Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

Hon. Joram Ismael Hongoli

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uamuzi wake wa dhati wa kutekeleza Sera ya Tanzania ya Viwanda. Mara baada ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 viwanda nchini vimeendelea kuongezeka kwa kasi kubwa na vya zamani vimeendelea kufufuliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara na Naibu Waziri kwa kazi kubwa wanazozifanya usiku na mchana. Mwenyezi Mungu aendelee kuwajalia afya njema katika kusimamia utekelezaji wa Sera ya Tanzania ya Viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya Waziri na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara ni kutengeneza mazingira ya watu wanaotaka kuwekeza kwenye viwanda na biashara nchini. Kazi hiyo inaendelea vizuri na kwa weledi mkubwa. Wawekezaji wengi wa nje na ndani ya nchi wanapenda sana kuwekeza nchini lakini kuna shida ya usumbufu wa kupata vibali mbalimbali vya kuanzisha viwanda na biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Wizara ione umuhimu wa kuunganisha baadhi ya vibali au kodi. Pia vibali au kodi hizo zilipwe kupitia ofisi moja. Mfano wa kodi au vibali hivyo ni kama vile TFDA, NEMC, OSHA na kadhalika. Mwekezaji anapoenda kutafuta vibali hivi avipate kwenye ofisi moja. Tuwe na jengo moja la uwekezaji na biashara. Hali iliyopo sasa imewakatisha tamaa wawekezaji na wafanyabiashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sera ya Ubinafsishaji nchini ilitekelezwa kwa shinikizo la Mataifa ya kibepari. Hivyo Tanzania ilitekeleza sera hiyo bila kuwa na uzoefu wa kutosha. Zoezi zima la ubinafsishaji halikufanyika kwa umakini na usahihi uliohitajika. Matokeo yake kuna mali za Vyama vya Ushirika ziliuzwa kwa wafanyabiashara bila hata kushirikisha Wanaushirika. Pia kuna maeneo viongozi wachache waliuza mali hizo bila ya vielelezo. Mfano fedha zilizopatikana hazijulikani zilirejea kwenye akaunti ipi?

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mzuri ni Kiwanda cha Chai cha Lupembe. Kiwanda hiki kilikuwa ni kiwanda chenye umiliki wa asilimia 100 ya wakulima wa chai kupitia ushirika wao wa MVYUULU. Baadaye miaka ya 1970 Serikali ilipewa kuendesha kiwanda hiki lakini baadaye Serikali ambayo ilipewa jukumu la kukiendesha tu, ikamwuzia mwekezaji bila kufuata taratibu na kusababisha mgogoro ambao una miaka 12. Ushauri wangu ni kwamba ni vizuri Serikali ikatatue migogoro kama hii mapema ili viwanda hivi viendelee kuzalisha kwa tija kuliko ilivyo sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa Liganga na Mchuchuma ni muhimu sana kwa maendeleo ya viwanda nchini. Mradi wa Liganga ukikamilika tutatatua tatizo la kuagiza chuma nje ya nchi. Tutapata fedha za kigeni na chuma tutapata kwa bei rahisi. Nchi ya Ujerumani ilifanya mapinduzi makubwa ya viwanda miaka ya 1870 baada ya kuanza kuzalisha chuma na makaa ya mawe. Pia uwepo wa makaa ya mawe Mchuchuma utasaidia kupata nishati ya kutosha na ya bei nafuu. Hivyo mradi huu ni wa muhimu kwa maendeleo ya viwanda nchini. Ni vizuri Serikali ikaona umuhimu wa kuutengea fedha za kutosha na uweze kuanza mapema.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa Bagamoyo SEZ kama ilivyoelezwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira ni wa muhimu katika kufungua fursa za kiuchumi. Pamoja na umuhimu wake, ni muhimu sana kupitia mikataba tutakayoifunga na mwekezaji isije ikatokea kama ilivyo kwenye nchi za Zambia, Sri Lanka, Eritrea na Namibia. Hivi sasa nchi hizo zimejikuta ardhi yao inamilikiwa na China. Mikataba mibovu itatuingiza kwenye Ukoloni Mamboleo. Naishauri Serikali tuendelee kupitia kwa umakini mikataba tunayotarajia kuifunga na wawekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda vidogo vidogo (SIDO). Viwanda hivi ni vya muhimu sana kwa maendeleo ya viwanda na ukuaji wa uchumi wa nchi. Viwanda hivi ndivyo vinavyoajiri watu wengi nchini. Serikali ione umuhimu wa kuongeza bajeti. Nchi zote zilizoendelea duniani zilianza na kuimarisha viwanda vidogo vidogo. Naishauri Serikali iweke utaratibu wa kutoa mikopo kwa watu au vikundi vyenye nia ya kuanzisha viwanda vidogo vidogo ili mazao yanayozalishwa yaweze kuongeza thamani kupitia viwanda hivi vya SIDO.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchukua fursa hii kuunga mkono hoja.