Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Richard Mganga Ndassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumve

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa nafasi hii kwa kuwa mchangiaji wa kwanza katika hotuba ya Waziri wa Ulinzi. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri pamoja na wataalam wote wa Wizara hii, mimi naomba nikuombe pamoja na wenzetu, lakini kwa Wabunge wote haipendezi hata kidogo kuzungumzia kuhusu posho, maslahi ya wanajeshi wetu humu ndani kwa kufanya hivyo kwa sababu hawa nao ni wafanyakazi pamoja na kazi nzuri wanazofanya lakini bado tuna Jeshi la Polisi, tuna Jeshi la Magereza lakini bado kuna wafanyakazi wengine tunapo- side kwamba eti hawa waongezewe posho ni kuwagombanisha hawa wanajeshi na Serikali yao.

Niwaombe sana ndugu zangu tusijipendekeze kwa kusema humu ndani eti waongezewe posho naomba sana. Jeshi hili lina utaratibu wake kuhusu maslahi, Jeshi hili lina utaratibu wake namna ya upandishwaji vyeo, hawapandishwi hivi hivi, tuwaachie wenyewe wafanye kufuatana na utaratibu wa kwao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo niseme tu kwamba Mheshimiwa Waziri kwasababu ya kazi nzuri sana inayofanywa na Wizara hii kupitia Jeshi letu, kupitia CDF na JKT wanafanyakazi nzuri sana niwape tu assurance kwamba bajeti hii itapita bila matatizo ili muende mkafanye kazi ya kulinda nchi yetu ndani na nje.

Mimi nina maombi mawili; la kwanza ni ushauri lakini pili ni ombi. Ombi langu la kwanza Mheshimiwa Waziri tulipokuwa pale Mlale nilitoa ombi mbele ya Amiri Jeshi Mkuu, mbele ya CDF, lakini na Mkuu wa JKT, nilisema hivi Kanda ya Ziwa kwa maana ya Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Geita, Chato na Singida hakuna Kambi ya JKT na hili ni suala la kisera Mheshimiwa Waziri. Tunaomba sana tunaomba sana Kanda hiyo siyo kwamba imesahaulika hapana, nafikiri ni utaratibu na muda ulikuwa bado haujafika nikuombe sasa Mheshimiwa Waziri kwa Kanda hii ya Ziwa hebu tupate Kambi ya JKT. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Kwimba, Tarafa ya Mwamashimba tunalo eneo la ekari 3750 nina uhakika eneo lile kwa sababu halitumiki kwa sasa, halitumiki vizuri eneo lile najua litatosha kwa ajili ya Kambi yetu ya JKT. Vijana hawa watakaokwenda pale mbali na Kambi najua watafanyakazi ya kilimo, ufugaji kwa kufanya hivyo watapata ajira kupitia ufugaji na kilimo. Niombe sana Mheshimiwa Waziri hili ulibebe kwa sababu nililisema siku ile na leo narudia tena kusema mbele ya viongozi wakuu, hebu mlibebe hili kwasababu Kanda yetu ya Ziwa kwa kweli haina Kambi ya JKT na nikuombe Mheshimiwa Waziri kama nilivyoomba pale Kwimba Mwamashimba tunalo eneo la ekari 3750. (Makofi)

La pili hili ni ushauri, vijana waliopitia JKT wanasifa kuu kadhaa ni wakakamavu, ni wachapakazi, ni wazalendo, ni watu wanaojituma, ni watu wenye nidhamu na wavumilivu sasa vijana hawa Mheshimiwa Waziri, kwa mwaka 2001 tuliporudisha JKT mpaka 2014 vijana walioenda JKT walikuwa 104,594. Walipomaliza walioajiriwa/waliopata ajira ni asilimia 24 tu kati ya vijana 104,594. Sasa nikuombe Mheshimiwa Waziri hawa vijana hawa wanafundishwa namna ya kutumia silaha za moto kundi kubwa hili la watu/la vijana karibu 76,000 linaenda vijijini, wakija wale ndugu zetu wa nchi zinazotuzunguka wakawashawishi kwa sababu hawana kazi, lakini wamejifunza namna ya kutumia silaha kwa njia moja, sitaki ..., wanaweza kushawishika, lakini nikuombe Mheshimiwa Waziri wanaweza wakashawishika kwenda kujiunga na makundi mengine yaliyoko nje.

Sasa ombi langu tunayo maeneo mazuri ya kilimo, madini, uvuvi, mifugo hebu hawa vijana hawa kwa sababu ni wataalam hebu tuwachukue tuwapeleke kwenye maeneo ya kilimo, mifugo na uvuvi. Kwa mfano ukichukua vijana ukawapeleka Kanda ya Ziwa ile kanda yote ile ni ya uvuvi, ukiwapeleka kule watafanyakazi ya kuvua pamoja na kuchakata samaki. Ukiwapeleka maeneo ya mifugo pale Mpwapwa na maeneo mengine watafanya kazi ya kufuga lakini pamoja na kuchakata mazao ya mifugo, hili ni jambo ambalo kuliko kuwaacha tu hawa vijana hawa ambao ni wengi kila mwaka tunawazalisha, niombe sana Mheshimiwa Waziri vijana hawa wa JKT tunaweza tukawapeleka wakafanyakazi nzuri zaidi kuliko kusubiri ajira, lakini wanaweza wakajiajiri wao wenyewe kutegemea na mafunzo wanayoyapata. Ajira haziwezi kutosha sijui kwenye Mashirika ya Umma wala sio Serikalini, lakini bado wanaweza wakajiajiri kwa kazi ya kulima, kufuga, uvuvi na kwenye madini. Huo ndiyo ulikuwa ushauri wangu.