Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

Hon. Ali Salim Khamis

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mwanakwerekwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

MHE. ALI SALIM KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia siku hi ya leo kuwa na afya njema na kusaidia kutoa michango yetu kwa ajili ya Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli ulio wazi kwamba suala la biashara limeingia katika matatizo makubwa na mimi nina mambo kama matatu tu hivi ambayo nitayazungumzia leo. La kwanza; kuonesha kwamba biashara ina utata ni kwamba nchi imetengeneza dheria hata bidhaa zake zinazotoka ndani ya nchi nazo zinalipiwa ushuru kama bidhaa ambazo zinatoka nchi za nje, kwa kweli hili ni jambo la ajabu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, kule Zanzibar tuna Kiwanda cha Maziwa kikubwa tu ambacho kinazalisha maziwa ya kutosha, lakini leo maziwa yale yakitoka Zanzibar kuja bara yanatakiwa yalipe ushuru kama maziwa ambayo yametoka nchi za nje, hili ni jambo la aibu sana na la ajabu sana. Kibaya zaidi, TRA inaonekana kwamba kuna jambo maalum hapa linaendelea kuhusu Zanzibar kwa sababu baada ya Wazanzibari kulalamikia huu ushuru, TRA imempa fursa mwekezaji Said Salim Bakhresa kumwondolea VAT ya asilimia 87 ili kiwanda kile kihame kutoka Zanzibar na kije kijengwe bara ili aweze kufanya biashara zake. Hili kwa kweli ni jambo la aibu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atuambie shida hapa hasa ni nini. Maana yake ikiwa leo anajiwekea vikwazo yeye mwenyewe ndani ya nchi, atashindanaje na Rwanda, Kenya na Burundi, atashindana nao vipi, ikiwa ndani ya nchi yake mwenyewe amejiwekea vikwazo yaani biashara zisiende, hawa walioko nje ya nchi hii anashindana nao vipi? Kwa hiyo naomba Mheshimiwa Waziri akija hapa atuambie kuhusu jambo hili linakaakaaje na matatizo haya yanaondoka.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, Mheshimiwa Waziri ni shahidi; mimi na Mheshimiwa Waziri Kakunda tulikwenda kwenye semina moja na semina hiyo inahusiana na masuala ya wajasiriamali pamoja na wafanyabiashara. Mwenyewe alikiri katika semina ile kwamba wafanyabiashara kwa mfano walioko mpakani baina ya Tanzania na Uganda wamehama wale wenye biashara zao kutoka Tanzania wote wamehamia Uganda, kwa sababu Uganda akishakata leseni yake ya kufanyia biashara hana bughudha nyingine anafanya biashara zake kwa utulivu, bila shida yoyote. Sasa leo ikiwa imefika mahali Watanzania wanaacha nchi yao wanakwenda kufanya biashara sehemu nyingine kutokana tu na vikwazo vya biashara ndani ya nchi hii, kwa kweli hili ni jambo la kusikitisha sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano mmoja; leo ukitaka kwenda kuwekeza UAE, UAE sharti lao kubwa ambalo wanalo lazima upate raia wa ile nchi akudhamini ndiyo uweze kufungua kampuni au kuanzisha biashara. Ukishafanya hivyo, basi wewe process zake hata wiki haifiki, umesajili ampuni yako, unafanya biashara zako na inakupa citizenship ya watu watatu ambao umetokanao ulikotoka ili wasimamie shughuli zako kufanya kazi zao katika nchi ya UAE. Leo ndani ya nchi yetu hii tumeporomoka mpaka tumefika watu wa 147 katika nchi 190. Hivi sasa Mheshimiwa Waziri nimwambie tu kwamba sasa hivi baadhi ya wawekezaji wanaangalia fursa kufanya biashara zao ama uwekezaji wao katika nchi ya Burundi, nchi ambayo inaonekana kwamba haiko tulivu katika masuala ya kisiasa, leo wawekezaji wanafikiria wakawekeze huko Burundi kulikoni kuja kuwekeza Tanzania hapa! Kwa kweli hili ni jambo la aibu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri akija hapa atuambie shida hasa ni nini? Tumsaidie kitu gani ili haya matatizo yatatuke?

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu, kule Kilwa Masoko waliambiwa wananchi wa kule kwamba watayarishe eneo ili waweze kujenga Kiwanda cha Mbolea. Eneo tayari limetayarishwa lakini mpaka leo hii hakuna jambo lolote ambalo limefanyika na watu wameondolewa katika maeneo yao kusubiri ili kiwanda cha mbolea kijengwe ili kuimarisha uchumi huo wa viwanda kupitia wakulima wetu ambao wanalima kule katika eneo la Kusini, sasa shida ni nini? Mheshimiwa Waziri akija hapa atuambie tatizo ni nini hasa ambalo mpaka leo linakwaza mambo haya? Kila kona ya nchi hii kuna shida ya suala la biashara na viwanda. Hebu akija hapa Mheshimiwa Waziri atuambie jambo ambalo linamkwaza ambalo mpaka hivi leo linamfanya asifanye kazi zake vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, kwa nini Mheshimiwa Waziri mpaka toka alipoteuliwa kuwa Waziri hajawaita wafanyabiashara akakaa nao akawasikiliza, shida iko wapi ili akaona kwamba ni taasisi gani ambayo inakwamisha au kuna ugumu mahali gani halafu tukatafuta njia ya kutokea hapa, lakini leo anakuja analeta bajeti hii ili ikishapitishwa hapa ndiyo imetoka matatizo ya nchi yanabaki kama yalivyo. Sasa Mheshimiwa Waziri akija hapa naomba atupatie ufumbuzi wa masuala haya ili Bunge lione ni namna gani bora kusadia nchi hii iweze kutoka katika masuala haya yenye mkwamo huu wa biashara pamoja na viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli sasa hivi ukija kwenye suala la biashara, hii dhana ya biashara kule Zanzibar yaani kama kuna njama za makusudi hivi kuiua biashara Zanzibar isifanyike. Sasa tunaomba Mheshimiwa Waziri ndiyo maana hapa kunaingia masuala mengi ya kuona kuna matatizo gani katika masuala ya Muungano ili yaweze kutatuliwa haya biashara zifanyike kwa uhuru…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana, kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa.

MHE. ALI SALIM KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.