Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

Hon. Hassanali Mohamedali Ibrahim

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kiembesamaki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

MHE. IBRAHIM HASSANALI MOHAMMEDALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi kwa mara nyingine kuchangia hii Wizara ya Viwanda na Biashara. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa pumzi zake mimi kusimama hapa nikiwa na afya, mzima, Alhamdulillah. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nachukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Kakunda na timu yake, kwa kweli bajeti aliyowasilisha leo ni bajeti ambayo inalenga kuwasaidia wafanyabiashara na wenye viwanda na matumaini yangu mimi ni kwamba Mheshimiwa Kakunda, katika nchi hii ya Tanzania tunawategemea sana wafanyabiashara na wenye viwanda. Wao ndiyo wanatuletea revenue kubwa sana katika nchi hii. Kama Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kila anaposimama kwenye kiriri akiwahimiza wafanyabiashara wa nje waje Tanzania kuwekeza, hii ni kwa sababu anawatakia mema Watanzania ili Tanzania iwe nchi ya viwanda tukifika 2025 na vilevile Watanzania watakuwa wanapata ajira kuongezeka katika viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka nimsaidie ndugu yangu Mheshimiwa Waziri Kakunda. Kwa kweli tatizo lililokuwepo kubwa sana kwanza kwa wenzetu wa TFDA. TFDA huwa wanachukua muda mrefu kutoa ripoti ya kile kitu ambacho kimewasilishwa kwao, wanachukua miezi mitatu. Mheshimiwa Waziri mimi ninao ushahidi. Wenzetu nchi za nje kama South Africa hapa, within 10 days wanakupa ripoti kwamba kitu hiki kinafaa au hakifai. Sasa wenzetu wa TFDA nataka wabadilike sana kwa sababu kumweka mtu miezi mitatu hujampa ripoti, kwanza unamvunja moyo kwamba asilete bidhaa na pili, vilevile unawarejesha nyuma wale ambao wanataka kuleta bidhaa katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lingine kubwa kwanza hii ada ya dola 200 kwa kila sampuli moja Mheshimiwa Kakunda kwa kweli ni nyingi sana. Naomba Wizara yako iliangalie hili suala kwa sababu mtu kwenye kontena ameleta item 20 na kila item dola 200, fanya hesabu hapa, huyo analipa kiasi gani? Kwa hiyo, badala ya kuwa-support wafanyabishara tunawa-discourage wasilete vitu nchini na wakileta vitu nchini, Tanzania inapata revenue, TRA wanakusanya pesa. Kwa hiyo, naomba TFDA wabadilike sana katika masuala haya ya haya mambo tunayokwenda nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nataka wenzetu wa TBS na ZBS washirikiane, waaminiane katika kazi hii kwa sababu mzigo unaotoka Zanzibar kuja huku kwa kweli inakuwa ni shughuli kubwa sana. Kwa sababu wafanyabishara wa Zanzibar wanapoleta vitu Zanzibar wanakuwa wameshapewa kibali kule na ZBS, sasa unapokuja huku TBS nao wanaweka mguu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri hili pia ni changamoto kubwa sana katika Wizara yako. Naomba TBS na ZBS washirikiane ili wafanyabiashara wawe wanafanya biashara kwa amani, wanatuingizia pesa, lakini hizi changamoto inatuletea vilevile sintofahamu katika Muungano wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nataka nikupe taarifa kwa sababu sisi ni watu ambao tupo mjini tukaa na wafanyabiashara. Hawa TBS wakikupa cheti cha kwamba wewe hiki kitu unaweza ukakiuza mfano, lakini wanakuja watu wa FTC wanaipinga TBS. Sasa hapo Mheshimiwa Waziri watu wanakuwa wanaonyesha mimi ni mkubwa kuliko wewe. TBS anasema sawa lakini anakuja FTC anakanusha anasema hapana, mimi sijaridhika. Sasa nani tumsikilize? Tumsikilize FTC au TBS? