Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

Hon. Dr. Godwin Oloyce Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Siha

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutambua na kuelewa vizuri ni namna gani ambavyo tunaweza tukaifikia Tanzania ya viwanda, lakini bila kusahau viongozi wa Wizara. Hata hivyo, napenda kuwakumbusha kwamba pamoja na kwamba kuna juhudi nzuri sana ambazo Wizara inafanya, lakini Rais anafanya tusipuuze sana malalamiko haya ambayo yanasemwa na Wabunge, lakini kuna mambo yanayotokea chini kwa watendaji ambayo tunatakiwa kukiri na kujaribu kuyafanyia kazi kama ambavyo Wizara ya Maji imekiri na ipo tayari kufuata chini ili kuweka mambo sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kusema kwamba tunajua kwamba ukisema unatengeneza kiwanda, huna namna ya kuwa na kiwanda wakati bei ya umeme ipo juu. Leo katika Tanzania hii umeme tunanunua unit kwa maana ya dola senti 10, lakini Uingereza ni 0.12 ya senti, maana yake huwezi ukajenga kiwanda cha nguo hapa Tanzania kwa umeme wa namna hiyo kwa standard ya nguo iliyotengenezwa Uingereza ukauza soko la nje. Kwa maana hiyo, hakuna namna yoyote mtu anaweza akawekeza kwenye kiwanda cha nguo ndani ya Tanzania. Rais wetu amelijua hilo, amewekeza kwenye Stiegler’s Gorge.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, utaona na watu wanasema Wizara hii ni Wizara mtambuka; uwekezaji unaofanyika kwenye Wizara ya Miundombinu, Wizara ya Afya na Wizara ya Elimu, yote mwisho wa siku unaenda kuonekana kwenye kuboresha hii Sera ya Viwanda na kuboresha kwenye eneo la viwanda. Kwa mfano, ukienda kwenye afya tunaposema tunaboresha afya na kupeleka hela kwenye afya, maana yake tunaenda kuboresha siyo afya tu kwa maana ya watu kutibiwa lakini tunaenda kuwaboreshea huduma akinamama na mwisho wa siku watazaliwa watoto wazuri tutafanya lishe, tutaendelea na tutapata watoto wenye akili nzuri kwa sababu kwenye viwanda siyo tu suala linalosaidia viwanda ni kwamba kuleta teknolojia kutoka nje, innovation na ugunduzi ni vitu ambavyo vinasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, utakuta leo SIDO yetu wana-copy vitu kutoka nje lakini hawawezi kwenda zaidi ya hiyo ku-copy kutoka nje. Rais anapowekeza kwenye eneo la afya maana yake generation inayokuja mbele tutaweza pamoja na ku-copy lakini na sisi tutaweza kugundua na tutaweza ku-compete kwenye soko la uwekezaji na ugunduzi na hasa viwanda sasa vitaanza kuonekana vina tija kwenye Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kwenye elimu; leo kwenye elimu tunawekeza kwenye VETA. Leo tumeambiwa tunajenga Vyuo vya VETA zaidi ya 26 mwaka huu, hii maana yake ni input ya Serikali kwenye kuwekeza kwenye viwanda, mwisho wa siku zile pesa zilizokwenda kule zinarudi kuingia kwenye viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile utaona watu wanazungumzia bandari; mimi niseme kwamba Rais Kikwete yupo vizuri sana, alianza huo mradi lakini akaona kidogo kuna shida akasema Morogoro walisema mimi ni mpole mpole lakini naenda kuwaletea chuma, mkali zaidi na mzalendo. Ametuletea mwisho wa siku akamkabidhi faili akamwambia hebu chunguza vizuri hata Stiegler’s Gorge akamkabidhi yote. Rais akaangalia akahakikisha uwekezaji utakaowekezwa kwenye Stiegler’s una manufaa kwa Taifa akaupitisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, akaenda Bagamoyo akaangalia akasema hatuna bandari ambayo tunaiuza Tanzania, tuna bandari ambayo tunataka kuwekeza. Akapiga breki yule mzalendo akasema ngoja nitulie niweke na wakati huo akichukua ushauri kutoka Spika na watu wengine namna nzuri ambayo tutawekeza kwenye bandari zetu zote kuanzia Mtwara mpaka Bagamoyo na tutaelekea mpaka Tanga na hatutaki mtu atakayekuja ku-dictate terms hapa ni namna gani tunaendesha hili Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilihama nikaja upande huu na kauli mbiu yangu ya kwanza nilisema naenda kuungana na wazalendo ambao watalinda rasilimali za Taifa hili. Tumekuja kuungana na mtu ambaye ningekuwa ni profesa wa chuo kikuu, Rais Dkt. John Pombe Magufuli ningempa Ph.D ya heshima ya sheria ya kuwa profesa wa uchumi na uongozi. Ameanzisha mambo mengi, wengi walikuja hapa wakifikiri haiwezekani, imethibitika inawezekana; Dodoma leo tupo hapa na jiji linakua. Ameanzisha Stiegler’s, watu waliogopa na inaenda, na amesoma chemistry lakini amefanya mambo ya uchumi ya kustaajabisha, ndiyo maana mimi leo nasema nashukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata ukiangalia China, China ambayo leo imeendelea vizuri, kabla ya kufungua mipaka kuingia kwenye foreign direct investment walifunga mipaka wakajihakikishia kwamba wana nguvu ya kutosha ya negotiation na wana nguvu ya ndani, ndipo sasa wakafungua mipaka na wanaenda kizalendo na ndiyo maana leo Marekani na China wanabishiana kwenye masuala ya biashara na… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)