap la mafuta ya kula, sasa sijajua kama nchi tumejipangaje. Ifike mahali sasa tuweke kilimo kwa zone kwa sababu tunategemea mafuta kutoka nje wakati wakulima wetu wana uwezo wa kufanya hivyo vitu. Sasa ni nini mpango wa Serikali wa kuhakikisha kwamba tunaliziba hilo pengo kuhakikisha kwamba mafuta tutayotegemea yatoke hapa nchini na ikiwezekana mafuta hayo tuweze kuuza nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna tatizo la mbolea. Kama nchi tumejipangaje kuwa na viwanda vyetu wenyewe vya mbolea badala kutegemea mbolea kutoka nje. Kwa hiyo mimi niseme tu, uchumi wetu wa viwanda utategemea kwa kiasi kikubwa kilimo na kilimo ni lazima tukipe kipaumbele kikubwa. Tukizungumzia viwanda usisahau kiwanda cha chuma kule Liganga na usisisahau makaa ya mawe Mchuchuma. Viwanda hivi ndivyo viwanda flagship ambavyo vina uwezo wa kuzaa viwanda vingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kuna kila haja ya kuhakikisha kwamba kilimo chetu kiwe ni kilimo cha uhakika, tuondoke kwenye kilimo cha kutegemea mvua twende kwenye kilimo cha umwagiliaji. Hii nchi ina mabwawa mengi, hii nchi ina mito mingi, kwa hiyo twende kwenye kilimo cha uhakika ili hatimaye wakulima wetu walime kwa tija na waone faida ya wao kuwa wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo Benki ya Kilimo, iko Dar es Salaam. Mimi ningependekeza kuwa hii Benki ya Kilimo ije Ludewa ambako wakulima ndipo wapo. Benki ya Kilimo kukaa Dar es Salaam mtu wa Ludewa aende Dar es Salaam kwenda kukopa mkopo; kwanza hata hiyo elimu ya mkopo hana. Kwa hiyo Benki hizi ambazo zinawa-target wazalishaji ziende kwa wazalishaji wenyewe ili hatimaye tuione hiyo tija. Kwa sababu leo hii unaponzungumza hapa kwenye taarifa unaiona kabisa Benki ni ya kilimo sawa lakini wakopaji wakubwa si wakulima. Kwa hiyo ifike mahali sasa kila kitu ambacho tunakilenga basi tukipe kipaumbele ili hatimaye tuone kwamba wakulima wetu wanaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo bado niendelee kusisitiza kwa Serikali kuhusu masoko ya mazao, bado ni machache. Na pia tuzungumzie suala la wale walio supply mbolea. Lipo hili ombi ambalo linaonekana kwamba walio supply mbolea walio wengi walighushi; lakini mimi ninaamini kwamba wapo walio supply mbolea hawakuwa na shida yoyote. Kwa hiyo wale ambao hawakuwa na shida yoyote walipwe sasa, kwa sababu tunasumbuliwa sana, kwa sababu hatusemi sasa ni nani ambaye ameghushi, ni nani ambaye amekuwa ni fisadi kwenye huo mfumo. Wale ambao wanaonekana wapo clean walipwe fedha zao, kwa sababu tunao watu wengi wako stranded sasa hivi huu ni mwaka wa tatu wanasubiri malipo. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri hebu jaribu kuliona hilo ili mwisho wa siku hawa watu waweze kukopa.

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Ngalawa.

MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na ninaunga mkono hoja. (Makofi)