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema nizungumzie zaidi biashara kwa sababu nakaa na wafanyabiashara wakubwa na wadogo. Kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mpina, juzi alikagua kiwanda cha maziwa Arusha na alihakikisha kwamba hakuna kitu kutoka nje kitakuja Tanzania ili kukilinda kile kiwanda. Wewe Mheshimiwa Waziri na hilo pia ulichukue kwamba viwanda vyetu vya ndani lazima uvilinde kwa sababu ukivilinda viwanda vya ndani ndipo ajira ya Watanzania itakapopatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti na Mheshimiwa Waziri, tatizo lingine kubwa lililokuwepo ni OSHA. Nasema tena OSHA. Hawa wanakuja maofisini wanasema kwamba huu umeme haujakaa sawa, hii meza haijakaa sawa; hii feni haijakaa sawa; hivi ni kazi ya OSHA, tunauliza? Kama ni kosa la umeme au nini, ni la mwenye nyumba mwenyewe aliyejenga siyo yule aliyekodi; na ushahidi ninao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni kuna wafanyabiashara Dar es Salaam wametozwa shilingi 850,000/=, wengine shilingi 650,000/=, wengine wametozwa shilingi 420,000/=. Ninao ushahidi OSHA wamekwenda kwa sababu eti huu umeme haufai, hii meza uliyokuwa umeweka hapa siyo mahali pake, jamani hawa OSHA wanataka kutupeleka wapi? Hivi OSHA wamepewa kazi ya kwenda maofisini na kuchaji pesa nyingi kiasi hicho? Mheshimiwa Waziri, ushahidi pia ninao ukitaka, nazungumza haya kwa ushahidi.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri Kakunda kwa sababu upo na Mheshimiwa Kairuki kwa sababu ni Waziri wa Uwekezaji, atakusaidia sana Mheshimiwa Kairuki kukuletea wawekezaji, lakini suala la wawekezaji kupata kibali cha kufanya kazi nchini, naomba hili ulibebe kwa sababu kuna malalamiko mengi sana. Kuna watu wanaenda ku-apply labor hawapati, wanahangaishwa, nenda rudi, nenda rudi. Kwa hiyo, nakuomba Mheshimiwa Waziri Kakunda, hili suala uliangalie kwa sababu kuna watu wamekuja wanawekeza hapa, Watanzania wanapata ajira lakini mwisho wa siku hawapati kibali cha kufanyia kazi. Kwa hiyo, nani anapata hasara? Ni wale Watanzania wanakuwa wanakosa ajira kwa yule mtu mmoja ambaye amekosa labor.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hili Mheshimiwa Waziri ulibebe sana. Nami ukitaka ushahidi wa mambo yote nitakuletea ofisini kwako. Tupo hapa kuwajenga Watanzania ili nao wapate kazi. Masuala haya ya nenda rudi haituletei sifa Tanzania. Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli anahangaika nchi nzima, anasema wawekezaji njoo, jengeni, fanyeni lakini kuna watu makusudi wanamkwamisha Mheshimiwa Rais. Hatukubali! Tunasema tena, hatukubali sisi! Mheshimiwa Rais anakufa na nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Kakunda mimi hayo nilitaka niyaweke wazi na vilevile naomba Manispaa zetu watenge nafasi ili mashine/viwanda vidogo vidogo wajasiliamali wetu wapate kuwekeza kama nchi zetu za China na India, kuna Manispaa wamewekeza nafasi maalum kwa viwanda vidogo vidogo kwa vijana wetu ili nao wachangie hii fursa ya biashara ya Tanzania ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na nimshukuru tena Mheshimiwa Waziri Kakunda kwa kuwasilisha hotuba yake hii nzuri. Naunga mkono hii hoja mia fil-mia na Inshallah Mungu atatusaidia. Naitakia kila la heri nchi yetu ya Tanzania, nchi ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana nakushukuru. (Makofi)