Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

Hon. Hawa Abdulrahiman Ghasia

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mtwara Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa juhudi kubwa sana anazozifanya katika kuhakikisha kwamba tunaingia katika uchumi wa viwanda na tunakua kibiashara na tunaweka mazingira mazuri ya biashara. Niiombe Wizara ya Viwanda na Biashara na Serikali kwa ujumla, tupunguze muda wa majadiliano pale ambapo tunapata wawekezaji katika miradi yetu mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti wakati napitia wakati napitia kitabu cha hotuba ya bajeti malengo ya karibu kila idara, nilikuwa naangalia NDC, kila unapoangalia ni kuendelea na majadiliano. Nimechanganyikiwa zaidi pale ambapo nimekuja kuangalia Mradi wa Liganga na Mchuchuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya bajeti ya mwaka jana walikuwa wameshafika eneo nzuri kabisa ambako mwaka huu nilikuwa na matumaini kwamba labda mradi tungeambiwa sasa hivi unakaribia kutekelezwa. Nilichokiona katika kitabu cha hotuba ni kwamba baada ya kuwa tumepitisha ile Sheria ya Kulinda Maliasili zetu inayonyesha majadiliano ya Liganga na Mchuchuma yameanza upya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunaenda mbele, tunarudi nyuma. Kwa kweli inasikitisha sana, kama majadiliano haya yangekuwa yamekwisha kwa wakati, nina uhakika kabisa SGR hii inayojengwa tungejenga kwa kutumia chuma cha Liganga na Mchuchuma badala ya chuma ya kutoka Japan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao Mradi wa Reli kutoka Mtwara kwenda Mbambabay na matawi kwenda Liganga na Mchuchuma. Wawekezaji wengi sana wameonyesha nia ya kujenga reli hii kwa njia ya PPP lakini wote wanavutiwa na makaa ya mawe na chuma iliyoko Liganga na Mchuchuma. Kama majadiliano hayataisha watafanya wale ambao wanahamu ya kujenga reli hii waondoshe ile hamu yao kwa sababu kila siku ni kujandiliana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, NDC watuambie wamekwama wapi kwenye Mradi wa Liganga na Mchuchuma. Mimi nakusudia kutoa shilingi kwa sababu mradi huu ukiendelea ndiyo utaifanya Bandari ya Mtwara ifanye kazi vizuri zaidi na hata Mji wa Mtwara uwe wa viwanda kwa sababu hiyo chuma na makaa ya mawe yatawezesha SEZ au EPZA ya Mtwara kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, majadiliano yanaendelea ya Kiwanda cha Mbolea kule Msanga Mkuu, huu unaingia zaidi ya mwaka wa sita majadiliano yanaendelea. Mimi napenda kujua au Waziri wa Viwanda na Biashara au Waziri wa Fedha wakija watuambie hivi wenzetu Rwanda wao wanajadiliana kwa kwa stahili ipi ambapo anaweza akaja mwekezaji ndani ya siku tatu wameshamaliza kujandiliana, wameshakubaliana, wameshasaini mikataba na sisi haswa hicho tunachokwama ni kitu gani? Au hao wanaojadiliana wanalipwa vizuri sana, kwa hiyo, majadiliano wamefanya ni sehemu ya maisha? Hebu tuangalie suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie eneo la biashara, siyo siri sasa hivi Kariakoo kumekufa. Kariako ilikuwa inapokea wafanyabiashara kutoka Congo, Zambia, Malawi, Zimbambwe mpaka Uganda, sasa hivi Watanzania tunaenda Uganda kununua bidhaa ambazo zimepita katika bandari yetu. Niiombe Serikali iangalie kuna nini kinachoua Kariakoo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo siri ukienda Kariakoo maduka mengi yamefungwa na hata ukitaka banda leo Kariakoo unapata wakati zamani kupata banda Kariakoo ilikuwa ni shida. Sasa kama Serikali tujiulize ni nini kimewakimbiza majirani zetu kuja kufanya biashara Kariakoo kwa sababu Karikaoo ilikuwa ndiyo Dubai ya Afrika Mashariki na Afrika ya Kati. Ni kitu gani sasa kinachowafanya watu waende Uganda wakimbie Kariakoo? Namuomba Waziri wa Viwanda na Biashara alifanyie kazi suala hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine ni vizuri tu Serikali ikapokea ushauri kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge. Kama tutakumbuka wakati tunapitisha Sheria ya Manunuzi, Kamati ya Bajeti ilikuja na mapendekezo ya kuweka kipengele cha kutumia force account kwenye miradi yetu, kwenye Kamati Serikali ililikataa pendekezo hilo na Kamati ikalazimika kuja kulileta pendekezo ndani ya Bunge na bahati nzuri pendekezo lilipita. Sasa hivi force account ndiyo inayotuwezesha kujenga vituo vya afya, hospitali zetu na miradi mingi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa lakini ilipita kwa kutumia nguvu za ziada hapa na sasa hivi tumesahau ilipitapitaje lakini manufaa makubwa tunayapata kwa kwa kutumia force account ambayo ilipita kwa shida sana ndani ya Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna taasisi na kodi nyingi katika biashara zetu. Sasa hivi ukiwa na kampuni yako unatakiwa ulipe PAYE, Workers Compensation na SDL, kwa nini hii kitu isije ikalipwa kwa wakati mmoja? Sasa hivi ukishalipa PAYE atakuja mtu wa Workers Compensation kwa wakati wake, atakuja mtu wa SDL kwa wakati wake, atakuja OSHA kwa wakati wake, atakuja TFDA kwa wakati wake, yaani unasikia pressure inapanda na kichwa kinauma. Kwa nini wasije kwa wakati mmoja halafu unalipa wenyewe wakaenda kugawana huko kwa sababu kila mtu chake kinajulikana? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo ndiyo vinavyokwamisha biashara zetu na pia ndivyo vinavyokwamisha uwekezaji katika nchi yetu, ni ugumu katika ufanywaji wa biashara. Hata kuandika tu zile return za VAT kwa wakati wake, SDL kwa wakati wake, PAYE kwa wakati wake, Workers Compensation kwa wakati wake, navyo vinachosha na vinatia ugumu katika kufanya biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja lakini lile la Liganga na Mchuchuma lenyewe tutalijua kesho, ahsante. (Makofi)